WIKI iliyopita Rais Uhuru Kenyatta alikuwa mbogo, akiwakashifu vikali wanasiasa wanaofanya siasa katika suala la ripoti ya jopo kazi ya Building Bridges Initiative (BBI) hata kabla Wakenya hawajaisoma.
Ripoti hiyo ya BBI ilizinduliwa hivi majuzi jijini Nairobi, huku viongozi mbalimbali wa siasa wakiisifu na kuwataka Wakenya kuisoma, lakini siku chache baadaye malumbano yaliibuka kuhusu ni njia ipi bora itumike kuipitisha.
Akionekana mwenye hasira wakati wa uzinduzi wa Hospitali ya Kanisa Katoliki Mangu iliyopo Gatundu Kaskazini, Rais Uhuru aliwataka viongozi wa siasa kuacha malumbano na badala yake kuwatumikia Wakenya wote.
Anasema dhumuni la ripoti ya BBI ilikuwa ni kuwaunganisha Wakenya na kuwalaumu wanasiasa wanaoeneza chuki na kuwagawa Wakenya kwa maslahi yao binafsi.
“Wanadhani mimi ni mjinga kwa sababu kabla ripoti hii haijawekwa wazi kwa umma, walikuwa wanazunguka nchi nzima kwa mwezi moja kusababisha taharuki isiyokuwa na maana. Na sasa ambapo tumeshatoa ripoti, wao wanaelekeza Wakenya njia ambayo si sahihi. Ni watu waliochanganyikiwa na hawana mwelekeo,” anasema Rais Uhuru.
Ripoti ambayo miongoni mwa lengo lake lilikuwa ni kutatua uhasama wa kikabila, imeshaanza kuzua hali ya joto la kisiasa linalotishia kuigawa nchi.
Tayari wachambuzi wa siasa wanadai kuwa Rais Uhuru na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, wapo upande moja wa namna gani ripoti ya BBI inahitajika kutafsiriwa kikatiba wakati Naibu Rais William Ruto na washirika wake wakiwa na mawazo tofauti.
Siku moja baada ya ripoti ya BBI kuzinduliwa, Raila na baadhi ya wanasiasa walipendekeza kufanyika kura ya maoni huku wanasiasa wanaogemea hususan kutoka kambi ya Ruto wakipendekeza Bunge ndiyo ipewe mamlaka ya kujadili na kupitisha au kuitupilia mbali ripoti hiyo.
Hata hivyo, kundi hili la pili limepata pigo baada ya Spika wa Bunge la Taifa, Justin Muturi, kupinga Bunge kutumika kutoa hatima ya ripoti ya BBI ikiwa ni ishara kwamba ripoti hiyo huenda ikalazimika kupigiwa kura ya maoni.
Akizungumza wakati wa uchangishaji fedha za kanisa eneo la Bunge la Uriri iliyopo Kaunti ya Migori, Muturi anasema ripoti hiyo ni mali ya wananchi ambao lazima wawe na neno la mwisho kuhusu utekelezaji wake.
“Haina njia ya kupitia kuja bungeni. Wacha ibaki huko na wananchi. Unajua kabla ya kufika bungeni lazima niidhinishe lakini nimesema (ripoti) ni ya watu na haina njia ya kupita bungeni,” anasema Spika Muturi ambaye alikuwa mgeni wa Mbunge wa jimbo hilo, Mark Nyamita, na Seneta Ochillo Ayacko huku viongozi wengine wakiwa Mwenyekiti wa ODM, John Mbadi, Seneta wa Nyamira, Okong’o Omogeni, na wambunge Tim Wanyonyi (Westlands) na Maisora Kitayama (Kuria East).
Spika Muturi alikariri ushauri wa Rais Uhuru wa kuwataka Wakenya kusoma ili kujua nini ni kizuri na maeneo yapi ya kuboreshwa.
Hofu ya Spika endapo ripoti ya BBI itaachiwa Bunge kuamua, itakiuka Kifungu cha 10 ya Katiba kuhusu ujumuishwaji wakati wanaopaswa kufaidi zaidi ripoti hiyo ni wananchi.
Hata hivyo, mshirika wa karibu na Naibu Rais ambaye ni Kiongozi wa Waliowengi Bunge la Seneti, Kipchumba Murkomen, anasisitiza Bunge ndiyo njia sahihi na maeneo yenye utata tu yatakayozua mjadala bungeni ndiyo yanayopaswa kupelekwa kwa umma ili kupitishwa kupitia kura ya maoni.