30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

REA, NBS kufanya utafiti umeme vijijini ni mwafaka

tanesco

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zinafanya utafiti utakaobaini takwimu sahihi za upatikanaji wa nishati ya umeme katika ngazi mbalimbali nchini.

Tunasema tangu mwanzo kuwa hii ni hatua muhimu na sahihi kuweza kujua mahitaji ya umeme vijijini kwa sasa na vijiji vile ambavyo tayari vimekwisha kupata huduma hiyo.

Kwamba Serikali imeanza kufanya utafiti wa kuangalia upatikanaji wa nishati Tanzania, hususan katika maeneo ya vijijini mwaka huu, utafiti ambao utafanyika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara kuanzia Oktoba 10 hadi Novemba 15, mwaka huu.

Kwamba sambamba na ukusanyaji wa takwimu hizi, utafiti huu utahusisha ukusanyaji wa takwimu za kidemografia na za kiuchumi za wanakaya; zikijumuisha umri, jinsia, hali ya ndoa, elimu, shughuli za kiuchumi, matumizi ya muda na ushiriki wa jinsia zote katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Kwamba tangu kuanzishwa wakala huo mwaka 2007 uliolenga kuboresha hali ya maisha ya wakazi wa vijijini, jumla ya vijiji 4,497 miongoni mwa 12,268, sawa na asilimia 37, vimepata umeme, ikilinganishwa na hapo awali ambapo ni vijiji 400 pekee vilivyokuwa na umeme.

Kwamba katika kuhakikisha wanafanikiwa katika hilo, Serikali imeongeza bajeti ya wizara hiyo kutoka bilioni 11.6 mwaka 2007 hadi kufikia bilioni 587.6 mwaka huu, hii ikiwa karibu mara 50 zaidi.

Jumla ya maeneo 676 ya vijijini na mijini yaliyochaguliwa kitaalamu katika mikoa yote 26 ya Bara yatahusika, zikiwamo kaya binafsi zipatazo 10,140.

Tunaweza kusema kuwa hili ni wazo zuri katika kuimarisha nishati ya umeme nchini. Tunasisitiza kuwa, huu ni mwendelezo wa juhudi za Serikali kuimarisha matumizi ya umeme nchini.

Akizungumza mwanzoni mwa Februari, mwaka huu na wazalishaji wa umeme wa maji ambao wanataka kuzalisha umeme, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter  Muhongo, aliitaja miradi kadhaa ambayo ni pamoja na uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali, maji, upepo, jua, nishati  jadirifu, makaa ya mawe na mawimbi ya bahari.

Kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kutafuta fedha ili kuendeleza miradi hiyo ambayo wananchi wameamua kuisimamia, kwani wawekezaji hawa sasa watakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme.

Kwamba ili kufanikisha suala hilo, lazima wanaotaka kuzalisha umeme wa maji chini ya megawati 20, wahakikishe wanaandika na kuwasilisha wizarani mapendekezo yanayochanganua miradi wanayotaka kuanzisha.

Profesa Muhongo alisema tayari Serikali ilikuwa imeshaanza majadiliano na taasisi za fedha kama Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Dunia (WB) na nchi wahisani kupata fedha za kuendeshea miradi mbalimbali ya umeme.

Kwa umeme unaozalishwa nchini kwa sasa, Serikali inatumia vyanzo mbalimbali, ikiwamo gesi asilia, maji na mafuta mazito.

Tunatoa pongezi kwa Serikali na pia kwa Profesa Muhongo kwa kuliona hili la umeme na kuamua kulisukuma mbele.

Tukumbuke kuwa, umeme ndio chanzo cha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali viwandani na kuwezesha kuwapo kwa huduma lukuki za kijamii.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles