27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

RC Mwanza awataka wananchi kuiamini Serikali kuhusu chanjo

Na Clara Matimo, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ameongoza wakazi wa jiji hilo kupata chanjo dhidi ya UVIKO- 19 katika uzinduzi wa kimkoa uliofanyika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekoutoure.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, akichanjwa chanjo dhidi ya UVIKO-19  inayokinga  maambukizi ya virusi vya korona, ikiwa ni uzinduzi wa chanjo hiyo  mkoani  humo leo uliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekoutoure,  nyuma yake ni Mganga  Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk.Bahati Msaki akishuhudia. Picha na Clara Matimo.

Akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa chanjo hiyo, Mhandisi Gabriel amesema mkoa huo umetenga vituo 27 vya kutolea chanjo na kuwataka wananchi kuiamini Serikali kwa kujitokeza kuchanjwa kwa sababu  chanjo hiyo ni  salama  kama ingekuwa na madahara isingeiruhusu kuingia nchini na raia wake kuitumia bali lengo lake ni kuwakinga na maambukizi ya  virusi vya korona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

 “Mwenyezi Mungu anawatumia sana wataalamu wa masuala ya afya,  Ukimwi ulipokuja uliuwa watu sana lakini wataalamu wa afya waliingia maabara wakaleta dawa za kufubaza virusi hivyo,  sasa hivi watu wanaishi kama vile virusi havipo, polia pia ilitupa shida watu walikuwa walemavu,  Mungu akawatumia wataalamu wa afya wakagundua chanjo ikaja nchini na wengi tumechanjwa tukawa salama .

“Na walioleta chanjo ni hao hao lakini Mungu ameendelea kutuhifadhi, nawaomba imani yetu isitindike kwenye changamoto hii wala tusiwasikiliza wanaotutia hofu, lakini pamoja na  uwepo wa chanjo  niwasihi wakazi wote wa Mkoa wa Mwanza muendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo, maana chanjo inakusaidia kupambana na dalili za ugonjwa  wa Covid-19 tuendelee kunawa mikono  mara kwa mara kwa maji tiririka, tutumie vitakasa mikono na tuepuke msongamano usio wa lazima pia tuvae barakoa,”amesisitiza  Mhandisi Gabriel.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  Dk. Thomas Rutachunzibwa, amesema Mkoa wa Mwanza umepokea dozi 90,000,  wataanza na makundi  matatu ambayo ni watumishi wa sekta ya  afya maana wao muda mwingi wanakuwa karibu na wagonjwa hivyo wako kwenye hali hatarishi ya kupata ugonjwa huo,  watu wenye umri kuanzia miaka 50 na kuendelea kwa kuwa wao wakipata ugonjwa wa corona wanapata madhara makubwa na wenye magunjwa sugu kama kisukari,  saratani shinikizo la juu la damu na seli mundu.

“Chanjo tulizozipokea ni chache  na ni dozi moja tu ukichanjwa mara moja umemaliza lakini hazitoshelezi wakazi wote wa Mkoa wa Mwanza,  haya makundi ambayo tumeyapa kipaumbele yajitokeze yapate chanjo lakini nawaasa wananchi waendelee kujiandikisha ili tutakapoagiza awamu ya pili tupate zinazoendana na mahitaji  yetu, hii ni awamu ya kwanza lakini tunashukuru mwitikio ni mzuri,”amesema.

Mganga Mfawidhi Hospitali ya Sekoutoure, Dk.Bahati Msaki, amesema pamoja na kwamba chanjo hizo wamezipokea leo asubuhi lakini watumishi zaidi ya 200 wameishajiorodhesha  kwa ajili ya kuchanjwa na bado zoezi la kujiorodhesha linaendelea ambapo pia amewasisitiza wananchi kuchangamkia fursa hiyo inayotolewa  bure na Serikali ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Uhuru iliyopo jijini hapa Dk. Derick Nyasebwa, ambaye ni miongoni mwa wananchi waliochanjwa amesema ameamua kuchanjwa kwa sababu chanjo hiyo ni salama na imethibitishwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)  ambayo inaviwango vya  nyota tano pia utendaji wake na ubora wake umethibitishwa na Shirika la Afya Duniani(WHO).

“Mimi ni daktari niwaambie tu ukweli kwamba wodini ninawagonjwa   wa ugonjwa huo na kwa sababu madhara ninayoyaona kwa wagonjwa hata kama wakipona  wengi wao mapafu yao yanakuwa yameharibika  kabisa na yanaweza yasirudi katika hali yake ya awali kwa hiyo  nawashauri watanzania wasitie mashaka chanjo ni salama.

“Maneno yanayoongelewa na watu mbalimbali kwenye mitandao  ya kijamii ambao baadhi yao hawana elimu ya masuala ya afya kwamba  mtu akichanjwa anaweza akapata matatizo baada ya miaka 10 tunasema hizo ni hisia lakini kitaalamu hakuna uthibitisho wowote kwamba chanjo hii itakuja kuleta matatizo kwa siku za mbele,”amesema na kuongeza

“Leo namshukuru Mungu nimekuwa miongoni mwa watanzania ambao wamepata chanjo  ya kujikinga dhidi ya janga la virusi vya korona,  nadhani waandishi wa habari mmenishuhudia nawasihi na nyie mchanjwe ili mjikinge na muwakinge muwapendao,”amesema Dk Nyasebwa.

Mmoja wa waandishi wa habari ambaye naye amepata chanjo hiyo,  Kisali Simba, ameishukuru Serikali kwa kutoa bure chanjo kwa wananchi wake pia amewashauri  waandishi wengine watumie fursa hiyo ya kujikinga kwani  kinga ni bora kuliko tiba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles