Ashura Kazinja, Morogoro
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare, amesema hawezi kufanya kazi na mtumishi asiyewajibika na kuwataka watumishi hao kutafuta sababu inayochelewesha maendeleo ya mkoa huo.
Sanare aliyasema hayo jana mkoani hapa wakati akizungumza na watumishi wa ofisi ya Mkoa wa Morogoro, ikiwa ni sehemu ya kujitambulisha rasmi kwa watumishi na kuweka mikakati ya namna ya kufanya kazi.
Alisema hayuko tayari kufanya kazi na watumishi wasio jituma wala kuwajibika na kama wapo watumishi kama hao, ni bora wakachukua uamuzi kuondoka kazini.
“Sitokuwa tayari kufanya kazi na mtumishi asiyetuma, kama unajiona huwezi kufanya kazi ipasavyo ni vema ukachukua kilicho chako na kuwpisha wengine wanaoweza kuwajibika ipasavyo” alisema Sanare.
Aliwataka watumishi hao kusaidia katika kutafuta kiini cha tatizo linalochelewesha maendeleo ya mkoa huo, na kuwataka wataalamu kuwasilisha kwa wakati taarifa muhimu zinazotakiwa zimfikie ili zisaidie kupatikana kwa ufumbuzi juu ya changamoto zilizopo.
Aliwataka watumishi hao wajibu wao wa kwanza uwe kuwahudumia wananchi kwa kuwa ni wajibu wao kuwatumikia na kuhakikisha wanapata maendeleo na kuondoa changamoto zinazowakabili.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Kalobelo, aliwataka watumishi hao kuwajibika na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyotolewa na serikali.
Alisema muda umefika sasa kwa watumishi hao kubadilika na kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa ufanisi ili kuendana na mabadiliko yenye lengo la kufanya mageuzi katika mkoa huo.