Clara Matimo, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adama Malima anatarajiwa kuzindua wiki ya madini kesho Aprili 4, 2023 inayofanyika kitaifa mkoani humo kuanzia Mei 3 hadi 10, mwaka huu 2023.
Hayo yameelezwa leo Mei 3 na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania(FEMATA), John Bina jijini Mwanza alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wiki ya madini, mkutano mkuu wa shirikisho hilo na kongamano la wachimbaji wa madini Tanzania.
Kwa mujibu wa Bina Mei 9 mwaka huu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi kwenye kongamano la wachimbaji wa madini na Mei 10, Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko atafungua Mkutano mkuu wa FEMATA utakaowakutanisha wajumbe 182 lengo likiwa ni kuunda timu ya kitaifa itakayoshauriana na serikali kuhakikisha soko la madini la Afrika linakuwa hapa nchini.
“Kongamano hilo litawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini kutoka ndani na nje ya nchi, litaambatana na mambo tofautitofauti ikiwemo maonesho ya teknolojia za kisasa za uchimbaji madini yatakayofanyika viwanja vya Rock City Mall hapa jijini Mwanza kisha usiku tutakuwa na usiku wa madini ambao utaambatana na kutoa tuzo za aina mbalimbali kwa watu walioshirikiana vyema na FEMATA katika kufanikisha shughuli za uchimbaji na waliolipa tozo na kodi zao vizuri serikalini.
“Washiriki wa wiki ya madini na kongamano la madini ni watu wote waliopo katika mnyororo wa thamani wa madini ambao watajadili mada mbalimbali wakilenga kauli mbiu ya maadhimisho ya wiki ya madini kitaifa mwaka huu 2023 isemayo ‘Amani iliyopo Tanzania Itumike Kuwa Fursa ya Kiuchumi na Tanzania Kuwa Kitovu cha Biashara ya Madini Afrika’,”amesema Bina.
Ameeleza kwamba wachimbaji kutoka nchi mbalimbali za Afrika watashiriki kongamano hilo ili kupeana elimu lengo likiwa ni kumaliza matumizi ya zebaki ifikapo mwaka 2030 ambayo ndiyo nia ya serikali.
“FEMATA tunampongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia royal tour watalii wameongezeka katika madini yetu ya Tanzanite tutumie amani iliyopo kukuza uchumi wetu,”amesema Rais huyo wa FEMATA.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Uhandisi TIES, Mhandisi Josia Komogo amesema ili kuwalinda wachimbaji wadogo dhidi ya athari zitokanazo na zebaki kampuni yake imeanzisha teknolojia ya CIL inayochenjua dhahabu kwa bei nafuu pia inaongeza uzalishaji maana inaondoa dhahabu yote katika udongo.
“Teknolojia ya CIL inatija sana kwa sababu inapunguza pia muda wa uzalishaji kutoka zaidi ya wiki mbili kwa matumizi ya zebaki hadi takribani saa 30, nawashauri wachimbaji wetu hapa nchini kutumia teknolojia hii ili wakuze uchumi wao na taifa kwa ujumla,”amesema Mhandisi Komogo.