Na Mwandihi Wetu, Mtanzania Digital
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amekerwa na watu wanaoibeza Tanzania kuhusu utaratibu uliofanyika wa kuwahamisha wananchi katika Kijiji cha Msomera mkoani Tanga kupisha shughuli za uhifadhi kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Kauli hiyo ya RC Malima aliyoitoa mapema leo Juni 22, wilayani Pangani Mkoani Tanga, imekuja siku chache baada ya kaya 21 kuhamia kijijini hapo huku utekelezaji wa kuwahamisha kwa awamu ukiendelea.
Amesema anashangazwa na watu hao ambao hawaitakii mema Tanzania kwa kuichafua serikali yake na namna inavyotekeleza majukumu yake.
“Nchi yetu inachafuliwa na watu wachache lakini yote hii ni sababu ya njaa. Haiwezekani Mtanzania anayeipenda nchi yake akachukia zoezi la kuinusuru Ngorongoro. Sisi tunainusuru Tanzania yetu kwa ajili ya mapato na faida ya Tanzania yetu kwa ajili ya vizazi vya Tanzania ijayo watu wanufaike.
“Kama wale watu wa Ngorongoro ambayo imeanzishwa miaka 64 iliyopita wasingetenneneza mikakati ya kuinusuru miaka ile sisi tungeiona wapi. Sisi tunatengeneza mikakati ya kuinusuru Ngorongoro miaka mingine 60 na Watanzania wanufaike na uwepo wake,” amesema Malima.
Pamoja na mmbo mengine, Malima amesema kwa mtindo huo dunia inakokwenda kuna siku itafika binadamu wa kawaida hataona tembo, twiga, simba, nyati hadi wawe kwenye maeneo maalumu ambayo Tanzania itakuwa nayo.
“Kama leo waarabu wanavyojivunia mafuta kuna wakati watu watajivunia utalii wa wanyamapori kwa sababu dunia nzima itakuwa hakuna,” amesema.