Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
MWILI wa binadamu unazo chembe chembe hai za damu ambazo zimegawanyika katika aina kuu tatu, nyeupe, nyekundu na sahani (mgando).
Kwa kawaida, chembe chembe hai za damu huzalishwa katikati ya mifupa yake na kila aina ina kazi maalumu ndani ya mwili.
“Kazi ya chembe chembe nyeupe za damu ni kulinda mwili dhidi ya magonjwa, chembe chembe nyekundu kazi yake ni kusambaza hewa ya oksijeni ndani ya mwili wakati chembe sahani zenyewe husaidia damu kuganda pale anapokuwa amepata jeraha,” anasema.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Emmanuel Lugina, anasema saratani ya damu ni mabadiliko ya chembe chembe hai za seli za damu.
Anasema mabadiliko hayo yanapotokea husababisha kuzalishwa kwa wingi kwa chembe chembe hizo mwilini, hali hiyo husababisha kushindwa kufanya kazi yake sawa sawa.
“Yaani hushindwa kulinda mwili, dhidi ya magonjwa, kusambaza oksijeni inavyopaswa na kule kuganda kwa damu kunakuwa si kwa ufanisi,” anasema.
Dk. Lugina anasema hadi sasa haijulikani chanzo cha saratani hiyo na kwamba vipo visababishi vinavyotajwa kusababisha mtu kuugua.
“Pamoja na hayo, ni saratani inayotibika hasa inapogundulika mapema na mtu anaweza kujikinga kwa kuzingatia mtindo bora wa maisha,” anabainisha.
Visababishi
Dk. Lugina anasema ingawa hadi sasa haijajulika nini hasa ni chanzo cha saratani hiyo hata hivyo, vipo visababishi vingi vinavyotajwa kuchangia mtu kuugua.
“Mtu anaweza kupata saratani hii kutokana na matibabu ya mionzi kama X-rays. Aidha, wakati wa vita kuna taifa kubwa liliwahi kurusha mabomu katika nchi fulani baadae katika nchi hiyo wakapatikana watu wengi wenye saratani hii.
“Dawa za saratani (chemotherapy) ingawa zinatumika kutibu lakini baada ya miaka 10 au 15 wapo watu ambao huweza kuugua saratani hii (lakini si wote), kuvuta sigara, unywaji pombe nazo zinaweza kuchangia,” anabainisha.
Anasema kisababishi kingine kinaweza kuwa ni matatizo (mabadiliko) yanayotokea katika vinasaba vya mwanadamu mwenyewe.
“Kwa mfano, watoto wanaozaliwa na wanawake wenye umri mkubwa huwa kwenye uwezekano wa kupata hali ya ulemavu (down syndrome), na baadae huwa katika hatari ya kupata saratani ya damu.
“Kazi tunazofanya ambazo zinatufanya tukutane na kemikali mara kwa mara, kama petroli, mafuta, rangi za nyumba, ‘polish’ za mbao, dawa za kuua wadudu, huweza kutusababishia pia kupata saratani hii.
“Hivyo, ikiwa mtu anafanya kazi inayokuweka karibu na kemikali mbalimbali mara kwa mara anapaswa kuwa makini kwani anaweza kuishia kupata saratani ya damu.
“Hapa ORCI kwa mwaka tunapokea takribani wagonjwa 60 wenye saratani ya damu, hasa watu wazima, hii ni sawa na asilimia moja ya wagonjwa wote tunaopokea kwa mwaka,” anasema.
Anasema kwa kawaida mwili wa binadamu unapokuwa ‘unakutana’ na kemikali mara kwa mara, kemikali hizo huenda kuharibu vinasaba vyake na hatimaye kusababisha saratani ya damu.
“Kimsingi, saratani ya damu huathiri chembe chembe za damu ambazo zimegawanyika katika aina kuu tatu ambazo ni chembe chembe hai nyeupe, nyekundu na sahani (mgando),” anasisitiza Dk. Lugina.
Dalili
Anasema dalili hutokana na namna ambavyo zile chembe chembe hai za mwili zinashindwa kufanya kazi yake sawa sawa.
“Yaani, ikiwa chembe chembe nyeupe hazifanyi kazi vizuri mtu hupata magonjwa na homa za mara kwa mara, ikiwa chembe chembe hai nyekundu hazifanyi kazi mtu huchoka mara kwa mara, hubanwa pumzi na kupata upungufu wa damu kwa sababu damu yake huwa chache mwilini.
“Ikiwa chembe mgando (sahani) ndizo ambazo hazifanyi kazi sawa sawa mtu atajipata hata akipata jeraha dogo au aking’oa jino anavuja damu kwa wingi, haigandi au kwa wakina mama akipata hedhi damu huwa inatoka kwa wingi na hata wengine kupata upungufu wa damu,” anasema.
Anasema kwa kawaida chembe chembe hizo huzalishwa katikati ya mifupa ya mwili wa binadamu, na kwa kuwa uzalishaji wake kwa mtu mwenye saratani huwa ni wa kiwango kikubwa kuliko inavyopaswa.
“Hali hiyo husababisha muhusika kupata maumivu makali ya mifupa yasiyo ya kawaida na wengine huvimba bandama zao,” anasema.
Dk. Lugina anasema zipo saratani za damu za aina mbili ambapo kuna inayowapata watoto kitaalamu inaitwa ‘acute leukemia’ na zipo za ile inayowapata watu wazima ‘cronic leukemia.’
Anasema kwa upande wa watoto mara nyingi huanza ghafla lakini kwa watu wazima huchukua muda mrefu kuonesha dalili.
“Mtoto mwenye saratani asipopatiwa matibabu mapema anaweza kupoteza maisha haraka, ni hatari zaidi kuliko kwa upande wa watu wazima,” anasema.
Anaongeza; “Hapa ORCI kwa mwaka tunapokea watu 60 wanaokabiliwa na saratani ya damu, hii ni sawa na asilimia moja ya wagonjwa wote wa saratani tunaowapokea.
“Wengi ni watu wazima, watoto huwa wanafikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kule kuna kitengo chao maalum,” anasema.
Uchunguzi
Anasema ili kufanya uchunguzi huwa wanachukua damu ya muhusika na kuipeleka maabara ambako hutenganisha kitaalamu zile chembe hai na kuanza kuzichunguza.
“Tukishabaini tunaanza matibabu mara moja, huwa ni ya muda mrefu kama miaka miwili hadi mitatu, watoto wa kiume huchukua muda zaidi kwa sababu wakati mwingine saratani huweza kujificha kwenye korodani,” anasema.
Matibabu
Dk. Lugina anasema katika nchi zilizoendelea saratani hiyo hutibika kwa kiwango cha asilimia 90 lakini hapa nchini wana uwezo wa kutibu kiwango cha asilimia 50.
“Changamoto kubwa ni kwamba hatuna uwezo wa kutoa zile tiba za ziada kwa mfano mtoto akiwa na maambukizi ya bakteria, virusi au akiwa na upungufu wa chembe sahani, huwa hatuna za kutosha kumuongeza.
“Hivyo, hupata upungufu wa damu, au hutokwa damu kwa kiasi kikubwa hali inayoweza kusababisha kifo, hizo chembe huwa tunazipata watu wakichangia damu, zinatenganishwa kitaalamu kwenye maabara,
“Lakini ni changamoto kupata kwani benki zetu za damu zinapata kiwango kidogo kulinganisha na mahitaji, watoto ndiyo ambao huhitaji zaidi kuongezewa damu kuliko watu wazima,” anasema.
Kinga
Daktari anashauri watu kupunguza ama kuacha kabisa uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, kufanya mazoezi na kuzingatia ulaji unaofaa ili kuepuka saratani.
“Ni vema pia kuchunguza afya mara kwa mara kwani itasaidia kugundulika mapema kama mtu anaugua saratani aina yoyote ile na kupewa matibabu kwa haraka,” anasema.
Anasisitiza: “Saratani haiambukizwi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine, hivyo watu wasiwanyanyapae wagonjwa, huwezi kupata saratani kwa kula au kulala na mgonjwa.
“Ni muhimu pia wazazi kuwachunguza watoto wao na kuwawahisha hospitalini kwa uchunguzi pale wanapoona mabadiliko wasiyoyaelewa, kwa mfano kutoka damu pasipo kuganda.
“Wito wangu pia kwa wakulima, wapaka rangi majumbani, ‘polish’ kwenye mbao na makundi mengine ambayo hulazimika ‘kukutana’ na kemikali mbalimbali kila siku ni vema wavae vifaa vya kujikinga ili kuepukana nazo,” anashauri.