Na HENRY PAUL- DAR ES SALAAM
KLABU ya Tiger ya Mbeya ni miongoni mwa timu inayokumbukwa na wapenzi wa soka nchini kutokana na kucheza soka safi na la uhakika wakati inashiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu) katika miaka ya 1990.
Ubora na umaarufu wa klabu hii ulitokana na viwango vikubwa vya wachezaji walivyokuwa navyo ambapo mmoja wa wachezaji aliyechezea timu hiyo katika miaka hiyo ambaye wapenzi wa soka nchini na hasa wa Mkoa wa Mbeya si rahisi kulisahau jina lake ni kipa mahiri, Ramadhani Lulandala.
Nyota huyo baada ya kustaafu kucheza soka ya ushindani mwaka 1998, aliamua kujikita katika kazi ya ujasiriamali na kilimo cha mahindi na mpunga shughuli ambazo kwa kiasi kikubwa zinamwezesha kupata kipato cha kujikimu yeye na familia yake.
Mkongwe huyo pamoja na kujishughulisha na kazi hizo, lakini kwa sababu yeye ni mdau mkubwa wa mchezo huu wa soka, hivyo bado anaendelea kuufuatilia kwa karibu na hivi sasa yeye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na pia ni Mjumbe wa Kamati ya Ufundi wa Chama cha Soka Wilaya ya Mbeya.
Hivi karibuni SPOTI KIKI ilikutana na mstaafu huyo wa soka na kufanya naye mahojiano kuhusiana na mambo mbalimbali ya soka yanayojiri hapa nchini kwa hivi sasa akiwa kama mdau mkubwa wa mchezo huu na kama ilivyotazamiwa hakusita, bali alitoa ushirikiano mkubwa.
Katika mahojiano hayo, Lulandala pamoja na mambo mengine anashauri klabu zetu nchini kuwekeza soka kwa vijana wenye umri mdogo na kuachana na kuwategemea wachezaji wenye umri mkubwa.
“Kwa muda mrefu sasa kiwango cha soka letu kimekuwa hakipandi moja ya sababu ni klabu zetu kuendelea kukumbatia wachezaji wenye umri mkubwa badala ya kuweka mkazo katika kuwekeza soka kwa vijana wenye umri mdogo.
“Kuwekeza soka kwa vijana wenye umri mdogo ndiyo njia pekee na sahihi ambayo kwa kiasi kikubwa inawezesha kuinua kiwango cha soka kwa klabu na nchi husika kwa ujumla.
“Nchi nyingi duniani zilizoendelea kisoka zimefika hatua hiyo kwa sababu ya kutilia umuhimu soka kwa vijana wenye umri mdogo na hii ni kwa sababu vijana wenye umri mdogo ni wepesi kufundishika na isitoshe viungo vyao bado ni vyepesi kulinganisha na wachezaji wenye umri mkubwa.
“Mfano mzuri wa kuwekeza soka kwa vijana wenye umri mdogo unaonekana katika nchi za Ulaya zilizoendelea kisoka kama Hispania, Uholanzi, Ujerumani, Brazil na Argentina.
“Nchi hizo zimefikia katika hatua hiyo ya kiwango kikubwa cha soka baada ya siku nyingi kuachana na kuwategemea wachezaji wenye umri mkubwa na badala yake kuanza kuwekeza kwa vijana.
“Hivyo basi na sisi kama tunataka kutoka hapa tulipo na kusonga mbele kisoka hatuna budi kuanza kuwekeza kikamilifu soka kwa vijana wadogo na kuachana kabisa na kukumbatia wachezaji wenye umri mkubwa.