Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amezitaka Halmashauri kutumia ofisi mpya zinazojengwa katika maeneo yao, kuboresha maeneo ya kazi na kutoa huduma bora na kutakua kwa wananchi
Akizungumza leo Septemba 25,2024 wakati akizindua jengo la ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, amesema ofisi hizo zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Madhumuni ya Serikali kujenga nyumba hizi ni kuleta mazingira mazuri kwa Maafisa wetu wanaofanya kazi ndani ya Halmashauri hizi, wito wangu ni kwamba ofisi hizi zitumike kuondoa kero za wananchi, pili Mkurugenzi Mtendaji na watumishi wote muweze kulitunza jengo hili kama lilivyo leo, kila tukija lionekane hivihivi,” amesema Rais Samia.
Ameeleza kuwa serikali imeendelea kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii, hivyo kuwataka watendaji kuweka nguvu katika kusimamia miradi ili yanayowakera wananchi yaondoke.
“Utumishi wetu mimi na nyinyi kuhudumia wanachi, sisi ni watumishi wa wananchi na sio mabwana wa wananchi, sio watawala wa wananchi, sisi ni watumishi kwa wananchi, ndio maana Serikali inashusha fedha nyingi ili zifanyiwe kazi wananchi hawa waondoshewe shida zao,” amesisitiza.