Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa sh 150 milioni kwa timu ya Taifa ya Soka kwa watu wenye ulemavu, Tembo Warriors, kuelekea michuano ya kufuzu Kombe la Dunia kupitia michuano ya Afrika (Canaf) itakayoanza kesho Novemba 27,2021, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati alipotembelea mazoezi ya kikosi hicho jana jioni Novemba 25, 2021 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema viongozi na Watanzania kwa ujumla wana imani kubwa na timu hiyo wakitumaini kuwafanya vizuri.
“Mhe Rais anafahamu mko hapa mnajiandaa kuipigania nchi na amesema nije hapa kwa niaba yake na ametoa kiasi cha shilingi milioni 150 ili kuwawezesha mfanye vizuri zaidi. Simamieni vizuri fedha hizi na mhakikishe zinatumika kama ilivyokusudiwa,”amesema Waziri Mkuu.
Naye, mlezi wa timu hiyo, Riziki Lulida ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Maandalizi amesema kwa kuwa Tanzania ni mwenyeji wa mashindano hayo ambayo yatajumuisha timu kutoka nchi 15 za ukanda wa Afrika, ni vyema timu hiyo ikaungwa mkono ili kufanya vizuri na kuwa miongoni mwa timu nne zitakazofuzu katika michuano ya dunia.
Riziki ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo na ameahidi kuwa watazitumia vyema ili kuhakikisha timu hiyo inashinda na kuleta heshima kwa Watanzania na hatimaye iweze kufuzu kushiriki michuano ya kimataifa.
Kwa Upande wake, nahodha ya timu hiyo, Steven Manumbu, pamoja na kumshukuru Rais Samia pia ametoa ahadi kuwa watajitahidi kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano hayo ili waweze kushiriki katika mashindano ya dunia ya michezo ya Walemavu.
Katika kutembelea timu hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Mabeyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu-Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda, na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam.