Anna Potinus-Dar Es Salaam
Licha ya rais Dk John Magufuli kutoa zawadi ya viwanja vya kujengea nyumba Mkoani Dodoma kwa wachezaji, viongozi wao na bondia Hassan Mwakinyo kama ishara ya kuonyesha furaha yake kwa Tanzania kufuzu kushiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika pia amempa zawadi nyingine mchezaji wa zamani wa Taifa Stars, Peter Tino.
Peter Tino ambaye ndiye alifunga goli pekee lililoiwezesha Tanzania kufuzu mashindano hayo kwa mara ya kwanza mwaka 1980 amepewa zawadi ya Sh 5milioni kwa ajili ya kumsaidia kufanyia biashara zitazomuwezesha kuendesha maisha yake.
“Kwa nafasi ya kipekee labda nimuombe Tino aje hapa mbele aseme kitu kwa ajili ya wenzake, na anaweza akatueleza changamoto maana tulikuwa tukisikia tu Peter Tino, Peter Tino,” amesema Dk Magufuli akimkaribisha kuzungumza.
Naye Peter Tino amewapongeza watanzania kwa kuivusha kushiriki Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa mara nyingine tangu mwaka 1980.
Baada ya Peter Tino kuzungumza na wananchi, Dk Magufuli alitaka kufahamu shughuli anayofanya na baada ya kumweleza akamtaka ataje kiasi cha fedha anachotaka lakini mwenyewe akataka afikiriwe na rais.
JPM: “Unafanya shughuli gani?”
Peter Tino: “Najishughulisha na uuzaji wa vifaa vya michezo?”
JPM: “Kwa hiyo wewe ulikuwa unataka nini?”
Peter Tino: “Nilikuwa nahitaji kiasi hivi?”
JPM: Kama shilingi ngapi?”
Peter Tino: “Unifikirie tu kama rais”
JPM: “Kuna katibu hapa! Ebu mtafutie shilingi milioni tano huyu mzee ili akakuze mtaji wake”.