26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

RAILA AKUTANA NA TUME UCHAGUZI

NAIROBI, KENYA


KINARA wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga jana alifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati kuhusu utata uliojitokeza kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio wa urais, Oktoba 26.

Raila alitangaza kufanya mazungumzo ya faragha ya dakika 40 na Chebukuti katika mkutano wake na waandishi wa habari nje ya makao makuu ya tume hiyo jijini Nairobi.

Alisema mazungumzo yao yalikuwa mazuri lakini msimamo wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio hadi masharti yake yatakapotekelezwa uko pale pale.

“Tumekuwa na mkutano mzuri na Chebukati lakini masharti yetu hayajabadilika,” alisema Raila.

Awali juzi Chebukati aliwaonya wagombea urais kutoingilia utendaji wa IEBC na pia aliwataka maofisa wa tume hiyo waliovuruga mchakato uchaguzi wa Agosti 8 kukaa pembeni.

Aidha alitoa wito kwa Raila na Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee kukutana naye ili kuzungumzia uchaguzi huo wa marudio.

Hata hivyo, Raila ambaye anataka wafanyakazi wa IEBC anaowashutumu kuharibu uchaguzi wa Agosti 8 waachie ngazi, amesisitiza kuwa hali iliyopo sasa haitafanikisha uchaguzi huru, haki na wazi.

“Wafanyakazi wa IEBC tuliowataja wangali ofisini, hatuna imani nao kamwe,” alisema Raila.

Akizungumzia kuhusu uwezekano wa kuketi katika meza ya majadiliano na Rais Kenyetta, alisema hatashinikiza yafanyike kwa sababau hataki kuonekana kuwa ana uchu wa kuundwa kwa serikali ya mseto kama inavyodai na Jubilee.

Katika mkutano huo ambao Raila alikuwa ameandamana na kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi alisema Rais Kenyetta anatarajiwa kukutana na Chebukati Jumatatu ijayo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mudavadi ambaye pia ni mkurugenzi wa kampeni za Nasa alisema kujiuzulu kwa Kamishna Dk. Roselyn Akombe na msimamo wa Chebukati ni mambo ambayo Nasa ilipata kuyazungumza kabla.

“Nyinyi wanahabari mkitathmini kauli ya Akombe na Chebukati, mtaona ni masuala tuliyoangazia kwenye malalamiko yetu. Matamshi ya Dk. Akombe na Chebukati yanaonesha hawana imani na kuwepo kwa uchaguzi wa huru, haki na wazi,” alisema Mudavadi.

Nasa imekuwa ikifanya maandamano sehemu mbalimbali nchini Kenya kushinikiza Mkurugenzi Mkuu wa IEBC, Ezra Chiloba pamoja na maafisa wengine wa tume hiyo kujiuzulu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio.

Wakati huo huo, Rais Kenyatta akiwa katika mkutano wa kampeni za chama chake cha Jubilee mjini Nanyuki juzi, alisema hatafanya mazungumzo yoyote na Raila na kusisitiza kuwa wananchi wa Kenya ndiyo watakaotoa uamuzi wa mwisho.

“Mimi sitaongea na yeyote, sina shida na IEBC. Nitaongea na wananchi pekee,” alisema Rais Kenyetta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles