MOSCOW, Urusi
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin, ametoa ushauri kuhusu mgogoro wa Korea Kaskazini na Korea Kusini akisema kwamba unaweza kutatuliwa kwa njia ya majadiliano na wala si kwa kivita.
Putin amesema hayo juzi wakati akiwahutubia wanachama wa Jumuiya ya Kimataifa ya Valdai na akapinga kuhusu vita dhidi ya Korea Kaskazini na akashauri kwamba nchi hiyo ni bora kushirikiana nayo katika miradi mbalimbali ili kupunguza mvutano na Korea Kusini.
Katika hotuba hiyo Rais Putin alisema vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini haviwezi kusaidia kitu chochote bali utaongeza zaidi migongano baina ya pande hizo mbili.
“Hali ni ya hatari. Ni nani anayeweza kusema ni kitu gani Korea Kaskazini wanacho na wanaficha wapi na kama ikiwekewa vikwazo itaharibu kila kitu. Kwanini tunakuwa na chaguo moja, inabidi tuwe na makubaliano na kuiheshimu nchi,” alisema Rais Putin.
Rais huyo alikwenda mbali zaidi akisema kama vikwazo vingekuwa njia mbadala basi yale makubaliano ya awali Serikali ya Pyongyang isingekuwa na mafanikio. Amesema Urusi tayari imesambaza miradi kadhaa na pia kwamba inahusisha Korea ya Kaskazini na Kusini katika miradi ya mabomba na ujenzi wa reli na mabomba.