26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Kilangi: Kuna watumishi ofisi ya AG wanatoa siri za Serikali

Ramadhan Hassan – Dodoma

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi, amesema kuna baadhi ya watumishi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wamekuwa wakitoa siri za vikao na mambo ya ndani ya ofisi hiyo.

Alisema ofisi yake itawachukulia hatua kali za kinidhamu watumishi hao kwa misingi ya maadili ya utumishi wa umma.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa wakati akizungumza katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alisema baadhi ya watumishi wamekuwa wakipiga picha ama kusambaza nyaraka za ofisi kupitia simu zao za mikononi.

Alisema watumishi wa ofisi hiyo wamepewa mafunzo kuhusiana na kutunza siri lakini baadhi wamekuwa hawazingatii sheria, kanuni taratibu na miongozo ya maadili ya utumishi wa umma.

“Kumekuwa na vitendo vya baadhi ya watumishi kutoa taarifa ambazo ni siri, kuzitoa ndani ya ofisi ni tatizo ambalo lilikuwepo, tumejitahidi kupambana nalo kwa kiasi kikubwa hali imeboreka lakini bado tunao watumishi wachache, jambo unaliamua ndani ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au mnalifanyia kazi baada ya muda mfupi unalisikia lipo nje linazungumzwa.

“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha kuwa hii ni ofisi ambayo inafanya kazi nyeti inawezekana watumishi wengi hawafahamu, lakini Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inabeba masuala nyeti na muhimu.

“Kiasi kwamba kama tuna kiwango cha utunzaji wa siri sisi ofisi yetu inatakiwa kuwa na kiwango kikubwa kuliko ofisi zingine, kwahiyo tunaendelea kupambana na hilo na hatutamvumilia yeyote ambaye atavunja utaratibu huo.

“Kwa ujumla ufanyaji wa vitendo hivyo ni ukiukwaji wa sheria, kanuni na maadili ya utendaji kazi katika utumishi wa umma, watumishi watakaobainika kufanya makosa hayo hatua stahiki za kinidhamu zitachukuliwa juu yao kwa misingi ya maadili ya utumishi wa umma,”alisema Kilangi.

Pia, alionesha kusikitishwa na baadhi ya watumishi kutumia muda wa likizo kufanya kazi kwenye ofisi zingine na kuondoka katika kituo bila ya kupewa ruhusa.

“Hii imedhihirishwa na baadhi ya watumishi kutumia muda wa likizo kufanya kazi zingine na kuondoka katika kituo cha kazi bila ruhusa.

Aidha, alisema ofisi yake ipo katika hatua za ukamilishaji wa ujenzi wa mfumo wa kieletroniki utakaotumika katika utekelezaji wa masuala yote ya kikazi kwa haraka na kwa ufanisi pindi utakapoanza kufanya kazi.

“Mfumo huu utawezesha wadau wetu wote popote walipo ndani na nje ya nchi kutumia hivyo natoa wito  kwa watumishi wote kuutumia mfumo huu pindi utakapoanza,”alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Augustino Mahiga, aliitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya kazi zake kwa kufuata kanuni sheria na taratibu ikiwa ni pamoja na  kusimamia suala la rushwa .

“Suala la rushwa sina haja ya kulizungumza sana kwani ndio kauli kubwa ya Rais wetu, tuna Rais ambaye anapambana na rushwa lakini lazima kuwe na vyombo ambavyo vinamsaidia Rais.

“Kama Rais amefanikiwa kupambana na rushwa sisi wanasheria na wengine lazima tuwe nae katika hili. Sisi wenyewe tuwe mfano na tuwe askari mstari wa mbele kati ya vyombo vyote katika kupamba na juhudi hizi Ofisi ya Mwansheria Mkuu imebeba dhamana hii.

“Hakikisheni hili mnalisimamia kwa nguvu zote kwa kuwafanya hivyo mtaiwezesha serikali kupata ushindi mkubwa,”alisema Waziri Mahiga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles