29.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Mkenda: Serikali kuja na mageuzi makubwa ya elimu nchini

*Amesema Serikali kusheherekea Siku ya Mwalimu Duniani 2023 Bukombe

*Dk. Mkenda ahaidi kujenga VETA wilaya ya Bukombe

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Imeelezwa kuwa, Serikali imepanga kufanya mageuzi makubwa katika utoaji wa elimu bora hususan katika elimu ya ujuzi wa vitendo katika Sekta ya Elimu nchini.

Hayo yamesemwa Oktoba 9, 2022 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati wa Sherehe ya Siku ya Mwalimu Duniani iliyoandaliwa na Chama cha Walimu wa wilaya ya Bukombe mkoani Geita.

Amesema, walimu wanaandaliwa vizuri katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini na kutoa mfano kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujenga madarasa zaidi ya 600 katika mkoa wa Geita na kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu ili kuweka mazingira mazuri ya ufundishaji.

Vile vile, Serikali itaweka mkakati mzuri wa elimu ili kusaidia walimu nchini kuweza kujiendeleza pamoja na kuongeza ujuzi. Ameongeza ndoto ya Serikali ni kuona mwalim anajiendeleza ili aweze kuwa mwalimu bora.

“Mwalimu akiomba ruhusa ya kwenda kusoma mpe ruhusa, mwalimu ni ufunguo wa maisha katika maendeleo ya nchi yetu, mafunzo kazini yataendelea, Serikali ya awamu ya sita imetenga bajeti kwa ajili ya kuwaendeleza walimu,” amesema Pro. Mkenda.

Aidha, Prof. Mkenda amemhakikishia Dkt. Biteko kuwa, mwaka 2023 katika kusheherekea Siku ya Mwalimu Duniani Serikali itahakikisha siku hiyo inasheherekewa Kitaifa katika wilaya ya Bukombe ili walimu wakutane kwa pamoja.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri na Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko amesema mwalimu ni msingi wa elimu na Serikali inautambua mchango wa wao katika utoaji wa elimu.

Pia, amewataka walimu waendelee kushirikiana katika shughuli zao za kila siku, wakipendana, kuthaminiana na kusaidiana wao kwa wao ili kujenga umoja.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela amempongeza mbunge wa Jimbo la Bukombe Dk. Biteko kwa kuandaa Siku ya Mwalimu Duniani kwa kuadhimishwa katika wilaya ya Bukombe.

Shigela amesema, atahakikisha mwaka 2023 tukio hilo linakuwa kubwa na kuadhimishwa katika Halmashauri nyingine za Mkoa wa Geita ili kusheherekea kwa pamoja.

Siku ya Mwalimu Duniani imeandaliwa na Chama cha Walimu wa wilaya ya Bukombe na imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles