MWANDISHI MAALUM -DAR ES SALAAM
WAGONJWA wenye matatizo ya moyo, kisukari, shinikizo la juu la damu, figo na saratani wameshauriwa kuhudhuria kliniki zao bila kukosa ili kuepuka kupata madhara ya kiafya ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha.
Rai hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza kuhusu kupungua kwa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo tangu virusi vya Corona vilipoingia nchini.
Prof. Janabi alisema hivi sasa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo imepungua kutoka 300 kwa siku hadi kufikia 50 kwa siku na wagonjwa wanaolazwa idadi yao imepungua kutoka 150 kwa siku hadi kufikia 30.
Kwa upande wa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo idadi yao imepungua kutoka wagonjwa wanne kwa siku na kufikia mgonjwa mmoja .
Wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo wamepungua kutoka kumi kwa siku na kufikia watatu.
Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema wao kama madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo hawaelewi hivi sasa wagonjwa hao ambao hawahudhurii kliniki wanatibiwa wapi.
Alisema kama mgonjwa ataogopa kwenda Hospitali kwa kuhofia kupata maambukizi ya ugonjwa wa Corona ambao ukiupata na kupona haukuachi na madhara yoyote wakati kuacha kliniki za magonjwa ambayo kama usipotibiwa yatakusababishia madhara makubwa katika mwili wako.
Alisema wagonjwa wa moyo wanatakiwa kuondoa hofu kutokana na taarifa mbalimbali wanazozipata kuhusiana na ugonjwa wa corona jambo la muhimu wafuate maelekezo ya wataalamu wa afya kwa kufanya hivyo wataweza kuepuka kupata maambikizi ya ugonjwa huo na siyo kuacha kuhudhuria kliniki.
“Wote tunafahamu kuwa kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika ulimwenguni zinaonesha wagonjwa wenye matatizo ya moyo, kisukari, shinikizo la juu la damu, figo, saratani na watu wenye umri mkubwa wa zaidi ya miaka 60 ndiyo wanaoathirika zaidi na ugonjwa wa Corona ikiwa wagonjwa hawa hawatahudhuria kliniki kama walivyopangiwa na madaktari wao wakipata maambukizi ya virusi vya corona ni rahisi kwao kupoteza maisha,” alisema .
“Wagonjwa wa moyo, kisukari, shinikizo la juu la damu, figo na saratani kama hawatahudhuria kliniki kwa kuhofia kupata maambukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Corona wanaweza kupata madhara ya kupoteza uhai, kupata kiharusi, kupoteza baadhi ya viungo vya mwili kwa mfano mguu, kupofuka macho na kupoteza nguvu za kiume lakini ukipata maambukizi ya virusi vya corona na ukapona hutaweza kupata madhara yoyote,” alisisitiza Prof.Janabi .
Prof. Janabi alisema ni muhimu wagonjwa hao kwenda Hospitali kutibiwa kwa kuwa mgonjwa akiwa na magonjwa hayo hawezi kujitibia nyumbani.
Alisema jambo la muhimu ni kufuata ushauri wa wataalamu wa afya hii ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni, kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
“Taasisi yetu inatuma ujumbe wa kuwakumbusha wagonjwa wetu kuhudhuria kliniki zao kutokana na tarehe walizopangiwa na madaktari lakini wengi wao hawaji kutibiwa.
“Ninaendelea kuwasisitiza waje kutibiwa kwani tumechukua tahadhari zote za kuhakikisha hawapati maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona wawapo katika eneo la Hospitali”,.
“Wagonjwa wanaofika kutibiwa hapa wanapimwa joto la mwili kabla ya kuanza kupata huduma ya matibabu, tumefunga mabomba ya maji pamoja na kuweka vitakasa mikono katika maeneo mbalimbali ya Taasisi yetu hii inawafanya kupata nafasi ya kunawa mikono mara kwa mara pia wanakaa umbali wa mita moja kati ya mgonjwa mmoja na mwingine,” alisema Prof. Janabi.
WALIPOKEA WAGONJWA WA CORONA
Alisema kuna baadhi ya wagonjwa walipokelewa katika Taasisi hiyo wakiwa na dalili za ugonjwa wa moyo ambazo ni kushindwa kupumua, kukohoa na kuchoka lakini baada ya kufanyiwa vipimo walikutwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona na kupelekwa katika vituo vya kuwatibu wagonjwa hao ambako wataalamu wetu wanakwenda kuwapatia matibabu ya moyo.
Kwa upande wao baadhi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo walisema tangu ugonjwa wa corona ulipotangazwa hapa nchini wanahudhuria kliniki kama walivyopangiwa na madaktari wao na wanapata huduma walizokuwa wanazipata kipindi ambacho hakukuwa na ugonjwa huo.
“Nimeanza kutibiwa na wataalamu wa Taasisi hii tangu mwaka 2008 na idadi ya wagonjwa ambao tunahudhuria hapa huwa ni kubwa ila leo nashangaa idadi ya wagonjwa ni wachache tofauti na siku za nyuma.
“Kama wagonjwa hawaji Hospitali kwa kuhofia kupata ugonjwa wa corona wasifanye hivyo waje kliniki wasiwe na hofu tarehe ya kliniki ikifika waje kwani kuna wakati unaandikiwa vipimo sasa kama hauji kwa daktari vipimo utachukuliwaje?”, aliuliza Mama Fitina Mkere mkazi wa Kigogo.