Na EVANS MAGEGE – Dar es Salaam |
VIKAO ambavyo Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli amekuwa akiviendesha kwa siku mbili mfululizo akiwa ameambatana na Makamu wake Bara, Philip Mangula, vinatajwa kupandisha presha ya vigogo ndani ya chama hicho, zikiwa zimesalia saa 24 kabla ya kufanyika kwa vikao vya juu.
Rais Magufuli ambaye katika vikao viwili ameonekana kuambatana na Mangula, kikiwamo kile cha jana alichokutana na makamu wake Zanzibar, Rais Dk. Mohamed Shein na kabla ya hapo Rais mstaafu Benjamin Mkapa juzi, alikutana pia na wenyeviti watatu wa jumuiya za CCM.
Wenyeviti hao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Raymond Mndolwa, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Gaudensia Kabaka na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Kheri James.
Vikao hivyo vya mfululizo vya Rais Magufuli vimekuja zikiwa zimesalia saa 24 kabla ya kuanza kwa vikao vya Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC) ya CCM huku kukiwa na dalili za kufanyika mabadiliko ya uongozi, lakini pia kuwachukulia hatua wanachama wake, wakiwamo wale wanaodaiwa kuiba mali za chama hicho.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa simu jana, Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo, alisema kamwe hawezi kupatwa na tumbo joto kutokana na ripoti ya uchunguzi wa mali za CCM iliyokabidhiwa kwa mwenyekiti wa chama hicho.
Alisema hawezi kukumbwa na hali hiyo kwa sababu anajua alifanya kazi yake kwa uaminifu na uadilifu zaidi.
“Mimi siwezi kuwa na tumbo joto, chochote kitakachotokea dhidi yangu sina shida kwa kuwa najua nilifanya kazi yangu kwa uaminifu na uadilifu zaidi.
“Lakini pia sitaki kuisemea kamati imeona nini, kuhusu kilichomo kwenye ripoti kitajulikana tu, kwa sasa tuacheni vikao vifanye kazi yake kwani mna haraka ya nini?” alihoji Bulembo.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa UWT, Sophia Simba, alisema hana mchecheto na ripoti ya uchunguzi wa mali za CCM kwa sababu anaamini aliiacha jumuiya yake ikiwa safi.
Alisema kama ripoti hiyo itaikuta jumuiya yake na dosari labda katika ngazi za watendaji, lakini yeye kama mwenyekiti aliondoka salama.
“UWT yangu nimeiacha safi, salama, kukitokea kasoro pengine ni mambo yao ya utendaji ofisini kama fedha, ambayo mimi nilikuwa siyagusi kabisa. Kumbuka wakati huo nilikuwa mwenyekiti, pia waziri. Kwahiyo nilikuwa mwenyekiti zaidi wa vikao, sio mtendaji,” alisema.