NAIROBI, KENYA
POLISI nchini Kenya waliwaua watu 33 katika mji mkuu wa Nairobi wakati wa ghasia na maandamano ya upinzani ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 8, mashirika mawili ya haki za binadamu yanasema.
Katika ripoti mpya ya Amnesty International na Human Rights Watch (HRW) wamesema polisi walihusika moja kwa kwa moja katika mauaji hayo.
Kuna taarifa nyingine ambazo hazijathibitishwa zinazodokeza huenda watu wengine 17 waliuawa jijini Nairobi wakati wa ghasia hizo.
Mashirika hayo mawili, ambayo yanasema kwa jumla watu 67 wameuawa na polisi kote nchini Kenya kipindi hicho, yamewatuhumu wanausalama kutumia nguvu kupita kiasi katika maeneo, ambayo ni ngome za upinzani ambako maandamano makubwa yalitarajiwa.
Aidha, yanasema utumiaji wa nguvu kupita kiasi umekuwa jambo la kawaida kufanywa na polisi nchini hapa.
“Wachunguzi wetu waligundua kuwa polisi wenye silaha wengi wao wakitokea Kikosi cha Kuzuia Ghasia (GSU) na Polisi wa Utawala (AP), walifanya operesheni maeneo ya Mathare, Kibera, Babadogo, Dandora, Korogocho, Kariobangi, na Kawangware jijini Nairobi kati ya Agosti 9 na 13,” taarifa ya mashirika hayo inasema.
“Waliwafyatulia risasi za moja kwa moja baadhi ya waandamanaji na wakati mwingine kiholela kuelekea kwenye umati,” ripoti inasema.
“Waathirika na walioshuhudia waliwaambia wachunguzi wetu waandamanaji walipokuwa wanakimbia, polisi waliwafukuzia hadi majumbani, wakavunja milango kwa nguvu na kuwakimbiza vichochoroni, wakawapiga risasi na wengine vibaya hadi wakafa.”
Mashirika hayo yanasema polisi walionyesha ukatili pia kwa wanahabari na watu wa mashirika ya haki za binadamu waliojaribu kupiga picha na video za matukio hayo, wakati mwingine wakiharibu kamera zao.
Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi George Kinoti hata hivyo amekanusha tuhuma hizo zilizotolewa na mashirika hayo akisema ni za kupotosha na zimetokana na taarifa za uongo.