GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM
CHAMA cha ACT Wazalendo kimelilalamikia Jeshi la Polisi kisiwani Pemba kuwabugudhi wanachama wake kwa kuwakamata baada ya kuhamia kutoka Chama cha Wananchi (CUF) na kubadilisha bendera za vyama hivyo.
Katika siku za karibuni kumekuwa na fukuto la siasa Zanzibar hasa kisiwani Pemba, baada ya wafuasi na wanachama wa CUF kuhamia ACT Wazalendo.
Wafuasi hao wamehamia ACT wakimfuata aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wenzake waliotangaza kujiunga na ACT Wazalendo Machi 18, mwaka huu baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa uamuzi wa kumtambua Profesa Ibrahimu Lipumba, kama Mwenyekiti halali wa CUF.
Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT -Wazalendo, Ado Shaibu, kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, alisema polisi kisiwani humo wameanza kuwakamata na kuwabugudhi wanachama wake.
Alisema mambo hayo yameanza kujitokeza baada ya ziara iliyofanywa Zanzibar na viongozi wa kitaifa wa chama hicho wakiongozwa na Zitto Kabwe, Maalim Seif na viongozi wengine wa kitaifa.
“Jana (juzi), Riziki Omar Juma na Mwinyi, waliitwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Wete na kuhojiwa kuhusu mkutano wa ndani wa ACT Wazalendo uliofanyika Machi 24, mwaka huu.
“Walituhumiwa pia kwa kupandisha bendera za ACT Wazalendo kwa takbiir Machi 18, mwaka huu na baada ya mahojiano wameachiwa huru juzi,” alisema Shaibu.
Pia alisema mwanachama wao mwingine, Khatib Kombo wa Wilaya ya Micheweni, naye aliwekwa ndani katika Kituo cha Polisi Micheweni kwa muda wa saa tatu kwa kutuhumiwa kushusha bendera ya CCM Machi 18, mwaka huu.
Alisema wapenzi wa chama hicho, Shame Kombo na Ali Nasoro wa Kijiji cha Shumba Mjini, walikamatwa na polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Machi 27, mwaka huu kwa tuhuma za kushusha bendera ya CCM usiku wa Machi 18, mwaka huu lakini nao pia waliachiwa huru juzi.
Akitoa msimamo wa chama hicho, alisema hawatavumilia kuona wanachama wao wakiendelea kubughudhiwa na polisi au kubambikiwa kesi.
“Mikutano yote iliyofanywa visiwani Zanzibar wakati wa ziara ya Zitto na viongozi wengine wa kitaifa, ilikuwa mikutano ya ndani, hakukuwa na maandamano wala mikutano ya hadhara, hivyo basi polisi waache kuwabughudhi watu wetu.
“Inafahamika kabisa kuwa CCM ni chama dhaifu Zanzibar, ACT Wazalendo hakiwezi kuhangaika na bendera za CCM kisiwani Pemba sehemu ambayo CCM haikupata mbunge wala diwani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na wanachama wake hawajai mkononi,” alisema Shaibu.
Alisema chama chake kinafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria, polisi na dola kwa ujumla wake viache kuwachokoza na wasiwafikishe katika kona ambayo hawatakuwa na namna isipokuwa kujihami.
Pia alisema katika ziara hiyo jumla ya wanachama wapya 125,000 walijiunga na chama hicho huku matawi yote yaliyokuwa ya CUF Zanzibar sasa yamekuwa ya chama hicho.