NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Hans Van Der Pluijm amesema hatofanya makosa katika usajili wa wachezaji kuelekea katika msimu mpya wa Ligi `Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa, kwani malengo yake ni kuona timu yake inaendelea kuwa tishio.
Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Azam katika mchezo uliyofanyika juzi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Pluijm alisema anapenda kuwa makini sana unapofika wakati wa kusajili, ili kujiepusha na lawama za wachezaji aliowachagua kushindwa kufanya vizuri.
Pluijm alisema kwa sasa ni mapema sana kuzungumzia sifa za wachezaji ambao atawapa nafasi ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao, hadi hapo kila kitu kitakapokamilika.
“Siwezi kusema sifa ambazo nitaziangalia kwa wachezaji watakaosajiliwa, ila nasubiri wakiingia makubaliano na uongozi hapo ndipo nitaweza sema vitu zaidi,” alisema Pluijm.
Mholanzi huyo alisema kwa kipindi chote ambacho ameifundisha na kuipa ubingwa klabu hiyo katika michuano ya Ligi Kuu, ameshuhudia ushindani wa hali ya juu.
“Ushindani wa ligi siyo mdogo, lazima msimu ujao tuandae kikosi imara zaidi ya hiki tulichonacho hivi sasa hapo tutafanikiwa kulitetea taji hili,” aliongeza.
Timu hiyo jana asubuhi iliondoka jijini kuelekea mkoani Mtwara, tayari kuikabili Ndanda FC katika mchezo wake wa mwisho kwa ligi utakaofanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani humo.