Na Clara Matimo, Mwanza
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma(PIC) imeridhishwa na ukuaji wa Shirika la Madini la Taifa,(STAMICO) kwa kubuni miradi mbalimbali iliyolisaidia kuliondoa kwenye hatari ya kufa.
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Vuma Augustine leo Machi 26, 2023 baada ya kutembelea na kukagua kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery( MPMR) kilichopo Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza kilichojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 16 ambapo STAMICO inamiliki asilimia 25 ya hisa.
Augustine amesema miaka michache nyuma mwenendo wa STAMICO haukuwa mzuri hali iliyosababisha PIC kuishauri serikali kulifunga lakini sasa maendeleo yake ni makubwa kutokana na uendeshaji na usimamizi mzuri.
“Wote tunafahamu kwamba mwaka 2017 kushuka chini Shirika hili lilikuwa linatengeneza hasara kubwa mpaka ilifikia kipindi PIC tulitaka kuishauri serikali ilifute maana ilikuwa ni mzigo kwake lakini sasa wameweka mikakati na wamejipanga vizuri kupitia miradi yao saizi limekuwa ni shirika ambalo linapata faida.
“Natoa wito kwa STAMICO kuendelea kubana matumizi na kufanya uwekezaji wenye tija ili waendelee kupata faida na kutoa gawio kwa Serikali, wajibu wetu ni kuisimamia serikali na mashirika yake ili kuhakikisha inafanya uwekezaji wenye tija na hatimaye yalete gawio kwa serikali,”amesema na kuongeza.
“Tunaipongeza Wizara ya Madini inafanya kazi nzuri sana kuilea STAMICO mradi huu ni mzuri sana ni wa kisasa na una tija, tumetembelea na tumethibitisha yote hayo, ushauri wetu ni kwamba migodi yote ambayo serikali inaubia au ambayo inachimba ilete dhahabu yake kwenye kiwanda hiki kwa ajili ya kusafisha pia watoe kipaumbele kwa kuwaajiri wazawa wenye sifa,”amesema Augustine.
Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko amewataka watanzania wote wanaojihusisha na uchimbaji wa madini kusafisha madini hayo kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi.
“Na huu ndiyo msukumo wetu mkubwa, tumejenga hivi viwanda si kwa kubahatisha bali viweze kufanya kazi, madini yote na dhahabu yanayochimbwa yasafishwe ndiyo yauzwe nje ya nchi, serikali imefanya kazi kubwa sana imepunguza kodi kwenye madini yanayouzwa ndani ya nchi,” amesema Biteko.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi STAMICO, Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo amesema” Tunapopata ugeni kama huu hasa viongozi kama hawa ambao wanasimamia uwekezaji katika upande wa mhimili wa bunge inakuwa ni faraja kwetu kwa sababu tunapata mawazo mapya na maelekezo.
“Tukiendelea kupata ziara kama hizi za viongozi tutaendelea kuongeza ufanisi na kiwanda hiki kitakuwa na manufaa sana, PIC imetembelea kiwanda chetu na kuona hatua zote za usafishaji dhahabu zinavyofanyika wameuliza maswali na sisi hayo maswali tunayachukulia kama maagizo tutayafanyia kazi,”amesema Meja Jenerali Mstaafu Isamuhyo.
Kiwanda cha Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR) ambacho ni kikubwa zaidi Afrika Mashariki kilizinduliwa Juni 13, 2021 na Rais Samia Suluhu Hassan kinauwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku, kinauwezo wa kusafisha dhahabu kwa asilimia 99.9(purity) ya ubora ambao ni wakiwango cha juu cha kimataifa