NA JENNIFER ULLEMBO
KOCHA mpya wa klabu ya Simba, Patrick Phiri, ametua nchini jana na kusema amekuja na malengo ya kurudisha heshima katika timu hiyo ambayo imepotea katika kipindi ambacho imekuwa haifanyi vizuri.
Phiri ni kocha mwenye historia nzuri na klabu hiyo msimu wa ligi kuu wa 2009/2010, ambapo aliweza kuisababisha timu yake hiyo kutwaa ubingwa wa ligi hiyo bila kufungwa mchezo hata mmoja.
Licha ya kuweka rekodi hiyo, lakini pia amewahi kunyakua ubingwa wa ligi kuu mara mbili akiwa na timu hiyo, ambapo pia timu yake hiyo ilikuwa mabingwa 2004/2005, baadaye aliamua kuiacha Simba kwa sababu zake binafsi na kumpa mikoba Kocha Milovan.
Akizungumza baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jana, Phiri alisema mikakati yake ataiweka wazi pindi atakaposaini mkataba na kufanya mazungumzo na uongozi juu ya kukinoa kikosi cha timu hiyo, kufuatia aliyekuwa kocha wake, Zdravko Logarusic, kufukuzwa Jumapili iliyopita.
Alisema amekuja kutokana na mwaliko aliotumiwa na Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva, hivyo watakapokubaliana na kuingia mkataba mikakati yake itaanza kujulikana.
“Nimepewa mwaliko, nimekuja kuzungumza na viongozi, ila naifahamu Tanzania, vizuri nilishafanya kazi hapa, nakumbuka wakati ule nilipoipa ubingwa klabu hii,” alisema Phiri.
Mapokezi ya Mzambia huyo yaliongozwa na wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Iddi Kajuna na Collin Fish.