- Askofu Kilaini aupinga mpango huo akihofia kanisa katoliki kudhoofika
ROMA, ITALIA
UPUNGUFU wa mapadri katika Bara la Amerika Kusini umelilazimu Kanisa Katoliki kubadili msimamo wake wa kihafidhina na kuruhusu wanaume waliooa kutoa huduma katika makanisa yake kama padri kamili.
Kiongozi wa Kanisa hilo Duniani, Papa Francis, ametoa matumaini makubwa ya kukubalika mpango huo, ambao unasubiri kupigiwa kura na Mkutano Mkuu wa maaskofu.
Inaelezwa kuwa, endapo mpango huo utapita, nchi ya Brazil itakuwa ya kwanza kwa watu waliooa kuruhusiwa kuwa mapadri, kutokana na uhaba unaiokabili nchi hiyo.
Tayari ipo taswira inayoonyesha kwamba, huenda mpango huo ukazua mjadala mkali ndani ya Kanisa Katoliki, licha ya hoja ya kukabiliana na uhaba wa makasisi katika Bara la Amerika Kusini.
Akizungumza katika ziara yake barani humo na kukaririwa na vyombo vya habari, yakiwamo magazeti ya The Independent na The Telegraphy ya Uingereza, Papa Francis alisema suala hilo linajadiliwa na baadaye kupigiwa kura na maaskofu wa Bara la Amerika Kusini, ili kutoa uamuzi wa mwisho juu ya kuwa na mapadri waliooa au la.
Kwa mujibu wa gazeti la The Telegraphy, ambalo lilinukuu chanzo cha habari cha gazeti la II Messaggero la Brazil, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki katika Ukanda wa Amazon, Kardinali Claudio Hummes, raia wa Brazil, ameripotiwa kumwomba Papa huyo kuunga mkono mpango huo, kwasababu hakuna njia mbadala ya kukabiliana na uhaba wa mapadri unaoikabili jamii katika ukanda huo.
Akisisitiza ombi hilo, Kardinali Hummes alisema kuwa, watu wasiofuata dini (wapagani) wameongezeka katika ukanda huo.
Aidha, imeelezwa kuwa, hatua hiyo itasaidia kuongeza ushawishi wa Kanisa hilo katika maeneo hayo kutokana na Ukatoliki kuzidiwa kete na makanisa ya Kiprostetanti, ambayo yamepokea waumini wengi.
MAASKOFU KUPIGA KURA
Katika kukamilisha mchakato huo, Baraza la Maaskofu litalazimika kupiga kura ili kuamua iwapo wanaume hao waruhusiwe au la.
Mkutano Mkuu wa Maaskofu wa Kanda ya Amazon utafanyika katika Sinagogi mwaka 2019 kutoa uamuzi wa mwisho chini ya Katibu wa Baraza la Maaskofu, Mhashamu Askofu Erwin Krautler.
Taarifa za ndani kutoka Vatican zinasema kuwa, mpango huo huenda utachochea ghadhabu miongoni mwa waumini na viongozi wahafidhina, ambao tayari wamekasirishwa na uamuzi wa watu waliovunja ndoa zao na kufunga nyingine kuruhusiwa kukomunika.
“VIRI PROBATI”
Mpango wa kuwachukua wanaume waliooa kuwa mapadri unajulikana kwa jina la “viri probati”, yaani “wanaume waliothibitishwa”. Unakusudia kuhakikisha wanaume wanaochaguliwa kuwa mapadri ni wale wenye imani nzuri ya dini ili kufanya kazi ya kueneza neno la Mungu.
‘Viri probati’ ni maneno yanayotoka katika lugha za Amerika Kusini. ‘Viri’ lina maana ya ‘wanaume’, wakati neno ‘probati’ likiwa na maana ya ‘thibitishwa’.
Maneno haya yamekuwa yakitumika ndani ya Kanisa hilo tangu karne ya kwanza kwa madhumuni ya kuwapima wale wote wanaotaka kuwa makasisi wa Kikatoliki.
Taarifa zinaeleza zaidi kuwa, mjadala kuhusiana na mpango wa “viri probati” umedumu kwa muda mrefu, hali ambayo uongozi wa Papa Francis umeamua kutoa kipaumbele kwa sasa pamoja na kukabiliana na nakisi ya makasisi wa Kanisa Katoliki.
KAULI YA UJERUMANI
Ikumbukwe Machi 11, mwaka huu, Papa Francis alidokeza kuwa, ipo haja Kanisa Katoliki kuanza kufikiria wanaume waliooa kuruhusiwa kuhudumu kama makasisi ili kukabiliana na upungufu wa mapadri, hususan kwenye maeneo ya vijijini.
Katika mahojiano na gazeti la Die Zeit la nchini Ujerumani, Papa Francis alisema: “Inatulazimu kufikiria iwapo watu waliooa na wana imani thabiti ya dini kama wanaweza kuwa mbadala. Kisha tufikirie namna ya kufanya kazi, hususan maeneo ya jamii za vijijini.”
Papa Francis alisema ruhusa ya wanaotaka kuwa makasisi kuamua kubaki kuwa waseja halikuwa jambo alilolipendelea, lakini alipendekeza kwamba hilo ni suala linalohitaji majadiliano zaidi.
Waumini wengi wa Kikatoliki wanaamini kwamba, kufungua njia kwa ajili ya kuwapa upadirisho wanaume waliooa kutasaidia kushughulikia uhaba wa mapadri katika baadhi ya maeneo duniani.
Pamoja mpango huo, kanisa hilo limeamua kuwa maeneo fulani maalumu yaachwe na sheria za useja, lakini pia ikielezwa kuwa, mpango wa ‘viri probati’ unatarajiwa kuenezwa sehemu mbalimbali duniani, ikiwamo barani Afrika.
Chama cha Makasisi wa Kikatoliki wa Marekani wanaohudumu katika parokia za nchi hiyo kimeupokea kwa furaha mtazamo huo, wakisema ni mabadiliko makubwa ndani ya Kanisa Katoliki.
Katika hatua nyingine, Papa Francis amesisitiza kuwa, kanuni kuu za kuwa kasisi wa Kanisa Katoliki ni nidhamu zaidi kuliko sheria zozote zinazoongoza.
ASKOFU KILAINI ATOA MTAZAMO
Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, alisema kwamba, kwa maoni yake haungi mkono watu waliooa kuwa mapadri.
Alisema kama hoja ni uhaba wa mapadri, Kanisa hilo limekuwa na uhaba mkubwa duniani kote, lakini uhaba huo umelisaidia kukua na kujiimarisha.
“Binafsi bado nasapoti kuwa na mapadri ambao hawajaoa, kwa sababu hiyo ni tunu ya Kanisa na imekuwapo kwa miaka mingi sana na kama ni hoja ya upungufu wa mapadri, tatizo hili lipo ndani ya Kanisa kwa miaka mingi, lakini Kanisa limeendelea kuimarika,” alisema.
Alisema mtazamo wa kuruhusu watu waliooa kuwa mapadri utawafanya vijana wenye wito wa upadri kuamua kuoa kwanza kisha kufuata mwito wa upadri, hatua ambayo itasababisha mapadri wote wapya wa Kanisa Katoliki kuoa.
Kilaini alipendekeza kuwa, mtazamo huo wa Papa ulenge mashemasi au kuweka msingi wa pekee kama ilivyokuwa kwa mapadri wa Anglikana ambao waliamua kujiunga na Kanisa Katoliki.
“Unajua mapadiri wa Kianglikana wanaoa, kuna walioomba kuingia katika Kanisa Katoliki na wakaruhusiwa, wakapewa mafunzo kidogo wakawa mapadri.