Na FREDY AZZAH, DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, amesema mpango wa uhakiki kwa watumishi wa umma haukuwagusa mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, kwa sababu sifa wanazotakiwa kuwa nazo ni kujua kusoma na kuandika pekee.
Akizungumza mjini Dodoma jana, kabla ya kumkabidhi Rais Dk. John Magufuli orodha ya watumishi wenye vyeti feki, Kairuki, alisema: “Uhakiki uliwahusu watumishi wa umma pekee, wakiwamo makatibu wakuu wote na viongozi mbalimbali katika ngazi ya utumishi wa umma.
“Hatua hii inatokana na ukweli kwamba, kwa mujibu wa sheria, pamoja na miundo ya maendeleo ya utumishi serikalini, wanatakiwa kuwa na sifa za msingi za kuingilia na kutumikia nafasi zao, ikiwa ni pamoja na vigezo vya elimu na vigezo vya kitaaluma, hivyo uhakiki haukuwahusisha viongozi wa kisiasa.
“Waziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya na madiwani kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, wote mnafahamu uteuzi na uchaguzi unafanyika kwa misingi ya wahusika kuwa na sifa ya kujua kusoma na kuandika.
“Na hii ni kwa mujibu wa Ibara 61(1) ya Katiba, isije ikaonekana ni maneno ya Kairuki,” alisema.
Alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa kuimarisha usimamizi na mifumo maalumu, hususan ya upokeaji wa taarifa za watumishi ili kubaini watumishi wanaotumia vyeti vinavyofanana.
“Ofisi yako imechukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi na mifumo maalumu, hususan wa kupokea taarifa, mfumo huu shirikishi umetusaidia kuweza kubaini wanaotumia vyeti vinavyofanana katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2014, tulibaini vyeti 344 kati ya 1,114 vilivyowasilishwa Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania (NECTA) vilibainika kuwa vinafanana (cheti kimoja kutumiwa na zaidi ya mtu mmoja).
“Baada ya uchunguzi kufanyika, watumishi waliokuwa wakitumia vyeti visivyokuwa vya kwao vilivyoghushiwa walichukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kufutwa kwenye utumishi wa umma na kufikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema Kairuki.
Alisema kwa kuzingatia maelezo ya Magufuli, ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, ilielekeza Necta kufanya uhakiki wa vyeti vya kidato cha nne, sita na vya ualimu.
“Tumefanya hivyo kwa kutambua Necta ndicho chombo cha Serikali kinachosimamia utahini na kutunuku vyeti kwa watahiniwa mbalimbali. Ukaguzi kama huu haujawahi kufanyika nchini,” alisema.
Alitoa mfano wa nchi zilizowahi kufanya ukaguzi kama huo kwamba ni Afrika Kusini, lakini haikuweza kuwafikia watumishi wote kwa wakati mmoja.
Akifafanua kilichogundulika kwenye ukaguzi, alisema kati ya watumishi 400,035 waliokaguliwa, 376,969 wamebainika kuwa vyeti vyao ni halali, ambao ni sawa na asilimia 94.23, wengine 9,932 sawa na asilimia 2.4 wameghushi vyeti.
“Alama za siri pamoja na mhuri uliopo katika vyeti hivyo haufanani na vyeti husika vilivyotolewa na baraza hilo, kundi la tatu ni wenye vyeti vyenye utata ambao ni 1,538, sawa na asilimia 0.3 na vyeti hivyo vinatumiwa na watumishi 3,076. Hii inamaanisha kuwa, cheti kimoja kinatumika na watumishi zaidi ya mmoja na vingine watumishi wawili hadi watatu.
“Ilibainika kuwa, jina la mtumishi mmoja linafanana na lililopo katika kazidata ya Necta. Waliobainika kuwa majina yao yanafanana na yale yaliyoko katika kazidata walihalalishwa na wale ambao hawajafanana tunasema cheti chake kina utata.
“Kundi la mwisho waliowasilisha vyeti pungufu ni 11,596, sawa na 2.8 waliwasilisha vyeti vya kitaaluma. Inatutia shaka kwa sababu haiwezekani ukaenda kupata sifa ya kujiunga na vyuo vya kitaaluma kama haukuwa na cheti cha kidato cha nne na sita, Baraza limewataka waajiri kuwasilisha vyeti hivyo ili wafanye uhakiki,” alisema.
Alisema kughushi cheti ni kosa la jinai na hatua za kisheria zitachukuliwa si walioghushi tu, bali kwa mawakala ambao wanatengeneza na kuuza vyeti, kanuni za kudumu za utumishi wa umma zinasema mwombaji wa ajira serikalini akitoa taarifa za uongo na zikathibitika baada ya kuajiriwa atachukuliwa hatua za kinidhamu na jinai.
MAGUFULI
Baada ya kupokea orodha hiyo, Rais Magufuli ameagiza wafanyakazi 9,932 waliobainika kuwa na vyeti feki wafukuzwe kazi mara moja na wale watakaoendelea kukaa ofisini hadi Mei 15, mwaka huu wapelekwe mahakamani ili wafungwe miaka saba kama inavyosema sheria kwa kosa la kughushi.
Alisema watumishi 1,538 waliobainika kuwa cheti kimoja kinatumiwa na zaidi ya mtu mmoja, nao mishahara yao isitishwe mara moja na wizara husika ikamilishe uhakiki na kujua ni nani mwenye cheti halali.
Kwa upande wa watumishi 11,396 waliowasilisha vyeti vya taaluma peke yake badala ya vile vya kidato cha nne na sita kama ilivyohitajika, ameagiza waendelee kulipwa mishahara wakati uhakiki ukiendelea kujiridhisha kama walifoji vyeti ama walipitia njia za kawaida za astahahada badala ya kwenda chuo kikuu, jambo ambalo si kosa.
“Katika uchambuzi mliofanya wa watumishi wa umma 400,035, watumishi 9,932 wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi na vyeti feki, sasa mimi unataka nifanyaje, watu wamegushi nimsamehe? Haiwezekani, kwa hiyo waziri mkuu upo hapa, na mawaziri mpo hapa, hawa watu 9,932 mshahara wao wa mwezi huu ukatwe na waondoke mara moja kwenye utumishi wa umma kuanzia leo (jana).
“Watakaobaki, kama utaingia mwezi wa tano wapelekwe kwa mujibu wa sheria, wakafungwe hiyo miaka saba, na hizo nafasi 9,932 zitangazwe mara moja watu waombe, hao 9,932 na majina yao muandike yote kwenye magazeti, nataka watu wajifunze wametuibia fedha, hawana qualification (vigezo), lakini wamekuwa kwenye position (nafasi) ambazo hawakustahili kuwa nazo.
“Hawa ni majambazi, majizi kama yalivyo mengine, kwa sababu kwa vyovyote hawawezi waka-perform vizuri, huwezi uka-perform kama huna qualification nzuri, Tanzania hata ukiwa la saba utaajiriwa kulingana na nafasi yako, hata ukiwa form IV (kidato cha nne) utaajiriwa kulingana na position yako, kwani wale makuli kule bandarini wana digrii? Si nguvu tu za bega?
“Ndiyo maana nasema hawa 9,932, watu wa Wizara ya Fedha mko hapa, mkafute majina yao kwenye kompyuta, na orodha ninayo hapa, nitakuwa nikicheki na mimi.
“Watakaojiondoa wenyewe kwa hiyari yao, msiwapeleke mahakamani, wale wanaojifanya wanajua sana itakapofika hadi tarehe 15 Mei, kila Mkuu wa Idara, vyombo vya dola, washikeni pelekeni kwenye vyombo vya sheria wakajibu vyeti vyao walivichongea wapi, hawa watumishi 1,538 sawa na asilimia 0.3 wenye vyeti vya utata, kwa maana kwamba vyeti vyao vinatumiwa na zaidi ya mtu mmoja, wizara ya utumishi mhakikishe ikifika tarehe 15, muwe mmeshajua ni nani mwenye cheti chake, na hao 1,538 mshahara wa mwezi huu wasipewe kwanza hadi atakapopatikana mwenye cheti halali,” alisema.
Pia alisema kati ya hao 1,538 wanaojijua wanatumia vyeti visivyo vyao, wajiondoe mara moja na kwa kufanya hivyo, Serikali itakuwa imetengeneza nafasi za ajira 12,000.
“Kwa hawa watumishi 11,396 waliowasilisha vyeti vya taaluma, muendelee kufanya uchunguzi, kwa sababu mtu anaweza kuwa daktari lakini alianzia medical officer, akaenda ngazi nyingine, alivyomaliza akaenda kuchukua digrii (shahada) ya udaktari, hiyo njia inajulikana, wapo pia walioanzia certificate ya ualimu daraja A, ametoka kule akaenda kuchukua diploma ya ualimu, akatoka akaenda kuchukua digrii.
“Mimi nafahamu chuo kikuu kilikuwa na profesa anafundisha amepitia njia hii, sasa ukimlazimisha profesa awe na cheti cha kidato cha sita utakuwa umekosea sana, kwa sababu alipita katika njia hii na kwa sababu sio kila mmoja lazima afike kidato cha sita, anaweza kupita kwenye mfumo huu ambao unakubalika kiserikali, kwa hiyo hawa muendelee kuwalipa mishahara yao, lakini bado muwachunguze,” alisema Magufuli.
Alisema kutokana na uwapo wa watu wanaoghushi vyeti, ndiyo sababu utendaji wa baadhi ya watu si mzuri.
Alisema baada ya kutangazwa kwa nafasi za watumishi waliobainika kuwa na vyeti feki, ikiongezwa na nafasi 52,456 za ajira kwa mwaka 2017/2018, hali kwa wanaosaka ajira itakuwa nzuri.
“Serikali ya awamu ya tano imejipanga kufanya kazi kwa bidii, hasa kwa Watanzania masikini, taifa hili ni tajiri, tuna kila kitu, tunaweza kufanya kitu chochote, ni bahati mbaya tumekuwa tunakosea na tunapokosea hatuchukui hatua, na haswa sisi wanasiasa kwa kuogopa kupoteza maslahi ya siasa, ni bahati nzuri sasa nchi imeshikwa na mtu ambaye si mwanasiasa.
“Mimi nilivyokuwa chuo nilikuwa nawachukia wanasiasa, wanayoyazungumza hawayatekelezi na ndiyo maana nataka niwaambie, kila mahali kuna matatizo, majina yaliyo hapa leo (jana) ni ushahidi kwamba kulikuwa na matatizo, unapokuwa na wafanyakazi hewa 19,706, unakuwa na watumishi ambao hawana sifa wana vyeti feki 9932, ni shida,” alisema.
Aliongeza kuwa, sakata la vyeti feki lilisubiri hadi Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, aje na hapakuwapo na mawaziri wengine walioona.
“Wao hawakuwaona, hatuko hapa kulaumu waliopita, lakini tuzungumze angalau dhambi walizozifanya ili kusudi tuliopo tujirekebishe.
“Tusipozungumza hatuwezi kujirekebisha tuliopo, tutaendelea na mfumo huo huo, watumishi hewa 19,000 hapakuwa na Waziri wa Utumishi?
“Vyeti hewa hawakuwapo mawaziri? Hawakuwepo makatibu wakuu, hawakuwepo wakurugenzi, si walikuwepo au niseme wapo,” alisema.
Pia alisema hatua anazochukua kwa kusimamisha watumishi hao hazitawafurahisha wengi, lakini wenye sifa watakaopata kazi baada ya nafasi hizo kutangazwa watamuombea.
“Hawa 9,900 leo (jana) wananiombea vibaya kweli, lakini ndiyo wameshaondoka hivyo, lakini watakaoingia kwenye nafasi zao ambao wana sifa wataniombea kweli kweli. Tanzania hatujafikia mahali ambapo mtu ana digrii halafu anakosa kazi,” alisema Magufuli.
Awali, alisema alivyoingia madarakani mishahara kwa watumishi wa umma ilikuwa Sh bilioni 700 kila mwezi.
“Unapozungumzia mishahara ya watumishi maana yake unazungumzia pia fedha zao za posho, likizo, michango yao ya pensheni na kadhalika.
“Tukasema hebu tujaribu kutafuta, kweli hawa watumishi wapo? Tulifanya ukaguzi na kugundua kulikuwa na watumishi hewa, 19,706, kila mwezi walikuwa wanalipwa shilingi bilioni 19.848 kama mishahara ambayo ni shilingi bilioni 238.2 kwa mwaka.
“Baada ya kuwatoa mishahara kwa mwezi imeshuka, na matumizi ndani ya Serikali yameshuka kwa sababu yalikuwa ni matumizi hewa.
“Ukishakuwa na mishahara hewa, wafanyakazi hewa, maana yake unakuwa na matumizi hewa, utakuwa na likizo hewa, kila kitu kinakuwa ni hewa kabisa.
“Baadaye tulijiuliza sana, kama tumekuwa na wafanyakazi hewa 19,000, maana yake hata increment (nyongeza ya mishahara) ilikuwa ni hewa, ukimpandisha mtumishi kwamba amefanya kazi, kumbe tulikuwa tunapandisha hewa.
“Tukaona tuingie kwenye zoezi jingine ambalo ni gumu, na nchi nyingi zimeshindwa kulitekeleza, kwa sababu huwa lina matokeo makubwa, zoezi la kuchambua watu wenye vyeti hewa.
“Unakuta mtu ana nafasi fulani, kumbe cheti siyo chake ni cha mdogo wake, au cha marehemu alikufa yeye anatumia, tunahangaika kutafuta ajira kwa walio na vyeti vilivyokamilika kama wanachuo wa hapa UDOM (Chuo Kikuu cha Dodoma), kumbe serikalini wapo wana vyeti feki, unamaliza hapa kusoma kila unapokwenda kutafuta ajira una cheti chako kina GPA ya 4.1 umepiga misonge (A) pale makarai (C) machache.
“Unavyopeleka cheti pale ofisini kumbe ni darasa la saba, ana cheti hewa, unafikiri atakupa kazi? Atakiangalia hiki cheti, ahaa, kumbe hajui hata kusoma GPA, kwa hiyo vijana wamekuwa wakizunguka kutafuta kazi lakini kazi zimekaliwa na wenye vyeti hewa,” alisema Magufuli.
Alisema kila sekta ina matatizo kwa sababu bandarini nchi ilikuwa ikipoteza mapato mengi, alivyochukua hatua watu wakaanza kulalamika kuwa mizigo imepungua.
“Nikawaambia mizigo acha ipungue hata ikija meli moja lakini ilipe kodi, nimetembelea pale juzi nimekuta kuna meli 30, zimekosa hata sehemu ya kupaki, tumeweka wakandarasi wapanue na kuchimba ile bandari na zaidi ya shilingi bilioni 300 zinatumika.
“Makusanyo yetu kwa mwezi yalikuwa shilingi bilioni 800 hadi 850, wakati mishahara tunalipa shilingi bilioni 700, kwa hiyo inabaki shilingi bilioni 100 kwa ajili ya maendeleo na matumizi mengine, sasa hivi wastani ni Sh trilioni 1.3, lakini bado kuna maeneo mengi tunaibiwa.
“Kampuni za simu zinafanya transaction (yanahamisha) fedha nyingi lakini hela hazingii serikalini, dawa yao tunaitengeneza.
“Nataka tuende mbele, ndiyo maana sasa hivi tunajenga reli ya standard gauge kwa fedha zetu, katika Afrika kama utahesabu nchi tatu au nne, ambazo zitakuwa na reli cross country ya standard gauge, inayotumia umeme (nyingi zinatumia umeme mjini) uitoe reli toka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa spidi ya 160, unaweza kukuta labda ziko nchi mbili tu, lakini tumeamua tuanze, kama Wajerumani walianza wakati wanatutawala, kwanini tusiweze tukiwa huru,” alihoji.
NDALICHAKO
Kwa upande wake, Ndalichako alisema awamu ya pili ya watumishi wa umma wenye vyeti feki, itakabidhiwa wiki ijayo kwa Kairuki, huku akishauri ukaguzi ufanywe pia kwa sekta binafsi kwenye elimu na afya.
Akitoa ufafanuzi wa namna wizara yake kupitia Necta ilivyoshirikiana na Ofisi ya Rais kufanya uhakiki kwa watumishi 400,035 wa Serikali za Mitaa, mashirika na taasisi za umma, alisema awamu inayomaliziwa sasa ni ya watumishi wa Serikali Kuu.
“Awamu ya kwanza ilihusu watumishi wa Serikali za Mitaa, taasisi, mashirika ya umma na wakala wa Serikali na awamu ya tatu inahusu watumishi wa Serikali Kuu, yaani waliopo wizarani na idara zilizo chini yake,” alisema.
Ndalichako alisema katika uhakiki huo, kikosi kazi kilijigawa katika makundi matano ya watu watatu watatu waliokwenda mikoani kufanya kazi za uhakiki.
“Makatibu tawala kote nchini walielekezwa kuleta nakala za watumishi wote kwenye wilaya zao ili kukiwezesha kikosi kazi kifanye kazi katika ofisi za wakuu wa mikoa, ili kupunguza gharama kuliko kila halmashauri ingekuja katika Baraza la Mitihani.
“Wizara, mashirika ya umma na wakala wao waliagizwa kuwakilisha nakala za vyeti za watumishi wao katika ofisi za Baraza la Mitihani.
“Kwa sasa awamu ya kwanza na ya pili imekamilika tayari tumemkabidhi Waziri wa Nchi, Utumishi na Utawala Bora atakukabidhi taarifa ya uhakiki wa watumishi wa Tamisemi, mashirika ya umma, wakala na taasisi za umma, uhakiki wa Serikali uko mbioni.
“Upo umuhimu pia wa kufanya uhakiki katika taarifa za sekta binafsi, hasa katika sekta ya elimu na afya, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazostahili,” alisema Profesa Ndalichako.
Katika hatua nyingine, alisema mwaka 2008 Necta walianza utaratibu wa kutumia picha katika vyeti ili kupunguza tatizo la watu kutumia vyeti vya watu wengine.
“Pia tumeunganisha mfumo wa mafunzo ya kati na juu katika kazidata ya Baraza la Mitihani ili waweze kufuatilia moja kwa moja matokeo yanayotolewa na Baraza la Mitihani.
“Tuliona kuwa baadhi ya waliokuwa wakiomba nafasi ya kujiunga na elimu ya juu walikuwa na nyaraka za kughushi. Tutakuwa tukivibadilisha mara kwa mara ili kuwabaini wanaoghushi vyeti,” alisema Ndalichako.
Alisema pia NECTA imekuwa ikiwataka waajiri wawasilishe vyeti vya watumishi wao waliowaajiri na wale wanaowaajiri ili kuhakiki vyeti vyao kama ni vya kugushi ama la.
“Wapo waajiri ambao wamekuwa wakishirikiana nasi katika kuhakiki na Mheshimiwa Rais katika kipindi cha mwaka 2009 hadi 2015, zaidi vyeti 187,504 vilihakikiwa na kati ya hivyo, 7,281, sawa na asilimia 3.8 vilibainika kuwa ni vya kughushi.
“Pamoja na jitihada za wizara yangu kuwataka waajiri kuwasilisha vyeti kwa ajili ya uhakiki, bado mwitikio haukuwa mkubwa,” alisema.
Alisema waajiri hao badala ya kuwasilisha vyeti kwa ajili ya kuhakiki kwa watumishi waliopo, waliwasilisha vya waajiriwa wapya pekee.
Alisema kwa kushirikiana na Kairuki, walihakikisha uhakiki unafanyika kwa umakini na usiri wa hali ya juu.
Alisema walihakiki vyetu vya kidato cha nne, cha sita na walimu katika ngazi ya cheti na stashahada kwa watumishi wa umma nchini.
“Kwa maneno mengine, hii ngoma bado ni mbichi. Matokeo tunayowasilisha hapa ni ya kidato cha nne, sita na vyeti vya walimu, vya taaluma bado,” alisema.
Alisema uhakiki huo, ulifanywa na kikosi kazi cha watu 15, kati yao 10 walitoka Necta na waliobaki katika Ofisi ya Rais.