Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umetoa mafunzo ya Usalama na
Afya kazini kwa wabunge chini ya Umoja wa Wabunge Vijana Tanzania (TYPF) 100,
ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa Taasisi hiyo kuhakikisha makundi mbali mbali katika
jamii yanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kanuni bora za usalama na afya mahali
pa kazi.
Mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika ukumbi wa OSHA jijini Dodoma
yalifunguliwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, ambaye alimwakilisha Waziri wake, Deogratius
Ndejembi.
Akifungua mafunzo hayo, Naibu Waziri Katambi amesema OSHA inaowajibu mkubwa
wa kulinda nguvukazi ya Taifa hususan vijana ambao ndio wanaunda asilimia kubwa ya
nguvukazi inayotumika katika uzalishaji nchini na duniani kote.
“Kazi kubwa ya serikali kupitia OSHA ni kuwalinda wafanyakazi ili wasipate ajali,
magonjwa au vifo vitokanavyo na kazi kwani kunapokuwa na wagonjwa wengi manake
Serikali inapata mzigo mkubwa wa kuwahudumia na hivyo kuathiri uchumi wa nchi
kutokana na fedha nyingi kutumika kununua madawa na vifaa tiba pamoja na uzalishaji
kushuka kutokana na nguvukazi kupungua na muda wa uzalishaji kupotea kwa kuuguza
wagonjwa,” amesema Naibu Waziri Katambi.
Katambi amewashauri wabunge hao waliopatiwa mafunzo kusaidia kusambaza elimu
juu ya umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usalama na afya nchini ili kuwalinda vijana
na wananchi wote kwa ujumla dhidi ya vihatarishi vya ajali na magonjwa katika shughuli
mbali mbali za uzalishaji.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Vijana Tanzania (TYPF) ambaye pia ni Naibu Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulika Elimu,
Zainab Katimba, amesema lengo la semina hiyo ilikuwa ni kuwajengea uelewa
wabunge vijana katika eneo la usalama na afya mahali pa kazi.
“Kupitia mafunzo haya tumejifunza mengi hususan dhana ya vihatarishi katika maeneo
yetu ya kazi na tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa. Hivyo, tutakuwa katika nafasi nzuri
zaidi kuendelea kuishauri serikali pamoja na kuwashirikisha elimu hii wananchi wetu,”
ameeleza Katimba.
Washiriki wengine wa semina hiyo akiwemo Ng’wasi Kamani, Mbunge wa Vijana Taifa
Pamoja na Venant Daud, Mbunge wa Jimbo la Igalula wameeleza umuhimu wa
mafunzo hayo kwao na wananchi wanaowaongoza.
“Mafunzo haya tuliyoyapata ni muhimu sana kwetu sisi kama wabunge vijana ambao
tunao wajibu wa kusaidia kuwaelimisha vijana wenzetu na wananchi kwa ujumla,”
ameeleza Mbunge Venant Daud.
“Sisi ni wawakilishi wa wananchi wakiwemo wafanyakazi serikalini na sekta binafsi,
usalama wao ni kitu cha msingi sana na hapo ndipo OSHA inapoingia. Kwahiyo yale
tuliyojifunza na yale tunayoyaona OSHA ikiyasimamia ndio yanapelekea kuuona utulivu
uliopo katika shughuli za uzalishaji nchini,” amesema Ng’wasi Kamani.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema mafunzo
hayo ni mwendelezo wa mkakati wa Taasisi ya OSHA kuyafikia makundi mbali mbali
nchini na kuyajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.
Amesisitiza kwamba mafunzo ya usalama na afya ni muhimu kwa wafanyakazi wote
nchini hususan vijana ambao ndio washiriki wakubwa katika shughuli za uzalishaji
ambapo tafiti mbali mbali ukiwemo utafiti uliofanywa na OSHA mwaka 2022 zinaonesha
kwamba vijana ndio wanaoathirika zaidi na ajali na magonjwa mahali pa kazi.