32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

‘OKTOBA 30 MWISHO URASIMISHAJI MAKAZI’

Na BENJAMIN MASESE-MWANZA

SERIKALI imetangaza siku ya mwisho ya mpango wa upimaji na urasimishaji makazi holela jijini Mwanza kuwa ni Oktoba 30, mwaka huu na imewataka wananchi kutambua kwamba, baada ya hapo maeneo yasiyopimwa au kuwa na mchoro wowote yatakuwa sehemu ya ramani maalumu ya mipango miji endelevu.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hosiana Kusiga, alipozungumza na gazeti hili kuhusu ukomo wa mpango huo na hatima ya maeneo yasiyofikiwa au kuwa na migogoro.

Pia alisema, ramani maalumu ya mipango miji endelevu inatarajiwa kutangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ifikapo Novemba, mwaka huu.

“Tumeamua kuweka matangazo kwenye vyombo vya habari ili kuwajulisha wananchi kwamba, mwisho wa upimaji na urasimishaji wa makazi holela ni Oktoba 30, mwaka huu, baada ya hapo, maeneo yote ambayo hayakufikiwa na mpango huo yatamezwa na master plan.

“Ila yapo maeneo ambayo hatukuyafikia kwa sababu ya kubanwa na shughuli hapa ofisini, kitakachofanyika hapo baada ya master plan kutangazwa ni kwamba, kama itaonekana eneo hilo linahitajika, basi Serikali italazimika kuwafidia wananchi ili kupisha mradi husika kujengwa.

“Hivyo hivyo, yale maeneo ambayo yana migogoro iliyotokana na mpango huo, hili la upimaji na urasimishaji makazi, kama suluhisho litapatikana na kuhitajika kupimiwa kama walivyojenga, basi tutafanya hivyo, lakini ikihitajika kutoa fidia ili master plan iendelee, Serikali itawajibika kuingia gharama,” alisema.

Aliwataka wale wasiolipia gharama za kupimiwa na kuandaliwa hati miliki ya makazi yao kujitokeza haraka kabla ya muda kumalizika kwa sababu kuna uwezekano wa kupoteza ardhi wanazomiliki.

Pia aliwatoa hofu wananchi wasiofikiwa katika maeneo yao na kusema watakaa na Serikali ili kufikia mwafaka kama yatahitajika kujengwa kama ramani ya mipango miji endelevu itakavyoonyesha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles