ACCRA, Ghana
VIONGOZI wa mataifa mbalimbali na Jumuiya za Kimataifa wameomboleza kifo cha Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa,(UN) na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Kofi Annan aliyefariki dunia juzi akiwa na umri wa miaka 80.
Miongoni mwa viongozi waliotuma salamu za rambirambi kwa familia na viongozi wa nchi hii, ni Katibu Mkuu wa sasa wa UN, Antonio Guterres, Rais wa Urusi, Vladimir Putin na Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, ambao walimuelezea Annan kama alikuwa kiongozi wa kuigwa na aliyesimamia vema dunia.
Annan, raia Ghana, aliitumikia UN kuanzia mwaka 1997 hadi 2006 na ndiye mwafirika wa kwanza kushika wadhifa huo katika taasisi hiyo kubwa duniani.
Baada ya kipindi hicho hadi anafariki dunia ndiye aliyekuwa msuluhishi katika mgogoro wa Syria akiongoza jitihada za kumaliza mfarakano uliopo nchini humo.
Mwanadipolomasia huyo alifariki dunia juzi katika hospitali mjini Bern, Uswisi baada ya kuishi nchini humo kwa miaka saba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na taasisi yake, kiongozi huyo alifariki dunia Jumamosi baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Putin alisema kumbukumbu ya Annan itaendelea kudumu mioyoni mwa wananchi wake.
Kwa upande wake Obama, ambaye pia ni mwafrika wa kwanza kuingia Ikulu ya Marekani, alisema baada ya kuvuka vikwazo vyote Annan hakuacha kusimamia jukumu la kuhamasisha kuwapo dunia yenye amani.