HERIETH FAUSTINE NA MAULI MUYENJWA, DAR ES SALAAM.
VILIO vilitawala jana wakati zaidi ya nyumba 400 za wakazi wa Mtaa wa Mloganzila, Kibamba katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, zilipokuwa zikibomolewa.
Ubomoaji huo ulianza saa 4:00 asubuhi baada ya mmiliki wa eneo hilo la ekari 33, Henry Kashangaki kushinda kesi dhidi ya watu 11 wanaodaiwa kuvamia eneo hilo na kuwauzia wananchi wengine ambao walijenga nyumba bila kufahamu undani wa eneo hilo.
MTANZANIA lilishuhudia ubomoaji huo ukiendelea huku baadhi ya wananchi wakianguka na kuzimia ovyo na wengine wakihamisha vitu mbalimbali vya ndani.
Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti baadhi ya waaathirika wa ubomoaji huo, walisema taarifa za kutakiwa kuondoka katika eneo hilo kabla ya kuvunjiwa nyumba zao, walizipata Aprili 30 mwaka huu na hawakupewa muda wa kutosha kuondoa mali zao.
Mkazi mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alilalamikia kuwa hawakutendewa haki kwa vile haikuwa rahisi kwa muda huo mfupi wa siku moja kuweza kuokoa mali zao.
“Sina la kufanya… watoto sijui nawapeleka wapi na nitapata vipi hela za kujenga nyumba kama hii.
“Hata kama kweli eneo ni la kwake siyo busara kutuvunjia hivi wakati wanajua hata sisi ni binadamu,” alisema mwananchi huyo.
Alisema hata mwenendo wa kesi hiyo ulitekwa na kuendeshwa na upande mmoja na mmliki huyo.
Mwananchi huyo alidai mmiliki huyo alitumia nguvu zake za fedha kuwanyima haki wakazi hao kwa sababu hawajawahi kuitwa kwenye kesi husika.
Mkazi mwingine aliyefahamika kama Mama Rahma, alisema diwani wa kata hiyo aliwaombea kwa mmiliki huyo awape siku tatu waweze kuondoa vitu katika nyumba zao lakini aliwakatalia na akawataka wahame baada ya kutolewa agizo hilo.
“Hali hii imenikuta wakati nikiwa peke yangu, mume wangu yuko Tanga kwenye msiba wa babu yake na tukio hili la leo (jana) limetokea baada ya kupita gari ya matangazo Jumamosi na kututaka tuhame katika maeneo haya.
“Hapa sijui nafanyaje kwa sababu sina fedha za kuhifadhi vyombo vyangu na watoto…nimechanganyikiwa,”alisema Mama Rahma.
Alisema wakati wananunua kiwanja hicho waliambiwa kuwa maeneo hayo ni halali.
Mama Rahma alisema wakati kesi hiyo ikiendelea wakazi wengi hawakujua mwenendo wake na hata uamuzi wa kubomolewa nyumba zao hawakuujua.
“Mjumbe wa eneo hili tunayemfahamu kwa jina moja la Mama Maimuna tulipomtafuta kujua hatima yetu alisema hana cha kutusaidia akidai hata yeye ni mwathirika wa hatua hiyo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlonganzila Kata ya Kiluvya, Emmanueli Yohana alisema shauri la kubomolewa kwa nyumba hizo lilitolewa na Baraza la Ardhi la Wilaya ya Kinondoni ingawa yeye hakuonyeshwa nyaraka za shauri hilo la kuwataka kuondoka katika eneo hilo.
Hata hivyo, alisema viongozi waliopita walipewa notisi lakini hakujua ni kwa nini taarifa hazikufika kwa wananchi.
Diwani wa Kata ya Kwembe, Dweza Kolimba (Chadema) alisema taarifa ya notisi za kuondoka maeneo hayo zilikuwa hazijulikani kwa wakazi wa eneo hilo akiwamo yeye.
Alisema alishitushwa na tangazo la Jumamosi ndipo alipoanza kulifuatilia.
“Ofisi ya Kata ya Kwembe haikupewa samasi yoyote ya kuitwa katika kesi hiyo wala notisi ya kuwaarifu wananchi ili waondoke maeneo hayo.
“Kwa kweli kesi hiyo ilisikilizwa upande mmoja.
“Baada ya kupata taarifa za kuhama siku ya Jumamosi tulianza kufuatilia katika Kituo cha Polisi cha Mbezi.
“Tunashukuru walitupa ushirikiano na kutueleza kuwa ni kweli kuna taarifa hizo na hata baada ya kuwasiliana na Mkuu wa Wilaya alisema suala hilo limeshaamuriwa na mahakama labda wananchi hao wazungumze na mwenye eneo (Kashangaki)… lakini hata yeye aligoma kuongeza muda,”alisema Kolimba.
Mabomu yaridima
Awali, wakati ubomoaji huo ukiendelea, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya baadhi ya wananchi waliokuwa wakifanya fujo kuzuia ubomoaji wa nyumba zao.
MTANZANIA ilishuhudia wananchi watatu wakiwa wamezimia na kupakiwa katika gari la polisi kupelekwa hospitalini baada ya nyumba zao kubomolewa huku wengine wakilia kwa uchungu.
Baadhi ya wakazi waliokuwapo karibu na nyumba zao walipewa muda wa kuokoa mali zao yakiwamo mabati, madirisha na vifaa vya ndani lakini kwa wale ambao walikuwa mbali hawakufanikiwa kufanya hivyo.
Wakati gazeti linaondoka katika eneo hilo saa 11.00 jioni, nyumba zaidi ya 80 zilikuwa zimekwisha kubomolewa.