Na ELIZABETH HOMBO-MWANZA
ALIYEKUWA Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amejiunga rasmi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku akiwataka Watanzania kutambua wakati wa mabadiliko ni sasa.
Nyalandu ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), alikabidhiwa kadi ya chama hicho jana jijini Mwanza na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Akizungumza na maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Mhandu, Godfrey Misana (Chadema), Nyalandu alisema aliisubiri kwa hamu siku ya kujiunga na chama hicho.
Nyalandu ambaye alijivua uanachama wa CCM Oktoba 30, mwaka huu, alisema amejawa na utayari na heshima kujiunga na chama hicho na kwamba saa ya mabadiliko ni sasa.
“Nasimama mbele yenu na mbele ya Watanzania wote nikiwa nimeisubiri kwa shauku kubwa siku hii ya leo ili nipate fursa ya kujiunga na harakati za kupigania mageuzi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi hapa nchini.
“Kwa kujiunga rasmi Chadema. Asanteni sana kwa upendo wenu na mapokezi makubwa. Nilijiondoa CCM Oktoba 30 mwaka huu na kujiuzulu nafasi yangu ya ubunge wa Singida Kaskazini kwa tiketi ya CCM, ikiwa ni pamoja na kujivua nafasi zote za uongozi ndani ya CCM, ikiwepo ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kwa kuwa katika miaka miwili ya uongozi wa awamu ya tano.
“Nimeamini na kujiridhisha kuwa CCM imepoteza mwelekeo, na kwamba niliporejea “ahadi za mwanachama wa CCM”, nikakumbushwa maneno haya: Nitasema kweli daima na uongo kwangu ni mwiko. Katika majira na nyakati tunazozipitia kama Taifa.
“Na mimi naogopa kusema uongo. Mabadiliko ya kisiasa ni lazima nchini Tanzania na wakati ni huu. Wakati wa kuondoka CCM, nililijulisha Taifa azma yangu ya kutaka kujiunga na Chadema, endapo wanaChadema wataona vema, kuniruhusu niingie malangoni mwenu. Niwe mmoja wenu, tushikamane pamoja.
“Wakati naondoka CCM, nililijulisha Taifa kuwa, daima nitakuwa mwaminifu kwa nchi yangu Tanzania na kwamba naungana na upinzani kupigania haki kwa kuwa imeandikwa haki huinua taifa, na kwa pamoja tutaitafuta na kuilinda tunu hii muhimu kwa taifa letu,” alisema Nyalandu.
Mwanasiasa huyo ambaye alipata kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema wakati anaondoka CCM, alijulisha Taifa kuwa anaamini kwamba Tanzania inahitaji Katiba mpya.
“Naomba kulikumbusha Taifa kuwa katika umoja wetu, tutaishinda hofu, tutaushinda utengano na tutaimarisha demokrasia ya kweli hapa nchini Tanzania.
“Na sasa saa imefika na saa hiyo ndio sasa, Watanzania tusinung’unike tena, tusiwe na simanzi tena, na tusihuzunike tena, kwa kuwa Mungu ameruhusu miongoni mwetu, na kwa wote mnaoyasikia maneno haya, kuamsha mashujaa watakaosimama na kuitetea haki Tanzania.
“Hakika, saa imefika ambapo, yeyote ajionaye mnyonge na dhaifu miongoni mwetu na asimame, akiri akisema mimi ni shujaa, kwa kuwa saa ya mabadiliko inakuja.
“Naam, saa imefika kwa mtu yeyote miongoni mwetu aliye maskini na akiri, mimi ni tajiri, kwa kuwa ndani yetu na katika ukiri wetu, tumepewa utayari wa kuiambia Tanzania, Mungu wako anamiliki,” alisema Nyalandu
Waziri huyo wa zamani ya Maliasili na Utalii, alisema kuwa sasa anaamini Mungu ameruhusu sasa kujiunga na Chadema sambamba na kusimama kwa chama hicho pamoja na vyama vingine vya upinzania.
“Kama chama cha Watanzania wote, bila kujali dini zao, bila kujali makabila yao na bila kujali mapokeo ya itikadi zao za kisiasa, ili kuleta mabadiliko mapya ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa.
“Kwa kuwa imeandikwa katika vitabu zamani, ni “mizuri kama nini, miguu yao waletayo habari njema.” Kwa Mwanza na Tanzania, na kwa wote waliosimama katika mkutano huu mkubwa, tunawatangazia uhuru kwa wale wasiojisikia huru kuongea, tumekuja kuwatangazia wote walio wapole wa kunena, wasije kunyamaza tena, kwa kuwa sote tunaungana kukiri kwa mara nyingine tena, Tanzania bila CCM, inawezekana!
“Nimekuja mbele yenu, nisimame miongoni mwenu nikiwa nimeachana na masilahi na heshima yangu ya kuwa mbunge, niungane nanyi katika harakati za kuleta mabadiliko mapya,” alisema Nyalandu huku akishangiliwa na mamia ya wananchi katika mkutano huo.
MGOMBEA ANADIWA AKIWA MAHABUSU
Mgombea huyo wa udiwani wa Kata ya Mhandu, Gerald Misana yupo gerezani tangu Jumanne iliyopita kwa kile kilichodaiwa kuwa alimjeruhi meneja kampeni wa CCM.
Kutokana na hilo, mbali ya Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho kumnadi mgombea huyo, mke wake Rose Misana pia alipanda jukwaani kumnadi mume wake achaguliwe.
“Leo ni siku ya tano sijamwona mume wangu, naomba mpeni kura za ndiyo, pia ninawaomba waliomkamata mume wangu wamwachie,” alisema Rose.
Katika hatua nyingine wakati Mbowe alipanda jukwaani mvua ilianza kunyesha kwa dakika 30 lakini aliendelea kumnadi mgombea huyo.
Baada ya dakika 30 Mbowe alishuka jukwaani na kuanza kuondoka na msafara wake ambapo umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo walimsindikiza na baadaye Jeshi la Polisi kupiga mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi hao.
MNYIKA NA MABOMU
Taarifa kutoka mkoani Songwe, zilisema kuwa msafara wa Naibu Katibu Mkuu Chadema (Bara), John Mnyika, uliokuwa unatoka eneo la mkutano katika Kata ya Ndalambo, wilayani ya Momba umezuiwa na polisi na ghafla wakaanza kupiga mabomu ya machozi.
Baada ya kuanza kupigwa kwa mabomu hayo watu wanaodaiwa kuwa ni polisi walivamia gari ya Mnyika na kumchomoa dereva wake.
Pamoja na hali hiyo dereva huyo alifanikiwa kuwakimbia watu hao na kukimbia kusikojulikana, huku viongozi wa Chadema Kanda ya Nyasa wakiendelea kumtafuta hadi kufikia jana jioni.