*Yakabidhi madawati 200, viti na meza vyenye thamani ya milioni 25
Na Gustafu Haule, Mtanzania Digital
WANAFUNZI 600 wa shule nne za msingi zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani wameondokana na adha ya kukaa chini baada ya Benki ya NMB kutoa msaada wa madawati 200, viti 16 na meza nane yenye thamani ya Sh milioni 25.
Shule zilizonufaika na msaada huo ni Kambarage, Lumumba, Kongowe na Bungo ambapo kila moja imepata madawati 50 huku katika shule ya msingi Viziwaziwa ikipata viti 16 na meza nane kwa ajili kuboresha ofisi ya walimu.
NMB imekabidhi msaada huo Oktoba 10, katika hafla iliyofanyika katika shule ya msingi Kambarage huku ikishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Dismas Prosper, amesema NMB imeweka utaratibu wa kila mwaka kusaidia jamii.
Prosper amesema kila mwaka NMB imekuwa ikitenga asilimia 1 ya faida yake na kurudisha katika jamii kwa kusaidia katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya na mpango huo ni endelevu nchini nzima.
Amesema wameweka utaratibu huo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi zaSerikali katika kusimamia sekta ya elimu nchini hasa katika shule za mijini na vijijini ili kuona wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri.
“NMB imeweka utaratibu wake maalum wa kuhakikisha kila mwaka inatenga asilimia 1 ya faida yake na kurudisha kwa jamii katika kusaidia sekta ya elimu na afya,lakini leo tupo hapa kwa ajili kukabidhi madawati 200, viti 16 na meza 8 kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa Shule nne na walimu wa lhule ya Viziwaziwa,” amesema Prosper.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John, ameishukuru NMB kwa kutoa msaada huo kwani umesaidia kuokoa wanafunzi wengi ambao walikuwa wakipata shida katika masomo yao.
John ,amesema walichokifanya NMB ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na benki hiyo ili kuhakikisha wanatatua kwa pamoja changamoto za elimu zilizopo katika Shule mbalimbali.
Naye Afisa Elimu ya Awali na Msingi kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha, Berdina Kahabuka, amesema msaada huo umesaidia kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji ambapo ameomba benki hiyo kuendelea kusaidia na Shule zingine zilizopo katika Halmashauri hiyo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kambarage, Happiness Msaki, amesema msaada wa madawati hayo umepunguza adha ya wanafunzi wake kukaa chini kwani awali kulikuwa na upungufu wa madawati 113 hali ambayo ilikuwa ikisababisha utoro na wengine kushindwa kufuatilia vizuri masomo yao.
Ameongeza kuwa shule yake inajumla ya wanafunzi 878 na kwa wastani darasa moja linachukua wanafunzi 150 ambapo wengi wao walikuwa wanakaa chini lakini baada ya NMB kutoa madawati hayo kwasasa wanaupungufu wa madawati 50.