Na WALTER MGULUCHUMA- KATAVI
BENKI ya NMB imetoa msaada wa mabati  300 yenye thamani za Sh 8,000,000 kwa ajili ya Shule ya Msingi Kilida, iliyoko Halmashauri ya Mpimbwe, Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi, ambayo majengo yake yaliezuliwa na mvua mapema mwaka huu.
Mbali ya msaada huo, pia wametoa kompyuta 7 kwa ajili ya shule tatu za sekondari zilizopo kwenye halmashauri hiyo.
Msaada huo ulikabidhiwa jana kwa   Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu Raphael Muhuga na Meneja Mahusiano Biashara ya Serikali wa NMB wa Kanda za Nyanda za Juu, Focus Lubende.
Focus alisema uongozi wa Mkoa wa Katavi ulitambua benki hiyo iko karibu na wananchi na hivyo kuwa ni sehemu ya kwanza ya kukimbilia ili kutatua changamoto ya majanga ya mvua yalioleta madhara makubwa wilayani Mlele.
Alisema vifaa hivyo walivyovikabidhi ni sehemu ya ushiriki wao katika maendeleo ya jamii na wao kama benki inayoongoza Tanzania kwa kuwa na matawi mengi wanahakikisha jamii inayowazunguka inafaidika kutokana na faida wanayoipata.
Wanafahamu kuwa Shule ya Msingi Kilida ilipata janga la kuezuliwa paa  na majengo ya madarasa, hivyo kufanya mazingira ya wanafunzi kuwa magumu.
Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kasanda, alisema msaada huo utasaidia kurekebisha majengo ya madarasa yaliyoezuliwa na mvua kali iliyonyesha Machi mwaka huu na kusababisha vifo vya watu sita na miundo mbinu mbalimbali kuharibika.
Naye Muhuga aliiomba ifungue matawi mengine kwenye wilaya hiyo.
Aliyataja maeneo ambayo yana watu wengi na mzunguko wa fedha kuwa ni Majimoto na Usevya, katika Wilaya ya Mlele na Kasekese wilayani Tanganyika.