25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yatenga Sh bilioni 2 kuendeleza sekta ya elimu, afya

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Benki ya NMB  imetenga zaidi ya Sh bilioni 2 kwa mwaka huu wa fedha  kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu na afya nchini, ikiwa ni utekelezaji wa sera ya kurejesha sehemu ya faida kwa jamii.

Kiwango hicho ambacho ni ongezeko mara dufu ya bajeti ya mwaka wa fedha ulioisha unadhihirisha dhamira ya NMB ambayo ndiyo benki yenye matawi mengi zaidi na huduma bora za kibenki nchini wa kufanya uwekezaji endelevu na wenye tija katika maendeleo ya sekta hizo muhimu.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Manyamanyama ya wilayani Bunda mkoani Mara, wakipiga makofi baada ya kupokea bati 400 zenye thamani ya Shilingi milioni 13.5  kutoka NMB kwa ajili ya shule hiyo na Shule ya Sekondari Nyamang’uta.

Katika jitihada hizo, benki hiyo juzi imetoa msaada wa vifaa vya ujenzi na madawati vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 72.5 kwa shule za umma na vituo vya afya katika wilaya za Bunda mkoa wa Mara, Kaliua mkoani Tabora na Kinondoni mkoani Dar es Salaam. 

Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea misaada yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 50 kwa shule za msingi na vituo vya huduma ya afya wilayani Kinondoni, mkuu wa wilaya hiyo, Godwin Gondwe alisema uwekezaji unaofanywa na NMB katika sekta za elimu na afya una tija kwa jamii kwa sababu unasaidia Taifa.kuoambana na maadui ujinga na maradhi.

“Inachofanya NMB kupitia Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ni zaidi ya uwekezaji kwa Taifa na watu wake. Kupitia programu hii, Taifa linakuwa na kizazi chenye afya bora, wasomi bora, viongozi, wafanyakazi na wafanyabiashara bora,” alisema Gondwe wakati wa hafla iliyofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mikumi, Magomeni.

Awali akikabidhi misaada hiyo iliyotolewa kwa Hospitali ya Mwananyamala, Kituo cha Afya Bunju, shule mbili za msingi na nne za Sekondari wilayani Kinondoni, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard alisema misaada iliyotolewa ni utekelezaji wa sera ya kurejesha kwa jamii asilimia 1 ya faida ya benki kila mwaka.

Wakati Hospitali ya Mwananyamala na Kituo cha Afya Bunju vikikabidhiwa misaada ya vitanda vyenye thamani ya Sh milioni 14,  shule za Msingi Mikumi na Wazo Hill ya Wazo zilipokea misaada ya mabati 50 na madawati 100, wakati shule za sekondari Kigogo, Mzimuni, Boko Mtambani na Kiseuke  zimepewa jumla ya viti 250 na meza 250, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 36.6. 

Kwa upande wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Meneja wa NMB kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus alikabidhi misaada ya mabati 400 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 13.5 kwa shule za sekondari za Manyamanya na Nyanaguta ambapo kila shule imepokea mabati 200.

Akipokea misaada hiyo wakati wa hafla iliyofanyika shule ya sekondari Manyamanyama juzi, mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari aliishukuru NMB kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akiwasihi wazazi na walezi wilayani humo kujitolea kwa hali na mali kuunga mkono juhudi hizo kwa kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule za maeneo yao.

“Sitakuwa na urafiki na wazazi, walezi na viongozi wa vijiji na kata ambazo shule zake hazina vyumba vya kutosha vya madarasa, matundu ya vyoo, maabara na mabweni kwa ajili ya watoto wetu. Kila mmoja katika eneo lake aonyeshe juhudi na serikali pamoja na wadau wengine wakiwemo NMB wataunga mkono,” alisema Nassari 
Kwa wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, NMB imetoa msaada wa mabati 90 zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 9 kwa shule za msingi Ilege na Mkiligi.

Misaada hiyo ilikabidhiwa na meneja wa NMB kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus kwa Mkuu wa Wikaya ya Kaliua, Chacha Matiko aliyeishukuru benki hiyo kwa  kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu katika shule za umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles