Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
HAKUNA mtu asiyependa kitu kizuri, sema tu wakati mwingine tunashindwa kuvipata vile tunavyovipenda kwa sababu ya uoga au kutokuwa na vipato sahihi.
Vivyo hivyo hata kwenye ujenzi wa nyumba, kila mtu anatamani angekuwa na nyumba nzuri lakini wakati mwingine kwa sababu ya uoga.
Nasema hivyo kwa sababu wakati mwingine tunajenga nyumba kwa kutumia mafundi wasioeleweka kwa sababu tu ya kutokuwa na taarifa sahihi.
Lakini ukweli ni kwamba unapotumia njia sahihi kujenga nyumba yako hupunguza gharama kuliko wengi wanavyodhani au kuogopa.
Katika ujenzi kamwe usiogope kufuata njia bora ili uweze kupata nyumba nzuri na ya kisasa kwa sababu ‘cheap is expensive’.
Kama wewe ni mfuatiliaji wa makala hizi utagundua kwamba nimekuwa nikisisitiza kufuata njia sahihi unapoanza ujenzi ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa na mafundi sahihi.
Sasa leo tutaangalia njia muhimu unazotakiwa kuzifuata unapojenga nyumba yako.
Njia hizi zitakusaidia uweze kujenga nyumba bora na ya kisasa.
Jambo la kuzingatia usiogope kuanza mapema kwa hofu la hasa! Anza na kila senti ina maana kubwa katika ujenzi na unapoanza mapema ndipo unapomaliza mapema pia.
Kwa bahati mbaya zaidi hilo halifanyiki kama hujafanya maandalizi ya mapema.
Maandalizi ya ujenzi huanzia nyumbani wewe na familia yako, unapanga unatamani nyumba yako iwaje baada ya hapo peleka mawazo yako kwa mbunifu wa majengo ambaye atakushauri kitalaamu.
Kila mtaalamu au mbunifu( deseiner) na mhandisi anafanya kazi yake kwa njia tofauti, lakini wewe kama mwenye mradi wa ujenzi unatakiwa kufuata njia zilezile ili kupata nyumba bora ya kisasa.
Zifuatazo ni njia sita zitakazokusaidia ku-plan au kufanikisha nyumba ya kisasa na ni muhimu kwa mradi wowote ule.
1. CHAGUA MTAALAMU
Ili kupata ramani bora na kazi inayoelezea kila kitu kuhusu nyumba yako au jengo lako ni lazima ukutane na wataalamu wa ujenzi ‘architects’ au wabunifu majengo, wabunifu wa ndani (interior designer) au wote.
Kila kampuni inafanya kazi yake kwa njia tofauti na leseni zao zinatofautiana.
Wabunifu wengi wa majengo wanafanya kazi katika mradi ambao unahusisha kazi kubwa ya ubunifu pia wanatoa msaada wa uchaguzi wa ‘material’ na vifaa vya ujenzi wa ujumla.
Ushauri unaotolewa na watalaamu hawa haulingani hata kidogo na mafundi wale tuliowazoea mitaani.
Watalaamu hawa wana ujuzi ambao utakusaidia pia kupunguza gharama nyingi ambazo zinasababishwa na mafundi wa mtaani wasio na viwango.
Mbunifu wa majengo anaweza kufanya kazi kwa upana au kufanya kazi ya kubuni jengo peke yake kwa maana ya ‘floor’ na kuta na kuacha kazi ya umeme, bafu na jiko kwa ajili ya mbunifu mwingine.
Kama nilivyosema mwanzo kwamba kuchagua staili ya jengo kunaanza na vikao, yaani kukutana na mbunifu wa majengo.
Ili uweze kupata kazi nzuri jaribu kukutana na wabunifu wawili au watatu na wapime yupi bora zaidi.
Vikao hivi vinaweza kuchukua wiki kadhaa. Inategemea kampuni ngapi ambazo umewasiliana nazo au umezifanyia usaili.
Hii ni nafasi ya kufahamu huduma ambayo kila kampuni inatoa kuhakikisha zinaendana na matarajio yako.
2. ANZA KUTENGENEZA RAMANI
Baada ya kuchagua kampuni ya kukubunia ujenzi wa jengo lako au mradi wako sasa ni muda wa kuanza kutengeneza ramani yako.
Mara nyingi kuna njia mbili au tatu ambazo ni nzuri ili kufikia malengo ya dizaini yako uliyoichagua.
Ubunifu mara nyingi unakuwa ni mwendelezo na mara nyingi huusisha michoro lafu kama msingi, kuta na mwonekano wa nje wa nyumba.
Inachukua muda kwa kazi ya kitalaamu kudizaini vitu kama hivyo na mara nyingi kwa wiki mbili au zaidi inategemea na aina ya jengo au mradi kwa mwenye mradi kufanya uamuzi.
Kama mradi ni mkubwa au mmiliki wa mradi anataka kufanya mabadiliko hilo linaweza kuchukua tena muda mrefu zaidi.
3. WAHOJI WABUNIFU MAJENGO
Hili nalo lipo kwenye hatua za kutekeleza mradi wako, pale unapochagua dizaini ya mwisho.
Kama kitu hujakielewa au unaona hakijakaa sawasawa mfahamishe mbunifu wako muulize na hakikisha unapata majibu yanayojitosheleza.
Katika hatua hii ya ramani kama kuna kitu hujakipenda pia ni wakati wa kuzungumza na kuangalia uwezekano wa kukiweka sawasawa
Mara nyingi kuna ‘idea’ muhimu za jinsi jengo litakavyoonekana kutoka nje, kuta na hata msingi na aina ya ‘material’ utakayotumia.
Katika hatua hii kuna uwezekano wa kutoa makadirio ya awali ya gharama ya ujenzi.
Wahandisi au wabunifu majengo wanaweza kuuliza kuhusu makisio ya gharama za ujenzi wakati wa mazungumzo ya ku-panga.
Inaweza kuchukua wiki tatu au kadhaa kufanya makadirio ya ujenzi.
Na inaweza kuchukua hata mwezi kwa mwenye jengo kupata makadirio ya gharama za ujenzi.
Baada ya hatua hiyo unaweza kutembelea eneo la ujenzi kwa ajili ya kufanya utafiti wa ziada kabla ya kufanya uamuzi wa mhandisi wa kumchukua.
Angalizo wewe kama mwenye mradi wa ujenzi unatakiwa kufuata njia zilezile ili kupata nyumba bora ya kisasa.
4. NENDA KUFANYA MANUNUZI WAKATI WENGINE WANAENDELEA NA SHUGHULI YA UHANDISI
Upende, usipende kufanya manunuzi hii ni hatua ambayo wewe kama mwenye mradi utatakiwa kuhusika ili uweze kuchagua kile ambacho unakipenda lakini pia kwa msaada wa ushauri wa mtaalamu wako.
Hii itategemea na jinsi mhandisi au mbunifu wako wa jengo atakavyokusaidia juu ya uchaguzi wa ‘material’.
Hata kwa wale wanaopenda kufanya manunuzi wenyewe wanaweza kuelemewa na hasa vile vitu vya kitalaamu vinavyohitajika.
Ndio maana katika ujenzi wa kisasa inashauriwa kushirikisha wataalamu katika kila hatua.
Kamwe hutakiwi kupuuzia idadi ya vitu zinavyohitajika kuchaguliwa iwe kutoka kwenye madirisha hadi kwenye vifaa vya umeme kama taa.
Hakikisha kile ulichoshauriwa na mtaalamu wako au kile mlichoshauriana na kukubaliana kinakwenda sawasawa na si kujianzia tu.
Kumbuka mtaalamu hafanyi kila bila sababu, kila anachoshauri kinakuwa na mantiki.
Ili kuweza kumudu gharama za ujenzi wa jengo lako ni vizuri kuchagua kila kitu hadi cha mwisho, wakati ubunifu ukiwa unafanyika na vilevile ujenzi ukiwa unaelekea kuanza.
Hii pia itamsaidia mhandisi wako kukuambia gharama kwa kila kitu ulichokipenda na ulichokichagua kwa wakati muafaka kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo lako.
Jipe ruhusa ya mwezi mmoja au miwili kuchagua kila kitu, kamwe usiharakishe fanya utafiti wa kutosha na jiridhishe wakati unafanya manunuzi mfano ya tiles au mbao ngumu kwa ajili ya sakafu.
Kumbuka hapo bado haujaanza ujenzi na ni wakati huo mhandisi wako naye atakuwa anahitimisha michoro ya ujenzi ya jinsi jengo lako litakavyojengwa.
5. JIPE RUHUSA
Inategemea na eneo la mradi wako lilipo, kibali chako au ruhusa yako inaweza kuchukua siku, mwezi au miaka. Lazima uwe na ‘idea’ ya jinsi ya kukamilisha ruhusa yako.
Hii itakusaidia kujua lini utakamilisha au kuanza mradi wako.
ANZA MIPANGO
Ramani ikikamilika na kukabidhiwa kwa ajili ya ruhusa ya uchaguzi wa ‘material’ mhandisi wako atakuwa na uwezo wa kumaliza kukuandikia gharama pamoja na mkataba kwa ajili ya ujenzi.
Katika hatua hii iwapo material zilizochaguliwa zimezidi uwezo wa bajeti yako inavyoruhusu, ipo nafasi ya kubadili mwelekeo wa kazi au ‘material’ ili kupunguza gharama.
Pia katika hatua hii wakati mkataba unasainiwa, mhandisi wako atakuwa ameanisha vitu zinavyohitajika haraka na vile vya baadae.
Kutokana na hali ya kipato kwa wengi, wahandisi wengi pia wanauwezo wa kushauri kipi kianze kununuliwa kipi kisubiri baadae.
Kwa maana hiyo wana nafasi ya kushauri ujenzi kufanyika hatua kwa hatua.
Hadi hapo tumefika mwisho wa njia sita za kufuata unapozingatia ujenzi wa nyumba bora na ya kisasa.
Tukutane wiki ijayo, kwa maoni au ushauri tuandikie kupitia barua pepe; [email protected]Â