MAPEMA wiki hii Kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliwaongoza wabunge wa upinzani na wafuasi wake kuitosa kampuni inayoongoza nchini Kenya ya mawasiliano, Safaricom na kuhamia ile inayoifuatia kwa ukubwa Airtel.
Uamuzi huo wa National Super Alliance (NASA) ni mwanzo wa mkakati wa ususiaji wa kiuchumi dhidi ya bidhaa au huduma zinazotolewa na kampuni, ambazo muungano huo wa upinzani unaamini zina ushirika na Chama cha Jubilee.
NASA inadai kampuni hizo zinasaidia kuendeleza udikteta wa chama cha Jubilee na kubomoa demokrasia na matakwa ya Wakenya.
Tayari mamia ya wafuasi wake walikuwa wameshaitosa Safaricom wakati mkakati huo ulipotangazwa rasmi Ijumaa iliyopita.
Chama cha mawakala wa Safaricom na wachambuzi wa uchumi nchini humo wameonya hatari ya mpango huo kwa taifa, ambao umezilenga pia Brookside Dairy na Bidco.
Kinara mwenzake wa NASA Musalia Mudavadi, ambaye alihutubia wanahabari siku hiyo alisema ususiaji huo wa kiuchumi utatoa funzo kwa kampeni zilizobadili matakwa ya watu wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 8.
Wakati Safaricom ikimilikiwa na Wakenya hususani vigogo wenye ufuasi wa Jubilee, Airtel inamilikiwa na wageni, kitu ambacho chama cha mawakala wa kampuni hiyo kimeuita uamuzi huo kuisusia usio wa kizalendo na wa kibaguzi.
Aidha wakati kampuni ya bidhaa za maziwa Brookside ikimilikiwa na familia ya Rais Uhuru Kenyatta, Bidco inamilikiwa na wafanyabiashara wa Kiasia ikizalisha mlolongo wa bidhaa kuanzia za kula, matumizi ya majumbani hadi wanyama.
Viongozi wa NASA wamesema wazi majina zaidi ya kampuni zaidi yatatolewa kama sehemu za kutaka kuishinikiza Serikali ya Jubilee irejee katika misingi ya kidemokrasia, ikiwamo kurudia uchaguzi mkuu ndani ya siku 90.
Tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, ambao Raila alishindwa na Rais Uhuru Kenyatta na ule wa Agosti 8, kiongozi huyo wa upinzani amekuwa akiituhumu Safaricom kusaidia kuchakachua matokeo ya chaguzi za urais kwa ajili ya Jubilee.
Uchaguzi wa Agosti 8 ulibatilishwa na Mahakama ya Juu baada ya IEBC kupatikana na hatia ya kukiuka sheria katika maandalizi na urushaji wa matokeo.
Safaricom, imejitokeza na kukanusha madai hayo huku ikisema kuwa ilitekeleza kwa uadilifu mkataba iliopewa wa kurusha matokeo kupitia mtandao wao.
Mawakala wa Safaricom wameingiwa wasiwasi na hatua hiyo ya upinzani wakisema maisha ya Wakenya milioni moja yataathirika kwa hatua hiyo ya kususa bidhaa zao ikiwamo huduma za M-PESA.
Lakini Mudavad amepuuza wasiwasi huo akisema uchumi wa taifa utabakia pale pale kitakachohama ni uchumi kutoka kampuni moja kwenda nyingine pamoja na ajira kutoka kundi fulani kwenda lingine.
Kiongozi huyo wa chama cha Amani, aliongeza kuwa hatua hiyo ya upinzani kususia bidhaa hizo ni ishara yao kuonyesha hawajaridhishwa na Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, ambayo wameitaja kuwa haramu kikatiba.
“Vita vya kupigania demokrasia havijawahi kuwa rahisi. wafuasi wetu wanapaswa wakae macho na wakatae bidhaa, ambazo huenda zikawekwa kwenye pakiti tofauti na kuingizwa nchini kutoka Uganda,” alionya.
Zaidi ya hayo, NASA imesema hivi karibuni itatoa orodha nyingine ya bidhaa ambazo wafuasi wao wanaweza kutumia kama mbadala ya hizo za kususia.
Jumatatu bei ya hisa za Safaricom zilishuka kwa kuuzwa kwa Sh 25 za Kenya kutoka Ksh 25.50 Ijumaa iliyopita.
Ijapokuwa Safaricom mapema wiki hii, ilikuwa haijasema lolote kuhusu tisho hilo, Mkurugenzi wake wa Mikakati na Ubunifu Joe Ogutu,aliwahi kukaririwa akisema mivutano ya kisiasa barani Afrika husababisha kushuka kwa soko la hisa.
Kwa upande mwingine Airtel imepanga kuanzisha promosheni ikilenga watumiaji wapya katika hatua inayoonekana kuwalenga wateja watakaojitoa Safaricom.
Ukiachana na mwelekeo huo unaoweza kuathiri kampuni husika kiuchumi pamoja na maelfu ya ajira za Wakenya, je mpango huo wa ususiaji kiuchumi utafanikiwa?
Jibu linaweza kuwa ndio au hapana kutegemeana na namna NASA na wafuasi wake watakavyokaza kamba pamoja na kupata bidhaa na huduma mbadala, baada ya kuachana na zile walizozizoea.
Lakini tayari Odinga mwenyewe ameonesha hofu yake ya uwezekano wa mpango huo kuhujumiwa kutokana na rasilimali kubwa hasa pesa waliyo nayo serikali kulinganisha na upinzani.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Odinga alieleza kwamba Serikali imeanza mkakati wa kuhujumu mpango huo kwa kuwashawishi kwa fedha na vyeo viongozi wa NASA akiwamo yeye mwenyewe.
Anasema Jubilee pia inatumia matatizo ya baadhi ya viongozi wa NASA, ambao wengi wao shughuli zao zilifuatiliwa na serikali ikiwamo akaunti kufungwa kwa madai ya kukopa kodi, utakasishaji fedha na kadhalika.
Miongoni mwao ni mgombea wake mwenza Kalonzo Musyoka, ambaye taasisi yake ilifungiwa kwa madai hayo, miezi michache kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8.
Kalonzo, amepotea katika harakati za hivi karibuni za NASA tangu muungano huo utangaze kujitoa uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 na kuzua gumzo.
Lakini Raila amesema Musyoka, ambaye ni kiongozi wa chama cha Wiper, kutoka eneo la Ukambani nchini Kenya yuko Ujerumani akimuiguza mmoja wa wanafamilia.
Licha ya hayo, raila alionesha wasiwasi uwezekano wa Kalonzo kununuliwa au kupewa cheo ndani ya Jubilee ili kudhoofisha upinzani na kuunda chama kimoja chenye nguvu cha siasa.
Tayari chama cha Wiper kimeeleza kutounga mkono hatua za Raila, kikisema kimechoshwa na migomo, maadamano na mivutano ya kisiasa badala yake kinataka kujikita kujipanga kwa uchaguzi wa urais 2022, ambao kinategemea Muisyoka atagombea urais.
Wakati NASA ikisema kampuni hizo zinashirikiana na Jubilee kupora demokrasia nchini humo, Jubilee inasema kampuni hizo zinalengwa kama kulipiza kisasi kuzihujumu baada ya kugoma kutoa pesa zilizoombwa kwa vitisho na upinzani.
Jubilee kupitia Naibu Rais William Ruto, ilisema kampuni zile zitakazokubali kuipatia pesa NASA aliyosema imefilisika zitateuliwa kuwa ‘mbadala’ kwa wafuasi wa NASA kununua bidhaa zao.
Je, mpango wa NASA kuzihujumu kiuchumi kampuni hizo, kuishinikiza serikali ikubaliane na matakwa yake ikiwamo uchaguzi mpya au kunufaka kipesa kutoka ‘kampuni mbadala’ kama wanavyodai Jubilee utawezekana? ni suala la kusubiri.
Lakini kilicho wazi kwa kuangalia idadi ya wafuasi wanaomwabudu ‘baba’ Odinga, kampuni zinazosusiwa zitaathirika hasa iwapo mpango utaendelea kwa muda mrefu.
Ni wazi pia hali ikiwa hivyo, aina hii ya mikakati itaiathiri vibaya Kenya kama Taifa, ambalo tayari linaugulia katika ‘saratani mbaya’ ya ukabila huku kukiibuka harakati mpya za kutishia kujitenga, ambazo hazikuwahi wazi namna hii kuonekana kabla katika historia ya Kenya huru.
Ni wazi pia uamuzi huo utazinufaika au kutozinufaisha hata kama ni kwa muda kampuni zitakazopewa upendeleo na NASA kama mbadala kwa wafuasi wake. Kwanini unaweza usizinufaishe lakini? Kuna uwezekano wafuasi wa Jubilee nao wakalipa kisasi iwapo hatua za kutibu mgawanyiko huu hazitachukuliwa mapema.
Lakini vipi kuhusu mkakati mkuu wa NASA unaolenga kuishinikiza Serikali ya Jubilee isalimu amri kutimiza matakwa ya NASA?
Hilo ni swali gumu kulijibu mara moja, ingawa wachambuzi wengi wanaamini NASA haitafanikiwa kupata kile inachotafuta licha ya kuwa itasababisha mtikisiko au kuishia kupatikana serikali ya umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, Raila amedai hayuko tayari kwa serikali ya mseto, huku wahafidhina ndani ya Jubilee pia wakiipinga kwa kile kinachoonekana hofu ya kukosa fursa ya vyeo.
Na uamuzi huu pia unaweza ukamgharimu Odinga mwenyewe, iwapo vinara wenzake katika upinzani wataamua kumwacha aiganie vita hii ngumu peke yake, na ambayo inaonekana ni karata yake ya mwisho kisiasa.
Mwisho