Utangulizi.
LABDA wewe unaweza kuwa shahidi wa familia nyingi au hata familia unapotoka kwamba watoto wengi hupoteza ukaribu na baba zao na kuongeza ukaribu na mama zao hususani pale wazazi hawa wanapokuwa na umri mkubwa au kuanza kuzeeka.
Utakuta mara nyingi watoto wanawasiliana sana na mama, watapiga simu kwake na kutuma meseji mara kwa mara, mama ndiye atajua nini kinaendelea kwenye maisha ya watoto hata kama wako mbali na baba anabaki kupewa taarifa na mama.
Hata inapofika nyakati za watoto kuwasaidia wazazi basi mama husaidiwa zaidi kwa uwazi au hata kisirisiri wakati baba anaweza kutelekezwa au hata akisaidiwa basi ni kidogo. Je unadhani sababu kubwa ni nini? Tatizo hili mizizi yake ni ipi? Nimetamani tuliangalie kwa pamoja maana linatuhusu wote na labda wazazi wanaweza kujitambua na kubadilisha namna ya maisha ili kupunguza au kuliondoa kabisa.
Sababu:
Kwa kiasi kikubwa katika familia zetu za kiafrika hususani katika miaka 25 ya kwanza ya maisha ya watoto, wengi huwa mikononi mwa wazazi na labda baba ndio huwa mwenye nguvu kubwa katika familia, baba ndio mfalme wa familia, ndio atasema nini kifanywe na nini kisifanywe, ndio atasimamia muda wa kurudi nyumbani na hata kuadhibu kila lisilosawa kwa watoto.
Maamuzi ya mwisho huwa ni ya baba ambaye ndiye kiongozi wa familia na hali hizi huwafanya watoto kujenga hofu kubwa kwa baba yao badala ya kujenga upendo kwake. Sio tu kwenye ukali na kuadhibu lakini katika kipindi hiki baba ndiye anayelisha familia, yeye ndiye wakuhakikisha kila mtu amekula, ameshiba, amevaa nguo na analala salama.
Hii inamuongezea nguvu sio tu za kiuchumi bali hata za kihisia dhidi ya wale anaowatawala (watoto na mke) pale nyumbani, maana ukikiuka amri na sheria za nyumbani madhara yake yanaweza kuwa makubwa, unaweza kukosa chakula, au usilipiwe ada au hata kufukuzwa nyumbani. Kwahiyo utake au usitake ni lazima kuzingatia kila sheria hata kama hauzipendi.
Sio tu hofu kwa baba bali hata chuki inaweza kuota katika kipindi hiki. Baada ya kipindi hiki, watoto wanapoanza kupata kazi wakiwa bado nyumbani mama sasa huanza kupata nguvu na baadae wakianza kutawanyika na kuishi maisha yao wenyewe ndipo nguvu na mamlaka huamia mikononi mwa watoto wenyewe, sasa wanajipangia kila kitu kuhusu maisha yao, wafanye nini, waende wapi, wahusiane na nani, walale wapi n.k. Sio baba tena wala mama anayeweza kuwazuia au kuwapangia.
Watoto wanapoanza kupata fedha baada ya kuanza kazi au biashara zao binafsi, wanaanza kumjali zaidi mama kuliko baba. Wanaendeleza na kuuongeza ukaribu zaidi na mama zaidi ya baba. Bahati mbaya sana wakati baba akiwa ndio mfalme na mwenye mamlaka ya nyumba, wakati anahakikisha wote wanakula na kuishi vema alikuwa bize na kazi, alimezwa na majukumu na kusahau kuwa na muda na watoto wake.
Alikuwa amekamatwa na ajira yake kuhakikisha anapanda cheo na kupata mshahara mzuri ili watoto wasome vizuri na waishi vizuri, au alikuwa ameshikwa na biashara zake kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa ili familia isiyumbe kiiuchumi na watoto wasome. Muda wakuwa rafiki na watoto wake haukuwepo kabisa na kwahiyo kukaanza kutengenezwa mpasuko wa ukaribu wa kihisia baina ya baba na watoto wake na kwa upande mwingine wakajenga na kuongeza ukaribu wa kirafiki na kihisia na mama yao ambaye mara nyingine walimwona kama muathirika mwenzao wa ukali wa baba, maana labda watoto mara nyingine walimwona baba akiwa mkali au hata kumpiga mama mbele yao.
Hapa watoto wanajiona kama wao pamoja na mama walishiriki maumivu ya uongozi wa mabavu wa baba, na hali hiyo inawafanya kuongeza ukaribu wa kihisia zaidi, sio tu wanampenda mama bali wanasimama upande wake kumlinda na kumtetea pia dhidi ya baba na hata uhitaji na hatari nyinginezo.