25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

NI VITA YA LWANDAMINA NA PLUIJM

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo watashuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu ugenini dhidi ya wapinzani wao, Singida United, katika mchezo wa ligi hiyo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Namfua, mkoani Singida.

Katika mchezo huo, Yanga itaingia uwanjani ikifahamu kwamba inahitaji ushindi ili kuwaondoa kileleni  wapinzani wao Simba, ambao kesho wataumana na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Yanga ipo nafasi ya pili  katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 16, sawa na timu za Simba, Mtibwa na Azam FC, huku Wekundu wa Msimbazi wakiongoza kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga.

Timu hiyo imekusanya pointi hizo baada ya kushuka dimbani mara nane kwenye ligi hiyo, huku ikishinda minne na kutoka sare minne.

Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa na hasira za kukabwa koo wa watani wao wa jadi na kulazimishwa sare ya bao 1-1, katika mchezo uliochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Singida United itaingia uwanjani ikisaka pointi tatu baada ya kulazimishwa sare tasa katika mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar, uliochezwa kwenye Uwanja wa Manungu Complex, mjini Morogoro.

Timu hiyo iliyopanda daraja msimu uliopita, inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza michezo minane, ikishinda mitatu, kutoka sare minne na kupoteza mmoja.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kwa timu hizo kutokana na kila upande kutaka kushinda mchezo huo ili kulinda heshima yake na kujiweka vizuri katika msimamo wa ligi hiyo.

Mvuto zaidi wa mechi hiyo utakuwa pale kocha wa sasa wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, atakapokutana na mtangulizi wake, Mholanzi Hans Der Van Pluijm, aliyeondoka Jangwani  baada ya kuipa mataji manne timu hiyo.

Pluijm aliondoka Yanga baada ya kile kilichotajwa kutoridhishwa na maamuzi ya Wanajagwani hao kumleta Lwandamina, huku yeye akipewa cheo cha ukurugenzi wa ufundi.

Vita nyingine kati ya wachezaji wa zamani wa timu hiyo ni kiungo, Deus Kaseke na kipa, Ally Mustafa ambao wamejiunga na Singida United wakitokea Yanga msimu huu.

Mchezo huo utakuwa wa kwanza kuzikutanisha timu hizo kwenye mechi ya kimashindano, awali timu hizo zilikutana kwa mara ya kwanza katika mchezo wa kirafiki ambao ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Katika mchezo huo, Yanga itawakosa nyota wake muhimu; Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko na Donald Ngoma, ambao bado wanakabiliwa na majeruhi mbalimbali.

Kocha Mkuu wa Yanga, Lwandamina, aliliambia MTANZANIA kwamba, baada ya kukosa ushindi katika mchezo dhidi ya Simba, wamepanga kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kumaliza hasira zao.

“Baada ya kuikosakosa Simba, kikosi kiliingia kambini kwa hasira kujiandaa na mchezo dhidi ya Singida United, lengo likiwa ni kupata ushindi na kufunga mabao mengi ili kukaa juu ya wapinzani wetu wa jadi kwenye msimamo wa ligi hiyo,” alisema Lwandamina.

Kwa upande wake, Kocha wa Singida United, Pluijm, anafahamu ubora wa Yanga kwa kuwa ina wachezaji wazuri, lakini amesema kwa upande wao wamejiandaa kukabiliana nao na kubakiza pointi tatu nyumbani.

“Najua mchezo utakuwa mgumu, lakini tumejiandaa ambavyo tumekuwa tukijiandaa tunapocheza na timu nyingine, tumepania kuhakikisha tunacheza kwa umakini mkubwa ili kupata ushindi kwenye mchezo huo,” alisema Pluijm.

Mbali na mchezo huo, ligi hiyo itaendelea katika viwanja vingine vinne, ambapo Kagera Sugar itasafiri hadi Mbeya kwa ajili ya kuivaa Tanzania Prisons, mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini humo, huku Njombe Mji ikiwa nyumbani kucheza na Mbao FC, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sabasaba, mkoani Njombe.

Mechi nyingine zitaishuhudia Azam FC iliyo nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 16, itakapokuwa   nyumbani kucheza dhidi ya vibonde wa ligi hiyo, Ruvu Shooting yenye pointi tano, huku Mtibwa Sugar iliyo nafasi ya tatu na pointi 16, itasafiri hadi mkoani Mtwara kuikabili Ndanda FC inayoshikilia nafasi ya tisa ikiwa na pointi tisa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles