*Ulega aahidi neema kwa wafugaji na wavuvi
*Migogoro ya wakulima, wafugaji yatafutiwa dawa
*Sekta ya uvuvi kuundiwa mamlaka kuisimamia
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
BAJETI ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewasilishwa bungeni leo Mei 2, 2023 huku hatua kadhaa zenye lengo la kuifanya iwe na mchango zaidi kwenye Pato la Taifa (GDP) na kupambana na umasikini kwa wafugaji na wavuvi zikitangazwa.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma leo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema kwamba hatua kadhaa zikiwemo za kuongeza ukubwa wa soko la nyama na samaki ndani na nje ya nchi, ufugaji wa kisasa wenye faida zaidi kwa wafugaji, kuongeza malisho ya wanyama na samaki na kuongeza usimamizi wa sekta ya uvuvi zina lengo la kuongeza mchango wa wizara yake kwenye pato la taifa na kupunguza umasikini nchini.
“Kwa sasa, mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato letu la taifa ni takribani asilimia saba na sekta ya uvuvi ni asilimia 1.8. Kwa ujumla wizara inachangia asilimia 8.8 ya pato letu na kwa hatua hizi tunazokwenda kuchukua kupitia bajeti hii, tunaamini mchango utakuwa mkubwa zaidi,” amesema Ulega.
Tofauti na miaka ya nyuma, bajeti ya wizara hiyo mwaka huu imeibua msisimko mkubwa ndani na nje ya viunga vya Bunge la Tanzania – ikitanguliwa kabla na kile kinachoitwa “Wiki ya Protini” ikimaanisha mazao makuu ya wizara hiyo – nyama na samaki, huku kauli mbiu ya mwaka huu, “MifugoNaUvuviNiUtajiri” ikiwa inatawala katika mitandao ya kijamii kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita.
Hii ni bajeti ya kwanza kutangazwa na Ulega akiwa Waziri kamili tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Februari mwaka huu. Katika hotuba yake hiyo, mbunge huyo wa Mkuranga aliliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024 yenye thamani ya Sh bilioni 295.9. Katika fedha hizo, kiasi cha shilingi bilioni 112 kitatumika kwenye sekta ya mifugo huku shilingi bilioni 183 kikienda sekta ya uvuvi.
Waziri huyo kijana alitumia hotuba yake ya bajeti kupongeza jitihada binafsi zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kufungua soko la biashara ya nyama katika nchi za kiarabu – ambako alisema biashara ya nyama imeongezeka kwa takribani asilimia 46 ndani ya miaka miwili ya kwanza ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita.
“Tanzania haikushiriki Kombe la Dunia mwaka jana nchini Qatar kwa maana ya kucheza lakini kutokana na diplomasia ya uchumi ya mheshimiwa Rais, Tanzania ilifanya biashara kubwa ya nyama wakati huo kuliko wakati mwingine wowote kwenye historia yetu. Sasa tunaambiwa hata tukiuza ng’ombe wetu wote waliopo hapa Tanzania, bado hatutaweza kukidhi kiu ya wateja wa nyama yetu huko uarabuni. Namshukuru sana mhe Rais kwa kutufungulia njia,” alisema Ulega.
Kulinganisha na bajeti iliyopita ya wizara hiyo, safari hii bajeti imejikita zaidi katika masuala yatakayoongeza tija kwenye mifugo na uvuvi na imejielekeza katika kuifanya wizara kuwa na mwelekeo wa kibiashara zaidi na unaotaka faida ya kuwa na mifugo mingi na samaki wengi ionekane.
Kwa mfano, Ulega aliliambia Bunge jana kwamba wizara yake itafanya uwekezaji mkubwa katika eneo la ukuzaji wa majani kwa ajili ya ng’ombe, lengo likiwa kuhakikisha mifugo inakuwa na chakula cha uhakika na pia nchi kuweza kuuza nje kwani ziko nchi zina shida ya majani.
“Kuna ofa tayari kutoka kwa wenzetu wa Saudi Arabia wanaotaka kununua aina fulani ya majani ya mifugo kutoka kwetu. Kama mambo yatakwenda vizuri, watu wetu watalima hapa na kupata soko la uhakika. Muda si mrefu, majani yanaenda kuwa biashara nzuri ya kutuingizia fedha za kigeni hapa kwetu,” amesema Ulega.
Akizungumza kwa kujiamini na kuonyesha uelewa mkubwa wa masuala ya wizara yake, Ulega alisema suala la kuwa na malisho ya kutosha kwa wanyama litapunguza migogoro ya mara kwa mara baina ya wakulima na wafugaji; akisema chanzo chake kikubwa huwa ni ukosefu wa malisho.
Ulega alitumia pia sehemu kubwa ya hotuba yake ya jana kufafanua kwa kina suala la sababu za kusudio la wizara yake kuanzishwa chombo cha usimamizi wa sekta ya uvuvi; akisema kwa hali ilivyo sasa, mfumo hausaidii sana usimamizi wa sekta hiyo.
“Nchi yetu ina maziwa, mito na bahari na kote huko uvuvi unafanyika. Wizara ina watu wanaosimamia eneo hilo lakini nadhani tunahitaji kuwa na chombo – kama ilivyo kwa Ewura kwenye mafuta, ambacho watu wake watakuwa wakilala na kuamka wanaangalia masuala ya samaki tu. Samaki ni rasilimali muhimu sana na ni muhimu kuipa umuhimu inaostahili,” amesema.
Waziri huyo alilitangazia Bunge jana kwamba serikali itaendelea na mipango iliyoanza kwenye bajeti za nyuma ikiwamo kununua boti kwa ajili ya kusaidia uvuvi kwenye maji ya kina kirefu, kutoa mikopo kwa wavuvi ili kuwawezesha kununua vifaa vya kisasa vya uvuvi na kuanza ujenzi wa bandari ya uvuvi huko Kilwa.
Mbali na hotuba ya bajeti, jana wadau mbalimbali wa wizara ya mifugo na uvuvi walionyesha bidhaa zao kwa wabunge na wageni wengine kupitia mabanda maalumu yaliyowekwa kwenye viwanja vya Bunge na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alitembelea mabanda hayo na kufanya uzinduzi rasmi wa Wiki ya Protini.
Wabunge walianza kuchangia hotuba hiyo jana jioni na kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bunge ya shughuli za wiki hii, mjadala huo utaendelea hadi leo ambako Waziri Ulega anatarajiwa kufanya majumuisho ya jumla baada ya kusikiliza hoja za wabunge watakaochangia.