Na MWANDISHI WETU-DODOMA
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa siku 14 kwa mashirika yasiyo ya serikali nchini kuhakikisha yanawasilisha taarifa za miradi na za fedha za mwaka 2016 na 2017 zilizokaguliwa kwa Msajili wa Mashirika ama sivyo yatafutiwa usajili wao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dk. John Jingu, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa kwa mashirika hayo.
“Septemba 28, 2018, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Faustine Ndugulile alikutana na wawakilishi wa vyombo vya habari na kutoa maagizo ya kuyataka mashirika yasiyo ya serikali kuwasilisha taalifa zao kwa mashirika hayo ikiwa ni pamoja na taarifa za miradi na taarifa za fedha zilizokaguliwa kwa mwaka 2017 na 2018,” alisema Dk. Jingu.
Alisema maagizo hayo yalipaswa kutekelezwa ndani ya siku 30 kuanzia Septemba 28, mwaka huu.
Hata hivyo imeelezwa kuwa mwitikio wa utekelezaji umekuwa wa kuridhisha kutokana na ukweli kuwa mashirika mengi yamezingatia maelekezo ya Serikali.
Wizara pia imepokea maombi kutoka Ofisi ya Baraza la Taifa la NGOs na baadhi ya mashirika yasiyo ya serikali yakiomba kuongezwa muda kidogo yaweze kukamilisha maandalizi ya taarifa zao na kuziwasilisha haraka.
“Kutokana na kutambua nafasi ya NGOs katika maendeleo ya taifa, Serikali imeridhia kuongeza siku 14 kuanzia leo (jana) kuwapa fursa wale ambao walikuwa hawajatimiza maelekezo hayo kutokana na sababu mbalimbali kufanya hivyo.
“Nasisitiza kuwa hakutakuwa na muda mwingine wa nyongeza kwa wale ambao hawatakuwa wamewasilisha taarifa hizo ndani ya muda wa nyongeza.
“Shirika ambalo litakuwa halijawasilisha taarifa wizara itachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisisitiza Dk. Jingu.
Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Ismail Suleiman, aliishukuru Serikali kwa kuridhia ombi la kuongeza muda wa kuwasilisha taarifa za fedha na miradi kuwezesha NGOs kutimiza matakwa ya agizo hilo.
Alisema kanuni mpya za NGOs (2018) zilizotangazwa Oktoba 19, mwaka huu kwa kiasi kikubwa zimezingatia utekelezaji wa kanuni za maadili.