KWA miaka mingi sasa mgodi wa North Mara umekuwa ukilalamikiwa na wananchi wanaouzunguka kwa kile wanachodai kuna maji yenye sumu yanatiririshwa kwenda yalipo makazi ya watu.
Maji hayo yanayodaiwa kuwa kemikali zinazotumika katika shughuli zote za uchimbaji, yamekuwa na athari kubwa kwa binadamu ambao wakati mwingine wanakwenda kuchota maji ya Mto Thigite kwa matumizi yao ya kila siku.
Ni miaka mingi sasa kumekuwapo na malalalamiko ya aina hii, huku wananchi kadhaa wakionyesha miili iliyochubuka kwa kile wanachodai ni athari zinazokana na maji hayo.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua kukabiliana na tatizo hili, lakini hadi sasa hakuna jibu la msingi lililopatikana juu ya maji hayo ambayo yanapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kina.
Hali hii imemsukuma Rais Dk. John Magufuli kuliagiza Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupeleka timu yake ya wataalamu kuanza uchunguzi mara moja ili kubaini ukweli wa tatizo hili.
Rais Magufuli amefikia uamuzi huu baada ya kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime wiki iliyopita, ambako moja ya kilio kikubwa cha wananchi kilikuwa maji hayo.
Tunaamini maagizo ya Rais kwa baraza hili yanaweza kuja na jibu la msingi, ili kilio cha maji hayo yanayodaiwa kuwa sumu ambayo inasababisha uharibifu wa mazingira na madhara kwa afya za wananchi wanaotumia maji ya Mto Thigite kipatiwe ufumbuzi.
Tumefurahi kuona Rais amesikia kilio cha wananchi ambao kwa miaka kadhaa sasa wamejikuta wakichubuka ngozi na mimea kushindwa kustawi kama ilivyokuwa mwanzoni.
Pamoja na ukweli kuwa timu ya uchunguzi imeanza kazi yake, wananchi hawa wamekuwa na malalamiko ya msingi yakiwamo ya mifugo yao kufa, hasa ng’ombe na mbuzi kwa sababu mara nyingi wanakimbilia Mto Thigeti kunywa maji wakati wa malisho.
Hali hii imesababisha umasikini mkubwa kwa wananchi wanaotegemea mifugo yao kuendesha maisha yao, ikiwamo kusomesha watoto katika shule mbalimbali.
Lakini jambo la kusikitisha kilio kuhusu maji haya ni cha muda mrefu, kwa miaka mingi tumeshuhudia viongozi wakiwamo wa kitaifa, mkoa, wilaya na kamati za Bunge wakienda eneo hili lakini hakuna ufumbuzi.
Sisi MTANZANIA tunasema huu ndio wakati wa NEMC kuja na majibu sahihi ambayo yatawaondolea Watanzania wenzetu kadhia hii ambayo wameteseka nayo kwa muda mrefu.
Tunaamini timu hii ya uchunguzi itakuja na majibu sahihi ambayo yatasaidia kuondoa au kumaliza kero hii. Tunaishauri timu ya uchunguzi kupitia kwa kina miundombinu ya mgodi huu kama kweli inakidhi matakwa yanayotakiwa kisheria katika shughuli za uchimbaji wa dhahabu.