25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

NEC YAVITAKA VYAMA KUFUATA TARATIBU

tume ya taifa ya uchaguzi

Na AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa kufuata taratibu za kisheria endapo ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi utatokea katika kampeni za uchaguzi mdogo zinazoendelea nchini ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima, baada ya Chama cha ACT-Wazalendo kuwataja watendaji wa Serikali ya Kata ya Nkome mkoani Geita kuwaandikisha wazee ili kuwapatia huduma za afya bure wakiwa na kadi za kupigia kura kinyume na taratibu za uchaguzi.

Kailima alisema NEC imeyapata malalamiko hayo kupitia vyombo vya habari yanayoonyesha watendaji wa umma na vyombo vya dola kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Kwa kuzingatia sehemu ya 5.4 ya Maadili ya Uchaguzi, NEC inavikumbusha vyama vya siasa kuwa iwapo vina malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi katika uchaguzi mdogo wa udiwani kuwasilisha malalamiko hayo katika kamati ya maadili ya kata saa 72 tangu ukiukwaji huo umefanyika,” alisema.

Kailima alisema endapo chama cha siasa au mgombea wa nafasi husika katika kampeni za uchaguzi mdogo anaamini maadili ya uchaguzi yamekiukwa awasilishe malalamiko yake katika kamati ya maadili ya ngazi husika.

“Hivyo tunakishauri ACT na vyama vingine kuwasilisha malalamiko ya ukiukwaji wa maadili katika kamati husika,” alisema.

Pia alisema kwa kuzingatia sehemu ya 5.7(a) ya maadili ya uchaguzi, endapo mgombea au chama atakuwa hajaridhishwa na uamuzi wa kamati ya maadili ya ngazi ya kata anaweza kuwasilisha malalamiko yake katika ngazi ya msimamizi wa jimbo.

Alisema malalamiko hayo yanapaswa kuwasilishwa ndani ya saa 24 baada ya uamuzi wa kamati ya kata kutolewa.

Alisema endapo chama kitakuwa hakijaridhishwa na uamuzi wa ngazi ya jimbo wana uwezo wa kuwasilisha rufaa hiyo katika Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa au rufaa ambazo ni NEC kwa kuzingatia sehemu ya 5.7(b) na (c).

Alisema kwa mujibu wa sehemu ya 5.7(e) ya maadili ya uchaguzi, kama mgombea au chama atakuwa hajaridhishwa na uamuzi wa kamati ya rufaa atakuwa na fursa ya kuwasilisha malalamiko hayo mahakamani baada ya uchaguzi.

Alisema malalamiko hayo yatawasilishwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi sura 343 na sheria ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa sura namba 292.

Kailima pia alisema kwamba, ni kosa kumiliki kadi ya kura isiyokuwa yako chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya uchaguzi sura ya 292 kifungu cha 100 cha sheria ya uchaguzi ya Serikali za Mitaa sura ya 292.

Aliwasihi wanasiasa na wadau wengine wa uchaguzi kuendelea na kampeni za kistaarabu za kuzingati sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi kwa kuwa ofisi hiyo haitasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayekiuka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles