24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Nani kuingia nusu fainali Uefa wiki hii?

BADI MCHOMOLO, DAR ES SALAAM 

MTOTO hatumwi dukani, ndio kauli ambayo inaweza kutumika wiki hii kuelekea michezo ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali, huku miamba minne ikitarajia kuyaaga mashindano hayo na mingine minne kuingia nusu fainali.

Timu nane ambazo zimeingia hatua ya robo fainali ni pamoja na Tottenham, Manchester City, Barcelona, Ajax, Juventus, Liverpool, FC Porto na Manchester United.

Kila timu inapigania nafasi ya kuingia hatua ya nusu fainali kati ya timu hizo, nani atafanikiwa? SPOTIKIKI imekufanyia uchambuzi na kuzipa nafasi timu ambazo zinaweza kufuzu kutokana na kile walichokifanya katika mchezo wao wa awali.

Juventus vs Ajax

Huu ni moja kati ya mchezo ambao utakuwa na ushindani wa hali ya juu. Bado Ajax wanapigania kulipa kisasi kwa kile kilichotokea mwaka 1996 ambapo timu hizo zilifika fainali na mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1 kabla ya Ajax kupoteza kwa mikwaju 4-2 ya penalti.

Katika mchezo ambao ulipigwa wiki iliopita huku Ajax wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani, walilazimishwa sare ya bao 1-1, lakini walicheza soka la hali ya juu na kupoteza nafasi nyingi.

Ugumu wa mchezo huo wa kesho utatokana na kuwaruhusu wapinzani wao kupata bao katika mchezo uliopita, lakini chochote kinaweza kutokea endapo Ajax wataweza kuyafanyia kazi makosa yao.

Juventus hawakuwa bora sana kwenye mchezo uliopita, lakini ubora wa mshambuliaji wao Cristiano Ronaldo ambaye alikuwa majeruhi kwa wiki kadhaa, aliweza kuwatafutia bao Juventus.

Lakini mchezo huo wa marudiano utakuwa wa marudiano huku Ajax wakiamini wanaweza kupindua matokeo kwenye uwanja wa ugenini.

Barcelona vs Man United

Huu ni mchezo ambao utakuwa na mvuto wa aina yake, baada ya mchezo wa wiki iliopita kumalizika kwa Barcelona kushinda bao 1-0 kwenye uwanja wa Old Trafford.

Manchester United wanaamini wanaweza kwenda kupindua matokeo kesho kwenye uwanja huo wa Camp Nou, lakini haitokuwa kazi rahisi.

Barcelona wamekuwa na histori kubwa ya kuwafunga Man United kwenye michuano hiyo mikubwa ya Ligi ya Mabingwa, waliwahi kufanya hivyo katika mchezo wa fainali mwaka 2009 ambapo Barcelona ilishinda kwa mabao 2-0, yakifungwa na Samuel Eto’o na Lionel Messi.

Mwaka uliofuata Barcelona ilishinda tena mabao 3-1 katika mchezo wa fainali, huku mabao hayo yakifungwa na Messi, Pedro Rodriguez na David Villa, huku bao la Man United likifungwa na Wayne Rooney.

Kwa sasa Barcelona hawana cha kupoteza katika michuano ya Ligi Kuu nchini Hispania, huku ikiongoza kwenye msimamo wa Ligi kwa pointi 73 wakifuatiwa na Atletico Madrid wenye pointi 62 na Real Madrid wenye pointi 60 baada ya timu hizo kucheza michezo 31.

Kwa michezo iliobaki Barcelona wana nafasi kubwa ya kushinda taji hilo, hivyo nguvu zao kwa sasa wanazihamishia kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kutokana na hali hiyo, Barcelona lazima wahakikishe wanashusha kikosi chake kamili ili waweze kushinda bila ya wasiwasi mbele ya mashabiki wao, lakini hata United wana nafasi kubwa ya kufanya makubwa huku wakiwa ugenini kama walivyofanya katika mchezo dhidi ya PSG katika hatua ya 16 bora huko nchini Ufaransa.

Man City vs Tottenham

Msimu huu timu nne za Ligi Kuu England zilifanikiwa kuingia hatua hiyo, lakini katika mchezo wa kesho kutwa zipo ambazo zitayaaga mashindano hayo hasa kati ya Manchester City au Tottenham.

Mchezo uliopita Tottenham walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani na kufanikiwa kushinda bao 1-0, huku Manchester City wakikosa bao kwa mkwaju wa penalti kutoka kwa Sergio Aguero, lakini walipoteza nafasi mbalimbali.

Manchester City walionekana kushusha kikosi ambacho hakikuwa na makali kwa Tottenham kwa kuwa walikuwa wanauangalia mchezo wa jana dhidi ya Crystal Palace.

Manchester City walikuwa wanajiandaa na mchezo dhidi ya Crystal Palace ambao walishinda katika mchezo wao wa mzunguko wa kwanza ambao Man City walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Etihad na kukubali kichapo cha mabao 3-2, Desemba 22, mwaka jana, hivyo walikuwa wanajiandaa kwa ajili ya kulipa kisasi.

Mchezo wa kesho kutwa Manchester City wanaweza kushusha kikosi kamili kwa ajili ya kupigania nafasi ya kuingia nusu fainali, huku Tottenham wakipambana kulinda bao lao na ikiwezekana kuongeza bao lingine.

Man City wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye uwanja huo wa nyumbani hasa kutokana na ubora wao katika safu ya kiungo na ushambuliaji.

Porto vs Liverpool

Tangu msimu uliopita, FC Porto wamekuwa katika kipindi kigumu wanapokutana na Liverpool, katika hatua ya 16 bora Liverpool ilishinda jumla ya mabao 5-0 dhidi ya wapinzani hao msimu uliopita.

Katika mchezo wa wiki iliopita pia Liverpool waliendeleza ubabe wao na kushinda mabao 2-0 huku Porto wakiwa kwenye uwanja wa ugenini, lakini kesho kutwa watakuwa kwenye uwanja wa nyumbani na kupambana na timu hiyo inayowania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Bado Liverpool wanapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo huo kutokana na ubora wao kwa misimu hii miwili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles