Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI (NACOPHA) limetakiwa kujenga umoja na kuimarisha ushirikiano baina yake na mitandao ya WAVIU ili kurahisisha uratibu na mgawanyo wa raslimali kwa walengwa.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam jana Ijumaa Julai 23, 2021 na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko, alipotembelea Ofisi za NACOPHA ikiwa ni sehemu yake ya uratibu na utekelezaji wa majukumu ya tume.
Akizungumzia lengo la ziara hiyo, Dk. Maboko amesema pamoja na sehemu ya uratibu wa Mwitikio wa UKIMWI pia ililenga kujifunza na kujua namna taasisi ya NACOPHA inavyotekeleza majukumu yake.
“Nimetembelea NACOPHA leo ikiwa ni sehemu ya ofisi yangu ya uratibu shughuli za mwitikio wa UKIMWI lakini pia kujifunza utekelezaji wa shughuli zenu kama kauli mbiu yenu inavyosema, hebu tuyajenga. Sasa mimi nasema, tuzungumze na kuyajenga pamoja.
“WAVIU wamekuwa na mitandao mingi ambayo kila mmoja anahitaji kufanya kazi na TACAIDS moja kwa moja jambo ambalo haliwezi kuleta utekelezaji wenye ufanisi, NACOPHA ipo hapa kwa ajili ya kuwaunganisha WAVIU wote nchini na kama kuna fursa yoyote inakuwa rahisi kwa walengwa kunufaika kwa kuwa NACOPHA itakuwa inaelewa mtandao upi unafanya nini,” amesema Dk. Maboko na kuongeza kuwa:
“Sitaki kuona migawanyiko, NACOPHA ifanyekazi inayofikia malengo ya uanzishwaji wake, ikiwezekana kuwe na Idara na vitengo au dawati ili kuweza kufikia walengwa wote.
“Kwani kwa kufanya hivyo inasaidia kurahisisha utekelezaji ili mhitaji akija hapa anaelekea moja kwa moja kwenye dawati husika,” ameongeza Dk. Maboko.
Aidha, amewataka WAVIU kuhamasishana kukata bima ya afya kwani ni haki ya kila Mtanzania na kwamba itapunguza changamoto za kupata matibabu au kuhofia kwenda hospitali kupata huduma kwa kuhofia gharama za matibabu.
Dk. Maboko pia amewataka WAVIU kuedelea kujiunga katika vikundi vilivyopo katika halmashauri zao ili kurahisisha upatikanaji wa fedha za mikopo zinazotolewa na serikali kupitia halmashauri na vikundi vya ujasiliamali.
“Fedha hizi ni kwa ajili ya Watanzania sio vyema kusubiri hadi litengwe fungu la WAVIU, huu mgawanyo uliopo unatosha kwani hata WAVIU wapo katika makundi hayo, kwa kutaka mgawanyo maalum wa WAVIU ni kuendeleza unyanyapaa, jambo ambalo hatupaswi kulipa nafasi,” amesema Dk. Maboko na kuainisha makundi hayo kuwa ni ya wanawake, vijana na walemavu ambapo hata kwa WAVIU watu hao wapo.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa NACOPHA, Deogratius Rutatwa amemshukuru, Dk. Maboko kwa ushirikiano na usimamizi anao utoa kwa NACOPHA katika kuhakikisha majukumu yanatekelezeka kwa ufanisi.
“Imekuwa ni jambo la faraja kwa ushirikiano huu unaotupatia katika kuhakikisha kuwa tunatekeleza majukumu yetu kwa ufanisi, pia naishukuru TACAIDS kwa wazo la kuanzisha NACOPHA ambayo leo hii ndio chombo kikubwa cha kuratibu WAVIU wote nchini.
“Pia nikuhakikishie tu kwamba tutatekeleza ushauri ulioutoa ambao unalenga kuboresha utekelezaji wa majukumu yetu,” amesema Rutatwa.
Awali Mwenyekiti wa Taifa wa Watu wanaoishi na VVU, Leticia Kapela, amesema NACOPHA ni jukwaa la uratibu utetezi na uraghibishi wa juhudi zote za WAVIU katika mwitikio wa UKIMWI.
Hata hivyo, kwa mujibu wa tafiti bado kuna haja ya kuendelea kuhamasisha wanaume kupima afya zao ili kujua hali ya maambukizi, kwani inaonesha bado mwitikio wa wanaume kupima unadorora.