28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mwigulu atoa majiko 900 kwa mama na baba lishe Iramba

Na Seif Takaza, Iramba

MBUNGE wa Iramba Magharibi, Dk. Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Waziri wa Fedha ametoa majiko ya gesi 900 kwa Mama lishe na Baba lishe kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mitungi hiyo iliyofanyika juzi katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya hiyo kwa niaba ya Dk. Nchemba alisema mitungi hiyo imetolewa na mbunge huyo kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za utunzaji wa mazingira kazi ambayo aliianza tangu alipokuwa Makamu wa Rais.

“Mhe. Mbunge alituita Dodoma mimi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya, Innocent Msengi na kutueleza kuwa amefanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania ambao watatusaidia kutupatia mitungi ya gesi lengo kuu likiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia alizozianza tangu akiwa Makamu wa Rais za kulinda na kutunza mazingira,” alisema Mwenda.

Alisema kulingana na kumbukumbu za wanamazingira nchini, zinaonesha kuwa uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokea unatokana na ukataji wa miti mikubwa inayohitajika kwa ajili ya nishati ya kupikia (kuni).

Alisema takwimu hizo zinatishia na kuonesha wazi kuwa tukiendelea na utaratibu huo wa ukataji miti kwa ajili ya nishati hiyo ya kupikia ifikapo miaka 10 hadi 20 ijayo nchi itabadilika na kuwa jangwa.

Mwenda alisema kutokana na hali hiyo Dk. Nchemba ameziiunga mkono juhudi hizo za rais na kuwataka kupanda miti ya kutosha kwa ajili ya kulinda tabia nchi na ndio sababu iliyomfanya azungumze na viongozi wa kampuni ya Oryx ambao walikubali kumpa mitungi ya gesi 700 na wao wakatoa mingine 200 na kufanya jumla ya mitungi kuwa 900 ambayo itatumiwa na wananchi wa wilaya hiyo badala ya kutumia mkaa na kuni kwani nao wameguswa na athari za uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Oryx Tanzania, Benoit Araman alisema kuanzia Julai, 2021 kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele kutekeleza maelekezo ya serikali waliyoyapokea kutoka kwa rais kuwa ifikapo mwaka 2023 wananchi wote wa Tanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Alisema kupitia mipango hiyo Oryx imepanga kutokomeza kabisa matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ambayo siyo mbaya kwa afya za watu bali pia ni hatari kwa uharibifu wa mazingira Mkurugenzi huyo mkazi wa kampuni ya Oryx Tanzania alisema wanajipongeza kwa kuwa kinara wa usambazaji wa gesi.

Baadhi ya wananchi waliopata mitungi hiyo ya gesi wakiwemo viongozi wa dini waliipongeza kampuni ya oryx kwa kutoa mitungi hiyo ambayo itasaidia kutunza mazingira na kuacha kabisa matumizi ya nishati ya kuni na mkaa.

Askofu Robert Lugiko wa Kanisa la Baptisti Tanzania, Jimbo la Singida, akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini, alimshukuru Rais Samia na kampuni hiyo kwa kutoa mitungi hiyo ya gesi na kuwa matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa yakiwaathiri sana wanawake na kueleza kuwa kuanzia sasa anakwenda kuwa balozi wa kuhimiza matumizi ya nishati ya gesi kwa ajili ya utunzaji wa mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles