Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ameibua maswali mapya juu ya sakata la kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kutokana na kauli zake.
Kauli hizo za Mwigulu zinazodaiwa kuibua maswali, ni pamoja na ile ya kusema, gari ambalo Lissu alidai lilikuwa likimfuatilia akiwa Dar es Salaam, lipo Arusha na halijawahi kufika Dar es Saalam.
Kauli nyingine ni ile ya kusema katika upelelezi wa sakata la Lissu, hadi sasa magari 10 yanayofanana na linalodaiwa kubeba watu waliomshambulia Lissu yamekamatwa na Jeshi la Polisi.
GARI DOGO
Mwigulu akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds jana, alisema gari dogo ambalo Lissu alisema limekuwa likimfuatilia katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, liko Arusha na halijawahi kufanya mizunguko ya aina yoyote jijini Dar es Salaam.
“Utoaji wa taarifa na wenyewe haukuwa rasmi, kwa mfano Lissu aliposema kuna gari inamfuatilia, nilielekeza polisi wakaifuatilia, ikakutwa Arusha kuna gari ndogo ya namba hizo, kwa hiyo kuna moja iliweka namba batili.
“Ile gari ilikutwa kule kule na haikuwa na ruti za huku (Dar es Salaam) huwa iko kule kule, kwa hiyo kwenye mambo haya ndiyo maana tunahitaji sana ushirikiano.
“Natamani hawa wasiojulikana tungewatia nguvuni pale pale. Kama ningepewa tip (taarifa) mapema, tungefuatilia hili na kitendawili cha watu wasiojulikana tungekitegua mara moja,” alisema Mwigulu.
Alisema Lissu mwenyewe anaweza kusaidia uchunguzi katika tukio hilo kwani ameshuhudia mengi.
“Watu wasiojulikana nawatafutia dawa ili wajulikane, hata wanapokimbilia sehemu zisizojulikana na suala la Lissu lipo ofisini kwangu naendelea kulifanyia kazi.
“Nikisema sasa hivi uchunguzi umefikia wapi, nitakuwa naingilia uchunguzi ambao unaendelea hivyo ni vyema tukafanya kazi hii kwa umakini mkubwa,’’ alisema.
Mwigulu pia alisema: “Sisi kama taifa tunatambua nchi yetu iko kwenye vita ya kiuchumi, sidhani kama kuna wengine wanaweza kuturudisha nyuma, ni vizuri tukashirishana ili kutatua hilo” alisema.
Kuhusu upelelezi wa kesi ya Lissu, Mwigulu alisema ikifika muda mwafaka watasema kila kitu ingawa hadi sasa wamekamata zaidi ya magari 10 yanayofanana na lililobeba watu waliomshambulia Lissu.
Uchunguzi wa nje
Akizungumzia uchunguzi wa tukio la Lissu kufanyikwa na vyombo vya nje, Mwigulu alisema. “ Tusingepanda kuitangazia dunia kuwa jukumu la kulinda raia wetu limetushinda, hili litakuwa jambo la mwisho kabisa, na lazima damu inayomwagika adhabu yake iwe kubwa zaidi.
“Tukishafanya kawaida kawaida, lawama zinakwenda kwa serikali, na kama tutaacha mambo yananing’ing’inia, watu watafanya hiyo kama fursa, kwa mfano kwenye matukio mengi kama kifo cha Mtikila (Mchungaji Christopher Mtikila), Mawazo (Alphonce Mawazo, aliyekuwa kiongozi wa Chadema, Geita),” alisema.
Baada ya maelezo hayo, aliulizwa iweje wafanye uchunguzi wa kifo cha Mtikila wakati kilitokana na ajali, Mwigulu alijibu “ni sawa ni ajali, lakini utakumbuka ilileta mjadala, kwa hiyo lazima tofanye uchunguzi,” alisema
CHADEMA WAIBUKA
Wakati Mwigulu akisema hayo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, akizungumza na Mtanzania aliibua maswali kuhusiana na kauli za Mwigulu, akisema waziri huyo amewashangaza.
Baadhi ya maswali yaliyoibuliwa na Mrema ni pamoja na vipi alijua gari ambalo Lissu alisema lilimfuatilia akiwa Dar halijawahi kufika Dar es Salaam ili hali nchi haina kamera barabarani wala kwenye mitaa.
Pia alihoji ni kwa namna gani waziri huyo anasema magari yanayofanana na lililokuwa limebeba watu waliomshambulia Lissu yamekamatwa 10, huku kukiwa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusika na shambulio hilo.
“Kwanza namshangaa huyu waziri, hivi hajui kwamba barabara za nchi hakuna kamera? Pia katika mitaa ya mikoani na Dar pia hakuna kamera, hajui hili? Kama Waziri wa Mambo ya Ndani hatambui hili, basi ni hatari sana,’’
“Nahisi labda waziri hakumsikia Lissu Agosti 18 alipofanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa kuna watu wanaomfuatilia na kwamba akiwa maeneo ya Protea Hoteli, aliwaona wakiwa na gari namba T 460 ACV na kuwaambia waache kumfuatilia kila anapokwenda,’’alieleza Mrema.
Kuhusu hatua za upepelezi na kufanikiwa kukamata magari 10, Mrema alihoji magari hayo yanashikiliwaje bila kuwa na watu wanaoyamiliki ama kuyaendesha.
“Yalikuwa yakijiendesha yenyewe? Kama yalikuwa na watu je watu hao wanashiliwa mpaka sasa?,” alihoji.
Alisema ni mkanganyiko kama aliouibua Mwigulu, ndio unaofanya Chadema itake suala hilo lichunguzwe na vyombo vya nje ya nchi.
NAPE KUTISHIWA
Mwiguli akizungumzia tukio la Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, kutishiwa bastola hadharani jijini Dar es Salaam, alisema aliyemtishia hakuwa askari isipokuwa ni mhalifu kama wahalifu wengine.
“Kijana huyo alikuwa ni mhalifu tu aliyetumia nafasi ya mkutano wa Nape na waandishi wa habari kutaka kutekeleza tukio hilo ambapo aliishia kumtishia bastola.
“Awali tulidhani yule kijana ni polisi, lakini hakuwa na sare za polisi, cha kwanza nilimwelekeza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kufuatilia na akaleta majibu kuwa hakuwa polisi,” alisema.
Alisema kwa nafasi aliyokuwa nayo Nape kwa wakati huo, wahalifu huwa wanatumia fursa ya kufanya matukio kama hayo.
“Kwenye nchi ambazo wamepitia misukosuko unakutana na askari ana silaha zote, hata kwenye matukio kama hayo alipomvamia Nape ambaye bado alikuwa na gari ya wizara, hatukuwa tutategemea uhalifu, tungekuwa tunategemea uhalifu ule kutokea, tungemlinda,” alisema.
Pamoja na mambo mengine Mwigulu alisema masuala kama haya ambayo yanabeba hisia za watu, wizara inachukua hatua ambazo si zote zinawekwa wazi.
BEN SANANE
Kuhusu kupotea kwa aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema taifa, Ben Sanane, Mwigulu alisema ni ngumu kulisema kama yuko hai au amefariki dunia, kwani polisi bado wanaendelea na uchunguzi.
“Kwa aina ya taarifa ninazopata ni kama inaelekea kufikia ukomo, ni jambo ambalo tumelipa uzito kulifanyia kazi, na Mtanzania yeyote mwenye nia njema anaweza kutusaidia kufuatilia,” alisema.
“Likishatokea jambo kama hili ambalo si la kawaida, ni lazima tulifanyie kazi, hata kwenye kamati ni moja ya jambo tulilozungumza sana, Ben Sanane, anasababisha watu wanauliza kwa sababu kuna vitu vinaning’inia,” alisema.
Mrema akizungumzia suala hilo, alisema sasa ni takribani mwaka hakuna kinachoendelea licha ya familia ya Saanane kuomba Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuangalia simu za mwisho zilizotumika kumpigia.