Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kheri James, amewaonya wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali nchini wanaokwamisha maslahi ya vijana.
Kiongozi huyo alisema, hatawachekea wakurugenzi na madiwani wa halmashauri nchini watakaoshindwa kutenga asilimia tano ya fedha za mikopo kwa ajili ya maendeleo ya vijana.
Alisema wakurugenzi na madiwani ni miongoni mwa watendaji wanaokwamisha mikopo ya vijana katika halmashauri zao, huku wakijua fedha hizo zinatolewa kwa mujibu wa sheria.
James alitoa onyo hilo jana alipofanya ziara katika Ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Limited zilizopo Sinza Kijiweni Dar es Salaam, ambao ni wachapishaji wa magazeti ya MTANZANIA, Rai, Dimba na Bingwa.
Mwenyekiti huyo mpya wa vijana alisema vijana wasipopata mikopo hiyo wanaweza kumalizia hasira zao kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwa kuwakataa.
“Hizi fedha zinatolewa kwa mujibu wa sheria, niwaambie wakurugenzi na madiwani kwamba wasianze kujadili kuhusu matumizi ya fedha hizo ambazo ni asilimia tano ya makusanyo yote ya halmashauri, niwaambie wazi katika hili tutatofautiana kauli.
“Niliwaambia vijana msicheke na viongozi wa serikali ambao wanacheza na kukwamisha fedha hizi, tunaona madiwani pia wanachangia kwa kiwango kikubwa sana hizo fedha kuhamishiwa.
“Baadhi ya halmashauri madiwani wanashirikiana na wakurugenzi kubadili matumizi ya fedha hizo, nasema vijana hawa mnaowaumiza leo kwa kuwanyima fedha kesho ni zamu yenu kuumizwa mwaka 2020 siyo mbali,” alisema James.
Kuhusu mikakati yake ya kujenga jumuiya hiyo, alisema anatambua jukumu la UVCCM ni pamoja na kusimamia sera na ilani ya uchaguzi ambayo ni ahadi kwa wanachama na wasiokuwa wanachama.
Alisema ni kundi pekee linaloweza kuiambia Serikali kwa lugha ambayo imenyooka juu ya sera mbalimbali kwa kuwa anaamini UVCCM ikisema ni vijana wote Tanzania wamesema.
Alisema mkakati mwingine alionao ni pamoja na kuifanya jumuiya hiyo kuwa mawakili kuhakikisha wanachukua jukumu la kuwaunganisha vijana wote nchini, huku wakiwa na jukumu jingine kubwa la kuhakikisha CCM inachukua ushindi wakati wa uchaguzi.
“Ni jukumu letu kuhakikisha CCM inashinda kwa gharama zozote, ‘come rain come sun’ kuhakikisha ushindi kwa mujibu wa sheria,” alisisitiza.
Hata hivyo James alisema hatasita kusitisha mishahara isiyokuwa na tija inayolipwa kwa baadhi ya watumishi, ambapo inadaiwa kuwa katika makao makuu ya umoja huo kuna watumishi ………….
Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya MTANZANIA.