29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanamke aliyekatwa mikono na mumewe kwa kukosa mtoto

hands cut2NAIROBI, KENYA

SIKU hizi watu wamegeuka kuwa kama wanyama. Wanafanya vitendo vya kikatili ambavyo kwa akili ya kawaida mwanadamu huwezi kuvitenda.

Mwanaume mmoja nchini Kenya, Stephen Ngila Thenge (24), amediriki kumkata viganja vya mikono yote miwili mkewe ambaye wamedumu naye kwa muda wa miaka saba.

Thenge alitumia kisu kikali na kikubwa kusambaratisha viganja vya mikono ya mkewe huyo kwa kosa la kushindwa kumzalia watoto.

Licha ya kwamba tunasema kuwa na uzazi ni majaaliwa ya Mwenyezi Mungu, mwanamume huyu alishindwa kuvumilia mitihani aliyopewa na Mungu kwa kukosa mtoto, na hivyo kujikuta akigombana na mkewe mara kwa mara akimtuhumu kwanini hamzalii watoto katika kipindi chote cha miaka saba walichoishi pamoja.

Mkewe huyo, Jackline Mwende, kutoka Kijiji cha Kathama, Masii katika Kaunti ya Machakos, mikono yake ilikatwa Julai 24 mwaka huu.

Mbali na kukatwa viganja vya mikono, alipata majeraha usoni na kichwani. Hakuishia hapo mwanamume huyo pia alimjeruhi mkewe shingoni wakati wa purukushani za ugomvi.

Akisimulia jinsi tukio lilivyotokea Mwende anasema; “Kwa sababu ya kunituhumu kuwa sina uwezo wa kumzalia watoto, mume wangu aliamua kuondoka nyumbani na kwenda kuishi nisikokufahamu kwa muda wa takribani miezi mitatu.

“Mara baada ya kurejea juzi Jumamosi, alipofungua tu mlango akaniambia kuwa siku hiyo ilikuwa ni ya mwisho kwangu, akaanza kunishambulia kwa kutumia panga alilokuja nalo.”

Mwende anasema alijaribu kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani wafike kumsaidia, lakini haikuwezekana.

Anasema kuwa baada ya kipigo ndipo majirani wakaja lakini kila mtu alikuwa akiogopa kumshika kwa kuhofia huenda atakuwa amefariki kwa kuwa alikuwa na hali mbaya huku damu nyingi zikimtoka.

“Sijui kwa nini alikuwa akinilaumu kwamba sina uwezo wa kuzaa wakati mwaka jana tulikwenda hospitali kupima na mume wangu ndiye aliyegundulika kuwa na matatizo.

“Daktari alisema mume wangu ndiye aliyekuwa na tatizo… hakuwa na uwezo wa kunipa ujauzito, hata hivyo alitusisitiza kuwa tatizo hilo linaweza kutibiwa na kuisha,” anasema.

Mwende anabainisha kuwa baada ya majibu hayo, mumewe ambaye ni fundi wa nguo katika Mji wa Masii, alikataa kufuatilia matibabu huku akimtuhumu kuwa yeye ndiye mwenye matatizo.

“Yeye alikuwa hataki kutibiwa… lakini licha ya majibu ya daktari, bado aliendelea kuninyanyasa na kunipiga kila kukicha.

“Ila safari hii ndio ameamua kabisa kunijeruhi vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili wangu.

“Ameniumiza vibaya sehemu mbalimbali za mwili, nimeumia kichwani, usoni na hata sehemu za siri,” anasema Mwende.

Mwende anasema kuwa pamoja na maswahibu yote yaliyomkuta ameamu kumwachia Mungu ambaye anaamini kuwa atamlipia tena kwa wakati.

“Nilimpenda mume wangu kwa dhati lakini haya ndio malipo yake hivyo Mungu ndio atakayemuhukumu,” anasema.

Wakizungumzia kisa hicho, ndugu zake wanasema kuwa wanandoa hao walikuwa na matatizo siku nyingi na kwamba Mwende alitaka kumwacha mumewe lakini kiongozi mmoja wa dini alimshauri kumvumilia mumewe na kwamba ipo siku Mungu atashusha neema na malumbano hayo yataisha.

Aidha, baada ya kipigo hicho na kupatiwa matibabu hospitalini, Mwende amelazimika kwenda kuishi nyumbani kwa wazazi wake.

Wazazi hao ambao hawana kazi yoyote, kwa sasa wamekuwa na jukumu la kuhakikisha wanamhudumia mtoto wao mahitaji yote muhimu.

Baba yake, Samuel Munyoki, anasema hawana budi kumlea na kumtunza binti yao huyo kutokana na ndoa yake kuingia doa, hivyo wakimruhusu arejee kwa mumewe huenda akamwondoa kabisa duniani.

“Licha ya kwamba sina kazi, nitamlea mwanangu la sivyo nikimuacha arudi kwa mumewe ni sawa na kumruhusu atoweke duniani.

“Mtoto wangu sasa amepata ulemavu wa kudumu hivyo hata iweje hawezi kurudi kuwa kama zamani, lakini nitaomba amlipe fidia zikiwamo za matibabu aliyopata na mambo mengine kwani kwa sasa amepoteza kabisa ramani yake ya maisha,” anasema Munyoki.

Mwanamume huyo baada ya kumuumiza vibaya mkewe alikimbilia kusikojulikana lakini Polisi walifanya juhudi za kumtafuta na kumtia nguvuni siku ya Jumatatu akiwa Mji wa Machakosi.

Wanawake wengi nchini humo wamedai kuwa ni lazima wahakikishe haki inapatikana kutokana na kitendo cha ukatili kilichofanywa na mwanamume huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles