PARIS, Ufaransa
SHIRIKISHO la Soka la Ufaransa (FFF), limetangaza kumsimamisha mwamuzi Tony Chapron, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumpiga teke na kisha kumpa kadi nyekundu beki wa timu ya Nantes, Diego Carlos.
Uamuzi huo umefanyika baada ya Kamati ya Waamuzi ya ligi hiyo kukaa jana na kufanya tathmini kuhusu tabia aliyoonesha Chapron kabla ya kutoa uamuzi.
Tukio hilo lilitokea juzi wakati wa mchezo wa Nante dhidi ya Paris St. Germain wa Ligi Kuu Ufaransa.
Kabla ya tukio hilo, Chapron alionekana akikimbia na kujigonga kwa Carlos kabla ya kuanguka na video za televisheni zilimwonyesha akitaka kulipiza kisasi kwa kumtegea mguu wake mlinzi huyo.
Sekunde chache baada ya tukio hilo, Chapron alimwonesha Carlos kadi ya njano ambayo ilisababisha mchezaji huyo aoneshwe nyekundu kutokana na kuoneshwa kadi ya njano kipindi cha kwanza.
“Najua kuwa ni mwamuzi mzuri, lakini anahitaji kujiuliza,” alisema mshambuliaji wa Nantes, Valentin Rongier.
“Ikiwa tunafanya kitu kama hiki, tunaweza kusimamishwa kwa michezo 10.”
Rais wa Nantes, Waldemar Kita, alikiambia kituo cha Les Equipe: “Ni mshtuko. Nilipata jumbe 20 kutoka ulimwenguni kote zikiniambia kuwa mwamuzi huyu ni kichekesho. Ni nini unataka nikwambie? Kama nikizungumza sana nitaitwa na kamati ya maadili.”