30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mwalimu aliyemchapa mwanafunzi ahukumiwa kunyongwa hadi kufa

Na RENATHA KAPAKA – BUKOBA

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Bukoba imemuhukumu mwalimu Respikius Mtazangira kunyongwa hadi kufa baada ya kumkuta na hatia ya kusababisha kifo cha mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kibeta, Spelius Eradius (13), mwishoni mwa mwaka jana.

Katika hukumu hiyo iliyosomwa kwa saa mbili, kuanzia saa nne asubuhi hadi saa sita mchana, mahakama hiyo ilimwachia huru mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, mwalimu Harieth Gerald baada ya kutokutwa na hatia.

Walimu hao walidaiwa kuwa Agosti 27 mwaka jana walimuua Eradius baada ya kumpiga fimbo hadi kufa, wakimtuhumu kuiba mkoba wa mwalimu Harieth.

Akisoma hukumu hiyo jana, Jaji Lameck Mlacha alisema upande wa jamhuri ulithibitisha bila kuacha shaka baada ya mashahidi tisa kutoa ushahidi wao mahakamani.

Alisema alipata muda wa kuwasikiliza mashahidi wote tisa ambao wote walijiamini na hawakutetereka.

Jaji Mlacha alisema shahidi namba 2, 3, 4, 5, 6 na 8 wote walitoa ushahidi unaoendana na kesi iliyowasilishwa mahakamani hapo.

Alisema kifo cha Eradius kilitokana na kupigwa kwani siku hiyo alifika shuleni salama, lakini baada ya pochi ya mwalimu Harieth kupotea, mshtakiwa namba mbili alimchukua na kumpeleka kwa mwalimu wa nidhamu ili amalize swala la pochi yake kupotea.

Jaji Mlacha alisema baada ya kumkabidhi kwa mwalimu Mtazangira, mshtakiwa namba moja alianza kumpiga mwanafunzi huyo katika sehemu mbalimbali za mwili hadi kusababisha kifo chake.

Alisema ushahidi uliotolewa na madaktari wawili waliopata fursa ya kuchunguza mwili wa marehemu,  unaonesha kuwa mwanafunzi alikufa kwa kupigwa fimbo katika maeneo mbalimbali ya mwili.

Jaji Mlacha alisema ushahidi wa madaktari hao ulienda sawa na ule wa wanafunzi waliofika mahakamani hapo kutoa ushahidi na kudai kuwa mwalimu Mtazangira alimpiga mwanafunzi huyo kwa fimbo isiyokuwa ya kawaida.

Miongoni mwa sababu zilizomfanya Jaji Mlacha kutoa hukumu, washtakiwa wote hawakatai kumfahamu marehemu, hawakatai kuwa siku mauti yanamfika marehemu alikuwa shuleni na afya njema. 

Hawakatai alituhumiwa kuiba pochi na kupigwa, hawakatai kuwa sasa ni marehemu, hawakatai kuwa mwili wa marehemu ulipatikana ukiwa na majeraha.

Mtazangira pia hakatai kuwa alimpokea mtoto na kumpiga viboko sita, pia hakatai kuwa alikutwa njiani akiwa na mtoto.

Pia Herieth hakatai kuwa alipokelewa vitu alivyokuwa navyo na wanafunzi, hakatai kwamba alikwenda kwa mwalimu mkuu kutoa taarifa kuwa alipokelewa pochi na 

hakatai kuwa alimwomba Mtazangira kumsaidia kumwadhibu.

Jaji huyo alimaliza kutoa hukumu hiyo ya mauaji ya kesi namba 56 ya mwaka 2018 kwa kuwataka walimu na watu wote kupitia kanuni, na sheria za elimu ili kufanya kazi yao kwa weledi.

Pia aliutaka umati uliohudhuria kesi hiyo kusema ukweli mbele ya mahakama bila kuzungusha.

AANGUKA KIZIMBANI

Baada ya hukumu hiyo, mshtakiwa huyo namba moja alianguka chini huku akibubujikwa na machozi.

Baada ya kuanguka, kizimba kilizungukwa na askari na watu kuambiwa watoke nje ya ukumbi wa mahakama, lakini baadaye alipitishwa mlango wa nyuma na kuwaacha solemba mamia ya wananchi waliokuwa wanasubiri kumwona.

ASOMA BIBLIA KABLA YA HUKUMU

Kabla ya kuanza kusomwa kwa hukumu, mwalimu Mtazangira aliyehukumiwa kunyongwa, alitumia dakika takribani tatu kusoma Biblia aliyokuwa ameishika.

Wakati huo mtuhumiwa namba mbili aliyekuwa ameketi kwenye benchi la mbele la mahakama hiyo, alikuwa ametulia wakati mwingi akitazama chini.

Wakili wa Serikali Mkuu, Hashimu Ngore, alisema upande wa jamhuri umeridhishwa na hukumu hiyo na kwamba kesi haikulenga kupotea kwa pochi bali nani alimpiga mwanafunzi hadi kufa.

Ngore alisema katika upande wa mashahidi, mwalimu Harieth hakuna alikotajwa kumpiga mwanafunzi tofauti na pochi yake kupotea.

Alisema mwalimu Mtazangira ndiye aliyetajwa kumpiga mwanafunzi katika sehemu mbalimbali za mwili, hivyo mahakama haikuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa namba mbili.

Ngore alisema kesi hiyo ilikuwa na masilahi mapana ya jamii na kwamba siku zote ilipokuwa ikiendeshwa watu walifurika na walitamani mahakama itende haki.

Kwa upande wake, wakili mtetezi wa mshtakiwa namba mbili, Aron Kabunga, aliishukuru mahakama kwa kutenda haki na kuendesha kesi hiyo haraka.

Alisema kesi hiyo ilikuwa na nguvu katika jamii ambayo ilitamani haki itendeke haraka juu ya tukio hilo la mauaji.

Kesi hiyo imesikilizwa kwa mwezi mmoja tu tangu Februari 6, mwaka huu hadi jana hukumu ilipotolewa.

Kabla ya Jaji Mlacha kutoa hukumu, alisema uchunguzi wa daktari bingwa wa uchunguzi na vifo, Kaima Jackson kutoka Hospitali ya Bungando Mwanza, ulibaini asilimia 95 ya majeraha ya nje ya mwili wa marehemu yalisababishwa na kitu chenye ncha butu.

Alisema ndani ya mwili marehemu alionekana kuwa na majeraha ya kitu kisichokuwa cha kawaida.

Spelius Eradius alifariki Agosti 27 na kuzikwa Septemba 2018 katika Kijiji cha Mbunda, Kata ya Mbunda, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

TAKWIMU UKATILI

Juni 16, 2018 katika kilele cha Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo kitaifa ilifanyika mkoani Arusha, Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi vinara kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kuliko uovu unaofanywa kwenye ujambazi.

Takwimu zilizowasilishwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, zinaeleza watoto 41,000 walifanyiwa ukatili na kati yao 3,467 kwa kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka juzi.

Lakini pia, Idara ya Ustawi wa Jamii wizarani hapo, ilieleza kuwa asilimia 60 ya ukatili dhidi ya watoto unafanyika nyumbani, asilimia 35 ni shuleni na iliyobaki ni maeneo mengine.

VIBOKO MARUFUKU SHULENI

Novemba mwaka jana bungeni, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, William ole Nasha, alisema kuna waraka uliotolewa kisheria kwa wadau wa elimu kuhusu uchapwaji wa viboko.

Alisema waraka huo unasema utaratibu wa uchapwaji viboko kwa wanafunzi, kwanza kibali kiombwe na kutolewa kwa maandishi.

“Haitakiwi vizidi viboko vinne, hairuhusiwi kwa mwalimu yeyote yule kuchapa viboko, bali ni mwalimu mkuu tu, na lazima kiombwe kibali cha kufanya hivyo.

“Ni marufuku mwalimu yeyote kumchapa mwanafunzi kinyume na taratibu na sheria, lakini vile vile ni marufuku mwalimu yeyote kutembea na viboko kwa lengo la kumchapa mwanafunzi, kufanya hivyo ni kuvunja sheria na hatua zitachukuliwa,” alisema Ole Nasha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles