NAIROBI, KENYA
MIVUTANO katika Chama tawala cha Jubilee umezidi kutokota huku Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, akitangaza mipango ya kuunda chama kipya kitakachotetea maslahi ya jamii za Mlima Kenya.
Kuria alieleza wazi kwamba uamuzi uliochangia kuvunjwa kwa chama cha zamani cha The National Alliance (TNA), ambacho Rais Uhuru Kenyatta alikitumia kuwania urais mwaka wa 2013, uliacha Mlima Kenya bila namna ya kujitetea vilivyo kisiasa.
TNA kilivunjwa pamoja na vyama vingine vya muungano uliokuwepo wa Jubilee, kikiwemo Chama cha United Republican Party (URP) kilichoongozwa na Naibu Rais William Ruto, kuunda Chama cha Jubilee ambacho kilishinda urais mwaka 2017.
Kauli ya Kuria imetokea wakati ambapo joto la kisiasa linazidi kuiandama Jubilee baina ya upande unaounga mkono azimio la Dk. Ruto kuwania urais mwaka 2022, maarufu ‘Team Tangatanga’, na kundi jingine linalopinga kampeni za mapema maarufu kama ‘Team Kieleweke’.
Wandani wa Dk. Ruto wamekuwa wakidai kuna njama zinazoendelezwa kumzuia Ruto kufanikiwa katika azma ya kuwa rais mwaka 2022 ikiwa ni pamoja na kuivuruga Jubilee.
“Tulikosea wakati tulipovunja chama chetu cha The National Alliance kwa sababu Jubilee ni chama kisicho na mwelekeo ambacho hatuwezi kukitumia kufanya mipango yetu ya Mlima Kenya.
“Nitasajili chama kipya cha siasa ambacho kitawapa viongozi wa Mlima Kenya nafasi ya kufanya mipango kuhusu masilahi yetu ya siku za usoni serikalini,” alisema Kuria.
Alikuwa akizungumza katika Kanisa Katoliki la Sabasaba, Kaunti ya Murang’a ambapo aliandamana na viongozi wengine wa Jubilee.
Viongozi hao ni pamoja na Mbunge wa Kandara, Alice Wahome na mwenzake wa Maragua, Mary Waithira pamoja na Seneta wa Murang’a, Irungu Kang’ata.
Kang’ata alikiri siasa zinazoendelezwa zimesababisha mgawanyiko wa viongozi na sasa chama kinaelekea mahali pabaya.
“Chama chetu kinaelekea pabaya kwa sababu pande mbili za Tangatanga na Kieleweke zinasababisha chuki miongoni mwa wale wanaochukuliwa kuwa wapinzani wao,” alisema.
Suala la iwapo Dk. Ruto atatumia Chama cha Jubilee kuwania urais 2022 limekuwa kwenye ndimi za baadhi ya wafuasi wake na wachanganuzi wa siasa kwa muda mrefu hasa tangu mwafaka wa Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga upatikane.
Wakati mmoja, ilifichuka kwamba viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais walisajili vyama vipya na kushukiwa kuwa hayo yalikuwa maandalizi ya kujitafutia makao salama endapo Dk. Ruto ‘atasalitiwa’ na viongozi wa Jubilee wanaotoka Mlima Kenya.
Wahome alitoa wito kwa Rais Kenyatta kuingilia kati ili kutuliza hali chamani na kuepusha mashua ya Jubilee kuzama katika dhoruba kali inayoshuhudiwa.
“Tulipiga kura kwa wingi kuwachagua Uhuru Kenyatta na Dk. Ruto na tunamtegemea kiongozi wa chama kudhibiti hali iliyopo chamani kwa sasa,” akasema