Asha Bani, Dar es Salaam
Mabasi 29 ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (Udart) kati ya 140, yameharibika kutokana na mvua zilizonyesha mfululizo wiki iliyopita na kusababisha madhara katika karakana kuu iliyopo Jangwani jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 7, Ofisa Habari Udart, Deus Bugaywa amesema mvua zilizonyesha Mei 4 mwaka huu zimeleta madhara makubwa kutokana na eneo kuu la maegesho Jangwani kujaa maji na matope jambo lililosababisha kukwama kwa magari na shughuli nyingine kushindwa kuendelea kufanyika.
“Kwanza ukuta wetu uliopakana na Mto Msimbazi ulianguka na kusababisha maji yote yaliyokuwa yanatoka katika mto huo kutiririka kwenye maegesho ya magari.
“Hata hivyo, kuna mpango endelevu kuhakikisha tunapata eneo jingine la maegesho hayo ya magari vinginevyo kutakuwa na hasara za mara kwa mara,” amesema Bugaywa.
Pamoja na mambo mengine, amesema kwa sasa Udart wana magari 140 na mengine 70 bado yako bandarini ambapo mradi unatakiwa kuwa na magari 300 hivyo ni lazima kutafuta eneo kubwa, zuri na la kudumu.